Kamishna Mhifadhi Misitu wa TFS nchini Tanzania Profesa Dos Santos Silayo, Mkuu wa Idara ya Masoko na Utalii wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Anna Lawuo (katikati) aliyekuwa akimwakilisha Kamishna Mhifadhi Misitu wa TFS nchini Tanzania Profesa Dos Santos Silayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa Kurehesha mikoko:Je tupande au tusipande wa Shirika la Wetlands International , sambamba na sherehe za Maadhimisho ya siku ya Mikoko Duniani.Kulia ni Mkurugenzi wa Wetlands International Kanda ya Afrika Mashariki na Ethiopia Julie Mulonga na kushoto ni Mratibu wa Programu-Wetlands International Tanzania Clare Haule.
Mkurugenzi wa Wetlands International Kanda ya Afrika Mashariki na Ethiopia Julie Mulonga akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Kurejesha mikoko:Je, Tupande au tusipande wakati wa maadhimisho ya siku ya Mikoko duniani ambapo wadau mbalimbali wa mazingira wamehudhuria.
Wadau wa mazingira kutoka taasisi na mashirika mbalimbali wakiwa kwenye majadiliano yaliyohusu kuweka mikakati ya uhifadhi na utunzaji mikoko wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mikoko Duniani sambamba na uzinduzi wa mradi wa Je, tupande au tusipande unaosimamiwa na Shirika la Wetlands International.
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) umewapongeza viongozi wa Wetlands International kwa juhudi inazochukua katika kuhakikisha mikoko iliyopo nchini inatunzwa na kuhifadhi kupitia mikakati na mipango mizuri waliyoiweka.
TFS imetoa pongezi hizo leo Julai 26,mwaka 2021 jijini Dar es Salaam wakati Wetlands ilipowakutanisha wadau kutoka taasisi na mashirika mbalimbali wa mazingira kujadili kwa pamoja kuhusu uhifadhi wa mikoko hasa kwa kuzingatia kila ifikapo Julai 26 ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya mikoko duniani.
Sambamba na kuadhimisha siku, hiyo Wetlands International imezindua programu ya kurejesha mikoko kupitia kauli mbiu inayosema hivi Je, tupande au tusipande?
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Mhifadhi Misitu wa TFS nchini Tanzania Profesa Dos Santos Silayo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko katika Utalii wa TFS Anna Lawuo amesema Wetlands wametoa mchango mkubwa kwenye kuhifadhi mikoko kupitia programu ambazo wamekuwa wakizisimamia.
"Shirika hili la Wetlands International limejitahidi na leo limekuja na uzinduzi wa mradi mwingine unaitwa Je, Tupande au tusipande ukiwa unaaminisha ulazima wa kupanda mikoko.Pia tufahamu sio lazima uipande mikoko kwani kuna njia nyingine mbadala unayoweza kuitumia kurejesha uoto wa asili wa mikoko na ukaipata kwa haraka zaidi.
"Kwa hiyo ndio maana wanasema tafiti mbalimbali ambazo zimefanyika delta ya Rufiji wameona njia gani ni muhimu au za haraka za kurejesha hiyo mikoko asili, delta ya Rufiji hapo mwanzoni ilikuwa ni eneo lenye mikoko mingi kuliko maeneo mengine.
"Japo mikoko hii ipo katika ukanda wa bahari ya Hindi kuanzia mkoani Tanga mpaka mkoani Mtwara lakini delta ra Rufiji ndio kuna eneo kubwa la mikoko.Awali kulikuwa na hekta 53,000 lakini kwa tafiti ambazo zimefanyika zinaonesha zimepungua na kubakia hekta 46,000 tu.
"Sasa ukiangalia utaona ni kiasi cha hekta 7,000 zimetoweka kabisa hazipo na tukumbuke urejeshaji wa uoto wa asili wa mkoko sio sawa na sehemu nyingine,unaweza kupanda robo heka hata kwa siku tatu usimalize hata mkiwa watu 10 au 20 , kwani inapandwa kwenye tope jingi na hivyo kuwa ngumu,"amesema.
Aidha amesema eneo la mikoko linachangamoto nyingi lakini Wetlands International wamejitahidi na sasa wamekuja na njia mbadala kuhakikisha mikoko inaendelea kuwepo.Ameongeza kuna aina tisa za mikoko na kwa Tanzania kwa tafiti zilizofanyika lakini sio sehemu zote zinaweza kuota kwa kupndwa miche, kwa hiyo kuna njia nyingine mbadala ya kufanikisha kupatikana kwa mikoko.
"Tunataka elimu kuhusu njia mbadala ya mikoko ifike kwa jamii nzima ya Watanzania na hasa wale wanaoishi ufukweni maana ndio wanuifaka wa kwanza wa mikoko ili wajue ni jinsi gani wanaweza kurejesha mikoko ya asili.
"Lakini eneo hili la mikoko linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo baadhi ya wananchi kuiharibu kwa kigezo cha kuadaa mashamba ya mpunga na wengine kwa ajili ya mashamba ya chumvi.Hivyo rai yangu hasa delta ya Rufiji tunaomba watu wasiharibu mikoko kwa ajili ya mashamba ya mpunga.Watafute njia nyingine mbadala ili sote kwa pamoja tuendelee kuitunza mikoko iliyopo,"amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Wetlands International Kanda ya Afrika Mashariki na Ethiopia Julie Mulonga amesema kabla yao kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)kuweka mpango mkakati wa kuhifadhi mikoko kulikuwa na uharibifu mkubwa mikoko na hasa delta ya Rufiji.
"Lakini kwa sasa kuna mipango na mikakati mizuri ambayo wameiweka kwa kushirikiana na TFS kuhakikisha mikoko inatunzwa na kuhifadhiwa.Huko nyuma watu walikuwa wanakata mikoko sana lakini huu mpango mkakati unasaidia watu kujipanga vizuri katika kuirejesha hiyo mikoko.
"Na kitu muhimu Wetlands kwa kushirikiana na wadau tunatumia sayansi kufanya tafiti kujua kiasi gani cha mikoko inatakiwa kupandwa na kiasia gani inatakiwa kukatwa.Jambo jingine ambalo Wetlands International tunaeleza huwezi kuondoa watu wanaoishi maeneo yenye mikoko kwani wanaitegemea kwa kiasi kikubwa wakiwemo wavuvi.
"Kwa hiyo tunachokifanya ni kuhakikisha kuna kuwa na njia nyingine za kujiendeleza ili usiwatoe kwenye mikoko halafu waathirike kiuchumi, hivyo kwa Tanzania wameweka ahadi ya kuhifadhi na kutunza mikoko ili iongezeke,'amesema.
Ameongeza tu na si mikoko peke yake bali , imeweka mikakati ya kuhakikisha inahifadhi misitu iliyopo pamoja na kuendelea kupanda aina ya miti mbalimbali.
Kuhusu faida za uwepo wa mikoko, Mulonga amesema inafaida nyingi lakini faida ya kwanza inauwezo wa kunyonya kaboni inayozalishwa na binadamu kupitia shughuli wanazozifanya."Watu wengine wanaangalia mikoko halafu hawaoni faida, mikoko inafaida nyingi sana , ndio inayonya hewa ukaa kwa wingi ukilinganisha na miti mingine."
Ameongeza faida ya pili kuna watu wanategemea hiyo mikoko katika kufanya shughuli zao za kiuchumi na kujipatia kipato , hata samaki wanazaliana kwa wingi kwenye mikoko."Halafu ukiona mikoko katika fukwe ya bahari inasaidia kuzuia mmomonyo wa ardhi."
Ametoa mwito kwa jamii kuwa ni lazima wapande mikoko huku akifafanua mikoko sio inapandwa kwenye maeneo yote lakini kuhakikisha yale maeneo ambayo mikoko inapandwa na kukubali basi ikandwa, ikatunzwa na kuhifadhiwa.
Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani Kanali Ahmed Abbas amekiri ni kweli miti ya mikoko imekuwa ikipotea kutokana na shughuli za kibinadamu lakini Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuirejesha ikiwemo ya kuweka mazingira rafiki katika uvunaji kwa maana kuna kipindi uvunaji na kipindi ambacho si cha uvunaji.
"Hivyo tumekuwa tukipeleka elimu kwa wananchi kuhusu uvunaji endelevu wa mikoko kwa ajili ya matumizi ya leo na baadae, kinachosababisha upotevu wa mikoko ni shughuli za kibinadamu ambazo nyingi tunazifahamu, kuna ukataji wa mikoko uliokithiri, lakini kuna mifugo inayoingia maeneo ya miti ya mikoko na kilimo cha mpunga katika maeneo hayo,"amesema.
Amesema jitihada zinafanyika kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulima kilimo rafiki pamoja na ufugaji uliorafiki katika maeneo ya mikoko huku akieleza kuhusu mapokeo ya wananchi amesema wanakosa fursa ya kuelimishwa na wakielimishwa wanaelewa, hivyo kwa sasa mapokeo ni mazuri na wanaelewa umuhimu wa mikoko na faida zake kupitia elimu ambayo wanaipata.
Awali Mratibu wa Programu-Wetlands International Tanzania Clare Haule amesema kwa kipindi cha miaka minne ambacho wamekuwepo nchini wamekuwa wakitekeleza mradi mingine kadhaa ukiwemo mradi wa Mangrove Capital Africa ambao unatekelezwa katika Bara la Afrika na kwa wakati huu huo unatekelezwa katika delta ya Saloum huko nchini ya Senegal na Tanzania, ingawa kwa siku za mbeleni wanategemea kufanya shughuli zao katika nchi ya Kenya kwenye Mji wa Lamu.
"Mradi huu wa Mangrove Capital Afrika unaolengo la kufanya urejeshaji wa misitu ya mikoko takribani hekari milioni moja na wakati tukifanya hayo tunategemea kufikia jamii ipatayo wananchi milioni mbili,sasa ukija kwa delta ya Rufiji kupitia mradi huu tunatarajia kufanya uhifadhi na urejeshaji wa mikoko takribani ekari 2000, pamoja na mradi huu pia tuna miradi mingine ambayo tunaitekeleza kwa kushirikiana na wadau wengine na mashirika rafiki.
"Kama ambavyo tumewaeleza katika taarifa mbalimbali , leo ni siku ya mikoko duniani ambayo husherehekewa kila Julai 26 katika dunia nzima na maadhimisho haya yameanza tangu mwaka 2016 na tangu wakati huo tumekuwa tukiadhimisha siku hiyo.Kwanini tuadhimishe siku ya mikoko, ni kwasababu tunaelezwa takribani asilimia 67 ya mikoko duniani imeshapotea na kila mwaka asilimia moja ya mikoko inaendelea kipotea, hivyo kwa kutumia siku ya leo wadau wanajadiliana kwa pamoja hatua za kuchukua kuokoa upotevu huo."Amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani Kanali Ahmed Abbas akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mikoko Duniani ambapo ametumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa jamii kutunza mazingira.
Baadhi ya wadau wa uhifadhi wa mazingira wakiwa makini kufuatilia majadiliano wakati wa maadhimisho hayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wetlands International -Tanzania John Yonazi akifafanua jambo kuhusu jitihada ambazo zinafanywa na shirika hilo katika kuweka mikakati ya kushirikiana na wadau kuhakikisha mikoko inaendelea kuwepo.
Wadau wakifuatilia majadiliano.
Mratibu wa Programu-Wetlands International Tanzania Clare Haule akisisitiza jambo kwa wadau wa mazingira wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mikoko duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Julai 26 ya kila mwaka.
Msanii Mrisho Mpoto a.k.a Mjomba Mpoto akitoa burudani wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mikoko Duniani.Mpoto ametumia nafasi hiyo kutoa ujumbe wenye kuhamasisha jamii ya Watanzania kupanda mikoko kwani faida zake ni nyingi.
Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Utalii wa TFS Anna Lawuo ambaye amemwakiisha Kamishna Mhifadhi Misitu wa TFS nchini Tanzania Profesa Dos Santos Silayo,aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mikoko pamoja na uzinduzi wa programu ya Kurejesha mikoko:Je, tutapande au tusipande inayosimamiwa na Shirika la Wetlands International.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wetlands International -Tanzania John Yonazi (aliyekaa)akijadiliana jambo na Mratibu wa Programu-Wetlands International Tanzania Clare Haule.
Wasanii wa kundi la Mrisho Mpoto wakitoa burudani kwa wadau wa mazingira.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...