Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
JULAI 25, 2021 Siku ya Jumapili, Taifa la Tanzania litaingia katika historia nyingine katika tasnia ya Soka kwa kuzikutanisha Klabu za Simba SC dhidi ya Young Africans SC katika mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports Federation Cup msimu wa 2020-2021 mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Mara kwa mara timu hizo zimekutana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam katika Mashindano mbalimbali ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA, lakini mara hii timu hizo zinakutana Kigoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Magharibi mwa Tanzania.
Yanga SC na Simba SC zimewahi kukutana mara ya mwisho kwenye Fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na Watoto wa Jangwani, Young Africans kuibuka na ushindi wa Mikwaju ya Penalti 4-3 dhidi ya Simba SC, Januari 13, 2021, licha ya timu zote kutokuwa na Wachezaji wake wote katika Vikosi vyao (Full Mkoko).
Lakini timu hizo Julai 3 mwaka huu zilikutana mbele ya Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika dimba la Mkapa, Dar es Salaam kwenye Ligi Kuu (VPL) ambapo Yanga SC kama kawaida yao mbele ya Marais ilitoa kichapo cha bao 1-0 kwa bao la Kiungo Zawadi Mauya na kuifanya Simba SC kufedheheka mbele ya Viongozi hao wa nchi.
Safari hii zikiwa zinakutana kwenye Fainali ya FA Kigoma, Mwisho wa Reli, timu hizo leo siku ya Alhamisi Julai 22, 2021 tayari zimetua kwenye Uwanja wa Medani mkoani Kigoma kwa Mwewe yaani Ndege kwa ajili ya mtanange huo wa Kihistoria ambao wanapokutana Mafahari hao wawili nchi nzima inasimama kushuhudia mbungi lao.
Ukiachana na timu hizo kukutana visiwani Zanzibar kwenye Fainali za Michuano ya Kombe la Mapinduzi, Simba na Yanga pia zimewahi kukutana katika mikoa ya Morogoro kwenye dimba la Jamhuri na Mkoani Mwanza katika dimba la CCM Kirumba.
Mara ya mwisho kwenye Kombe la FA, miamba hiyo ya Soka ilikutana kwenye Nusu Fainali ya Michuano hiyo msimu wa 2019-2020 ambapo Wekundu wa Msimbazi waliibuka kidedea kwa kuwaadhibu Wananchi bao 4-1 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Wakati Yanga SC kupitia kurasa zao za Mitandao ya Kijamii kutoa taarifa ya kumkataa Mwamuzi wa Pambano hilo la Fainali siku ya Jumapili, Ahmed Arajiga, Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu amewatuliza Wapenzi, Mashabiki na Wanacha wa Klabu hiyo kwa kile kinachoendelea Mitandaoni kikitajwa kuwa mivurugano ndani ya Klabu yao.
Yote kwa Yote! Mashabiki wa Soka nchini wana hamu na shauku tele kushuhudia pambano hilo, Je nani kuibuka Bingwa wa Michuano ya FA msimu huu…???
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...