Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman
Masoud Othman, ameuhimiza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar kuzingatia maslahi na thamani ya walimu katika utekelezaji wa
majukumu yao kwa lengo la kukuza ubora katika sekta ya elimu nchini.
Mheshimiwa
Othman ameyasema hayo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika
ujenzi wa banda la kusomea katika Skuli ya Mtoni Kidatu, Wilaya ya
Magharibi 'A' Unguja.
"Tutakapowawekea
mazingira bora ya kazi, heshima, mishahara mizuri pamoja na kuthaminiwa
katika kupata huduma za kijamii, tutawafanya walimu wetu kuwa na hamasa
na kuukuza utendaji wao,”alieleza Makamu wa Kwanza wa Rais.
Mheshimiwa
Othman amesema walimu wamekuwa wakipata changamoto mbali mbali katika
utekelezaji wa kazi zao, hivyo kuwajengea mazingira wezeshi ya kielimu
na hata katika upatikanaji wa huduma za kijamii kutawapa uwezo wa
kufanya kazi zao kwa ufanisi.
"Hapo
zamani mtu aliyekuwa na heshima kubwa katika kijiji ni mwalimu. Hivyo
serikali hatuna budi kuhakikisha tunamrudisha mwalimu kuwa mtu mwenye
heshima na hadhi katika jamii,” alifafanua Mheshimiwa Othman.
Aidha
ameipongeza Kamati ya Wazee wa Skuli hiyo pamoja na wadau wengine wa
elimu kwa juhudi zao kubwa walizozichukua katika kuhakikisha banda hilo
linasimama pamoja na kuwaomba kuendelea kushirikiana na Serikali
kuongeza nguvu na kuboresha miundombinu mbalimbali ya elimu nchini.
Mbali
na hayo, Mheshimiwa Othman ameahidi kuzifanyia kazi changamoto mbali
mbali zilizopo katika maeneo hayo kwa lengo la kukuza maendeleo ya
wananchi.
Naye Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mheshimiwa Simai Mohammed Said,
alisema wizara bado inaendelea kutafuta fursa mbalimbali katika
kuhakikisha matatizo yanayoikumba sekta ya elimu nchini yanamalizika
pamoja na kuwaomba wazee kutenga muda wa kuwashughulikia watoto wao
katika masomo wanapokuwa majumbani ili kukuza ufaulu nchini.
Akiwasilisha
taarifa ya ujenzi wa banda hilo mjumbe wa kamati ya ujenzi ya skuli
hiyo, Bwana. Juma Shaame Khamis, ameiomba Serikali kuwasaidia kumalizia
hatua iliyobakia ikiwemo utiaji wa plasta, sakafu na madirisha.
Mbali
na hilo, Kamati hiyo imeiomba serikali kuwajengea jengo jengine
litakalowasaidia wanafunzi wa Sekondari ambao kwa sasa wanalazimika
kutumia madarasa ya wanafunzi wa Msingi kutokana na tatizo la uhaba wa
madarasa linaloikabili skuli hiyo.
Takriban shilingi milioni ishirini na tatu zimetumika katika ujenzi wa banda hilo lenye madarasa sita na ofisi mbili za walimu.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...