Charles James, Michuzi TV
UKIZINGUA Nakuzingua! Ni kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo amekua akiisema akimaanisha mtumishi au mtendaji yeyote wa umma ambaye atafanya kazi na sheria na utaratibu basi atachukuliwa hatua.
Kauli hiyo imetumika leo na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso baada ya kumsimamisha kazi Ofisa Ugavi wa Wizara ya Maji, Victor Kaphipa ambaye kwa sasa kituo chake cha kazi ni Bonde la Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.
Hatua hiyo ya Waziri Aweso imetokana na kile alichodai kuwa Ofisa huyo amekua akifanya udalali ndani ya Wizara ya Maji na hivyo kuchafua taswira ya Wizara katika kuwahudumia watanzania.
Akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha watendaji wa Wizara ya Maji na taasisi zilizo chini yake katika kada ya manunuzi na ugavi, uhasibu na wakaguzi wa ndani, Waziri Aweso amesema hawatosita kumchukulia hatua mtumishi yeyote ambaye atakua na nia ovu ya kuichafua Serikali inayoongozwa na Rais Samia.
" Kuna mtu anaitwa Khaphipa yupo hapa?asimame, hayupo? huyu amekuwa dalali ndani ya wizara, simtaki katika wizara yetu ya maji na namsimamisha kazi kuanzia leo," Amesema Waziri Aweso.
Amefichua kuwa Rais Samia alimuita na kumueleza nia na azma yake ya kuhakikisha kuwa anamaliza changamoto ya Maji kwa wananchi na hivyo kuwataka watumishi na watendaji hao kushirikiana pamoja kuweza kutimiza ndoto ya Rais ya kuwatua watanzania ndoo kichwani.
" Nawaibia Siri Rais aliniita akaniambia Serikali kwa miaka mitano iliyopita iliwekeza nguvu zake katika sekta ya Afya na wote tumeona mafanikio makubwa katika ujenzi wa Hospitali za Kanda, Rufaa, Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati kila kona. Azma ya Rais kwa Awamu hii ni kupunguza shida ya maji kwa watanzania.
Ni vema tufanye kazi kama wanajeshi haiwezekani Rais yeye kiu yake ni kumaliza shida ya maji halafu sisi wenye Wizara husika tuwe kikwazo kwake, ni lazima tujipange maana tukishindwa kujipanga wenyewe tutapangwa," Amesema Aweso.
Amesema kwa maelekezo hayo ya Rais Samia ni wazi kwamba hawatakuwa tayari kumvumilia mtendaji yeyote ambaye ataonyesha dhamira ya kuwakwamisha na kwamba hawako tayari kuona viongozi wao wa ngazi ya juu akiwemo Rais wakisema na kunung'unikia wizara hiyo kila wakati na kuifanya kuwa wizara ya kusemwa semwa wakati wote.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nadhifa Kemikimba amemshukuru Waziri Aweso kwa kutoa kibali cha kufanyika kwa kikao hicho chenye lengo la kuwajengea uwezo watendaji wa kada ili kuongeza ufanisi kwenye Wizara hiyo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nadhifa Kemikimba akizungumza kwenye kikao cha pamoja na watendaji wa kada za Uhasibu Uafisa Ugavi na Wakaguzi wa ndani kutoka Wizara ya Maji na taasisi zake Nchi nzima.
Watumishi na Watendaji wa Wizara ya Maji na taasisi zilizo chini yake kutoka kada za Uhasibu, Uafisa Ugavi na Wakaguzi wa Ndani wakimsikiliza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso(hayupo pichani) wakati wa kikao cha pamoja kilichofanyika leo jijini Dodoma.
Waziri
wa Maji, Jumaa Aweso akiwa katika picha ya pamoja na watendaji Wakuu wa
Wizara yake na baadhi ya Watendaji wa kada za Uhasibu, Uafisa Ugavi na
Wakaguzi wa ndani mara baada ya kufungua kikao kazi cha pamoja jijini
Dodoma leo.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...