Akikabidhi hundi hiyo kwa waandaaji wa mbio hizo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa Masoko, Mawasiliano na Mahusiano Benki ya KCB Tanzania, Bi Christina Manyenye alisema udhamini huo unalenga kuunga mkono jitihada za waandaji wa mbio hizo pamoja na serikali kwa ujumla katika kuhamasisha michezo na utalii wa ndani hapa nchini.
“KCB tunafuraha kwa mara nyingine kushiriki kikamilifu kwenye mbio hizi. Tumekuwa tukiguswa sana na masuala ya kimichezo sababu tunaamini ustawi wa sekta yetu ya benki unategemea sana uimara wa wanananchi katika kujenga uchumi wao na ili hilo lifanikiwe tunahitaji kuwa na watu wenye utimamu kiafya na kiakili. Michezo ni moja ya namna bora kabisa katika kujenga afya ya wateja wetu na pia kuburudika,’’
“Ni kutokana na ukweli huo ndio sababu KCB Tanzania hatutaishia tu kuwa sehemu ya wadhamini wa mbio hizi bali pia tutashiriki kikamilifu kwenye mbio hizi hususani zile za KM 10 ambazo zitafahamika kama ‘KCB Bank Rock City Corporate Challenge’ na tutakimbia sambamba na wadau wetu mbalimbali wakiwemo wateja wetu…tunawakaribisha sana, tukutane Mwanza Oktoba 24,’’ alisisitiza.
Pamoja na benki hiyo, tayari mbio hizo zimefanikiwa kuungwa mkono na wadau kadhaa wakiwemo kampuni za TIPER, Pepsi, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),Kampuni ya Uhandisi ya Magare, Unilever, NSSF, Hospitali ya Bugando, CF Hospital, Garda World, Maji ya Uhai, Azam TV, Rock City Mall, Hotel Farm, EF Outdoor, The Cask na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) cha Mwanza.
Bi Shose aliongeza kuwa ili kutangaza utalii wa ndani benki hiyo itaendelea kushirikiana na waandaaji wa mbio hizo kuhakikisha zinafanikiwa kuvutia zaidi washiriki kutoka ndani na nje ya nchi ambao ujio wao jijini humo hautaishia katika kuimarisha sekta ya utalii pekee bali pia utafungua milango ya mahusiano ya kibiashara kwa wakazi wa jiji hilo.
“Zaidi nitoe wito kwa washiriki wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi wajitokeze kwa wingi jijini Mwanza ili kwa pamoja tufurahie mandhari nzuri ya jiji la Mwanza, watembelee vivutio vya utalii Kanda ya Ziwa pamoja na kutafuta fursa mpya za kibiashara katika ukanda huo.’’ Alisema.
Akizungumza baada ya kupokea hundi hiyo, Mratibu wa Mbio za Rock City Marathon Bw Kasara Naftal pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa kuunga mkono mbio hizo, alisema ushiriki wa benki ya KCB inayoheshimika ndani nan je ya nchini utasaidia kuendelea kuzitangaza mbio hizo kimataifa.
“Ushiriki wa benki ya KCB iliyojijengea heshima kubwa kupitia huduma zake ndani na nje ya mipaka ya nchi utatusaidia pia kuvutia wadau na washiriki kutoka nje ya nchi, hatua ambayo ni muhimu katika kufanikisha agenda yetu ya kutangaza utalii wa ndani husani kanda ya Ziwa,’’ alisema.
Alisema maandalizi ya mbio hizo yanaendelea vizuri huku akibainisha kuwa ubora wa vifaa (Kits) kwa ajili ya washiriki wa mbio za mwaka huu ikiwemo medali na fulana unatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa washiriki.
“Zaidi tunashukuru pia kuona kwamba viongozi mbalimbali wa kiserikali pamoja na wadhamini na wadau wetu wengine wakiwemo wadau wetu wote watashiriki kikamilifu kwenye mbio hizi.’’ alisema
“Tunatarajia kuwa na washiriki zaidi ya 3000 wakiwemo wakimbiaji wa kimataifa, wakimbiaji kutoka mashirika mbalimbali, wanafunzi sambamba na wenzetu wenye ualbino watakaoshiriki mbio za km 5.’’ Alitaja.
Alisema usajili wa mbio hizo unaendelea kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya mbio hizo pamoja na njia ya simu.
Naye Afisa Biashara, Mahusiano ya Makampuni kutoka Tigo Pesa Bw Amani Chuo aliwathibitishia washiriki wa mbio hizo kuwa kampuni hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba washariki wa mbio hizo wanajisajili kwa urahisi na kwa uhakika.
Mratibu wa Mbio za Rock City Marathon Bw Kasara Naftal (Kulia) akipokea mfano wa hundi yenye thamani Tsh milioni 20 kutoka kwa Mkuu wa Masoko, Mawasiliano na Mahusiano Benki ya KCB Tanzania, Bi Christina Manyenye ikiwa ni udhamini wa mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 24 mwaka huu, kwenye viunga vya Rock City Mall jijini Mwanza. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam leo.
Mratibu wa Mbio za Rock City Marathon Bw Kasara Naftal akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa hafla hiyo.
Mkuu wa Masoko, Mawasiliano na Mahusiano Benki ya KCB Tanzania, Bi Christina Manyenye (kushoto) akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Mratibu wa Mbio za Rock City Marathon Bw Kasara Naftal (wane kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa mbio hizo wakiwemo maofisa wa benki ya KCB Tanzania na maofisa wa Kampuni ya Tigo Pesa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...