Na Said Mwishehe,Michuzi TV
SIKU chache baada ya aliyekuwa Msemaji wa Klabu ya Simba Haji Manara kuondolewa kwenye nafasi hiyo leo Agosti 4,2021 ameibuka na kuzuungunza na waandishi wa habari na kuibua mambo mazito huku akitoa shutuma za wazi kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo Mohamed Dewji na Ofisa Mtendaji Mkuu Barbra Gonzalez.
Manara ametumia muda wa saa 1:20 kuelezea maisha ambayo ameyapitia akiwa Simba huku akiyaeleza hatua kwa hatua aliyoyaita manyanyaso aliyokuwa akiyapata kutoka Barbra.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Manara alianza kwa kufafanua namna gani alifanya kazi Simba kwa mikaa sita bila kuwa na mkataba rasmi wa kazi.
"Nilifanya Kazi Simba kwa moyo mmoja kwa miaka sita bila kupewa mkataba wowote licha ya juhudi za kutaka kupatiwa mkataba, lakini kwa mapenzi yangu kwa Simba nilifanya kazi kwa moyo tena bila kinyongo," amesema Manara.
KUJIGHARAMIA SAFARI
Mbali na kufanya kazi kwa miaka sita bila kuwa na mkataba, Manara ameweka wazi kuwa katika kipindi cha CEO Barbra, Manara hakuruhusiwa kusafiri na timu inapoenda kucheza ndani na nje ya nchi licha ya kazi kubwa ambayo alikuwa akifanya ya kutangaza mchezo ili mashabiki wajae uwanjani.
"Leo nataka nielezee kila kitu hili watanzani waelewe kwa nini yalitokea yale yaliyotokea, katika kipindi cha Barbra mimi kama msemaji wa klabu nilikuwa sisafiri na timu na yote ni maelezo ya CEO, hii ni tofauti na ma CEO waliopita.
"Kwa mfano nilianza kusafiri kipindi cha Magoli akiwa CEO. Na hata baadae alipokuja Senzo pia nilikuwa nasafiri, na Senzo alikuwa anaagiza kabisa nigharamiwe safari na hoteli simba inapokwenda, hawa waliiona na kuthamini kazi yangu," amesema Manara.
"Nlikuwa najisafirisha kwenda mikoani na hata nikifika huko bado nilikuwa naendelea kufanya kazi yangu, Mo alipoingia na neema kuanza kuonekana matatizo yakaanza na yakakolezwa zaidi CEO Barbra," amesema.
AMJIBU HANSOPE
Sehemu ya maelezo Manara ni kama amemjivu mmoja wanwajumbe wa klabu hiyo, Zacharia Hanspope juu ya mkataba.Hivi karibuni Hanspope alionekana kwenye mitandao akimjibu Haji juu ya kutopewa mkataba ambao Hansope alisema Manara alipewa mkataba wa mshahara wa mikioni nne lakini alikataa kusaini.
"Mzee wangu huyu inawezekana utu uzima nao unamsahaulisha.., kuhusu mkataba aliouzungumzia ni hivi..., kama nilivyosema nimefanya kazi Simba miaka sita bila mkataba, baadae nikapata dili la aAzam niwatangazie bidhaa zao.., wakanipa mkataba mnono na niliupokea kwa sababu Simba sikuwa na mkataba.
"Lakini kwa uungwana nikaenda kumwambia Mwenyekiti wetu Mo kuwa nimepewa mkataba na Azam kutangaza bidhaa zao, Mo akanikatalia akataka nimuonyeshe mkataba wa Azam ili aupandie dau.Nikaenda kwa mabosi zangu wa Azam nikawaambia jamani Mo anataka nikafanye naye kazi kwenye bidhaa zake je niende?
"Watu wa Azam waungwana wakaniambie 'why not', nikaenda kwa tukakaa na Barbra wakaupitia ule mkataba wa Azam...kwa bahati mbaya kwenye mkataba wa Azam kulikuwa na kipengele cha kulipa milioni 300 kama utavunjwa.
"Mo akashtuka.., baadae wakanipa mkataba wao ambao ulikuwa nilipwe milioni tatu kama mshahara na sio milioni nne kama anavyosema Hanspope, lakini wakaniwekea kipengere cha mimi kutofanya kazi na kampuni nyingine yoyote mshindani wa Mo...
"Sasa jamani milioni tatu ndio inibane kutofanya shughuri nyingine?, Azam wamenipa mkataba mnono.., jamani mkataba mnono sana," amesema Manara huku akitumia muda kumzungumzia Barba kama mmoja ya viongozi ambao amemtesa.
SHUTUMA ZA KUIHUJUMU TIMU
Mambo mengine ambayo Manara amefunguka ni juu ya shutuma za kuihujumu timu kuelekea kwenye mchezo wa Derby dhidi ya watani za Yanga.
" Hizi shutuma zilianza wiki chache kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Yanga kule Kigoma, nakumbuka ilikuwa kuelekea kwenye sikukuu ya Idd, unajua sisi na imani yetu hii ni siku muhimu sana, ni sikukuu ya kuchinja, siku hiyo nilinunua mbuzi nyumbani kwangu na kuchinja.
"Hivyo nikasema niende kugawa nyama na mchele kwetu kariakoo, baadabya kufika nikiwa na wazee wangu Barbra akanipigia simu ananiuliza nipo wapi n annafanya nini, nikishangaa lakini nikamjibu nipo kariakoo, akaanza kunifokea kuwa mimi muongo na wala sipo kariakoo nipo Posta na Ghalib, akasema naihujumu timu, dah nilishangaa lakini sikutaka kumjibu nikamwambia sawa nikakata simu," amesema Manara
Ameongeza kwamba "Kesho yake Sikuku nikaamka kujinadaa kwenda msikitini, nawasha simu nakutana na meseji ya Barbara akiendelea kunituhumu kuwa nahujumu Simba, Mo akanipigia nikaenda kumuona, nilishangazwa na yeye kunituhumu huku akitoa simu ya mpambe wake sijui na mlinzi wake.
"Na kunionyesha namna walivyonifuatilia na kuonekana nikiwa Posta na Kigamboni kwa nyakati tofauti, cha kushangaza simu ilionyesha nikikuwa huko tarehe 7, iliniuma sana, kwanza ni uongo lakini pia Kigamboni naenda mara kwa mara kwa sababu kuna wakwe zangu na pia nna mji wangu najenga na siku hiyo kweli nikikuwa huko,"
Manara ameongeza " Kwa nini wanidukue.., na pale niliona namba za watu wengine wa Simba na wanafudukuliwa, kwa nini wafanye hivyo, Mamlaka ya kufanya hivyo wametoa wapi? Serikali ipo macho ifuatilie kibali cha kudukua wamekitoa wapi? Mimi siwezi kuihujumu timu ya Simba.Wanasema naenda kambi ya Yanga sasa nikienda naenda kusemaje!!?, naenda kuhujumu vipi?"
MKATABA WA AZAM
Amesisitiza umaarufu wake na mikataba ya Azam ndio chanzo cha kuondolewa Simba.Aidha aligusia sababu ya Simba kukataa mkataba wa udhamini wa Azam ambao Yanga pia wamesaini kwa bilioni 2 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka 10.
"Wanasimba tusikubali kudanganywa.., Januari Simba walisaini mkataba na Azam wa haki ya vipindi vyao vya Televisheni kwa shilingi milioni 300, baadae Azam wakamwaga fedha kwenye udhamini wa haki ya matangazo ya mechi za ligi, Simba wakagomea kupewa fedha sawa na vilabu vingine.
"Barbra akawapigia simu viongozi wa Yanga wakawapa mchongo wa kukutana na Azam kuomba wao Simba na Yanga kuongezewa fedha, Azam walikubali na wakawaambia wataongeza fedha kwenye mikataba yao ya vipindi vyao vya televisheni ndio wakatoa fedha hizo ambazo Yanga wamezikubali Simba kupitia kwa Mo wamezikataa," amesema Manara.
Amesema Mo na Barbra wanawadanganya wana simba kuwa Mo hapati faida kwenye klabu hiyo wakati bidhaa zake zinatangazwa kwenye jezi za Simba.
AKATAA MASWALI YA WAANDISHI
Baada ya kutumia saa 1:20 kuelezea yote wakati waandisi wakijiandaa kwa maswali, Manara alimaliza kuzungumza huku akikwepa maswali."Nimeongea kwa saa 1 na dakika 20, nikitoka hapa nawahi ndege nasafiri nje ya nchi hivyo naomba niondoke niwai," amesema.
Manara ambaye alikuwa akizungumza huku akiwa na walinzi wawili waliovalia suti nyeusi huku mwenyewe akivaa suti rangi ya damu ya mzee sawa na viatu huku ndani akivaa shati jeupe na saa kisasa mkononi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...