Na Eleuteri Mangi- WHUSM, Dodoma

KAMATI ya Uratibu na Maandalizi ya Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) imekutana Agosti 20, 2021 kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alilotoa Agosti 15, 2021 wakati alipomuwakilisha Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan katika mbio za hisani za “CRDB Bank Marathon” zilizofanyika Jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho pamoja na mambo mengine kimependekeza mashindano hayo yafanyike Makao Makuu ya nchi Jijini Dodoma ili kuleta ushiriki mzuri wa wizara zote na itatoa fursa kwa Idara za serikali na mikoa kwa kuwa Dodoma ni katikati ya nchi.

Kikao hicho kimeongozwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Yusuph Singo. Wajumbe wengine wanatoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuweka mikakati ya pamoja ya kuleta hamasa ya kuendeleza michezo nchini kwa kushirikisha watumishi, wanafunzi na wananchi kwa ujumla.

“Lengo la Serikali ni kuwawezesha watumishi wafanye mazoezi kwa ajili ya afya zao, hatua hii itawasaidia watumishi wa umma kuboresha afya zao ikiwemo kujikinga na maradhi yasiyoambukiza hatua inayosaidia kuongeza hamasa ya utendaji kazi hivyo kuongeza tija na ufanisi wa kazi” amesema Mkurugenzi huyo wa Maendeleo ya Michezo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu SHIMIWI ndugu Alex Temba kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania amesema mashindano ya mwaka huu yanatarajiwa kufanyika Dodoma kuanzia Oktoba 20, 2021 hadi Novemba 02, 2021.

Ametaja michezo itakayofanyika ni mpira wa miguu kwa wanaume, mpira wa pete, kuvuta kamba, riadha, mbio za baiskeli, drafti, bao na karata yote ikihusisha wanaume kwa wanawake.

Aidha, kikao hicho kimeazimia kabla ya mashindano hayo, ufanyike uzinduzi rasmi wa michezo hiyo kwa watumishi wa umma na wananchi kwa kufanya mazoezi ya pamoja ikizingatiwa mazoezi ni dawa likiwa  pia ni agizo la  mheshimiwa Rais. 

Sambamba na hayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri watu wafanye mazoezi angalau dakika 150 kwa wiki. Kwa mantiki hiyo, kila siku mtu anatakiwa kufanya mazoezi kwa dakika 30 kwa siku 5 za juma ikiwemo kutembea, kuendesha baiskeli,  mchakamchaka ili kuleta utimamu wa mwili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...