Na Mwandishi Wetu

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) unatarajia kutoa mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wafanyakazi wapatao 6,500 katika sekta ya mafuta na gesi nchi nzima.
Mpango huo wa OSHA umewekwa wazi na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe, alipokuwa akifunga awamu ya kwanza ya mafunzo hayo katika wilaya yake ambapo amewaasa washiriki wa mafunzo kuwa mabalozi wa ujuzi walioupata katika maeneo yao ya kazi ili kuokoa maisha ya watu wanaoumia wakiwa kazini.

“Kutoa mafunzo kwa wafanyakazi 6,500 nchi nzima sio kitu kidogo hivyo OSHA wanastahili pongezi kubwa sana hasa tukizingatia kwamba malengo mahususi ya mafunzo tajwa ni kumlinda mfanyakazi na wateja wanaofika kupata huduma kwenye vituo vya mafuta. 

Aidha, mafunzo hayo yanalenga pia kulinda mali za wawekezaji dhidi ya majanga mbali mbali ikiwemo majanga ya moto na hivyo kuwa na uwekezaji endelevu na wenye tija kwa maendeleo ya Taifa letu,” amesema Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe.
Akitoa maelezo ya awali kuhusiana na mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema mafunzo hayo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria Na.5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, yanatolewa kwa wawakilishi wa wafanyakazi wa maghala ya kuhifadhia mafuta pamoja na vituo vya kuuzia mafuta nchi nzima baada ya kuhitimisha ukaguzi kwenye maeneo hayo na kubaini changamoto mbali mbali za usalama na afya.

“Sheria ya Usalama na Afya mahali pa kazi inataka kila sehemu ya kazi kuwa na wawakilishi wa wafanyakazi waliopatiwa mafunzo ya namna ya kutoa huduma ya kwanza endapo itatokea dharura kwa baadhi ya wafanyakazi kuumia ama kupata changamoto nyingine za kiafya. Hivyo, katika kuwezesha hilo, sisi tumefanya ukaguzi wa mazingira ya kazi katika depoti za mafuta pamoja na vituo vya mafuta nchi nzima na baada ya ukaguzi huo tumeanza sasa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa maeneo tuliyoyakagua,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo yaliyoanza kutolewa mwanzoni mwa juma lililopita katika Wilaya ya Kinondoni, Kassim Mtema, amesema katika mafunzo hayo washiriki wamefundishwa mada mbali kuhusiana na dhana nzima ya utoaji wa huduma ya kwanza katika maeneo ya kazi ikiwemo sheria za huduma ya kwanza, utangulizi katika huduma ya kwanza pamoja na mafunzo kwa vitendo juu ya kutoa huduma kwa wagonjwa waliopata dharura mbali mbali.
Washiriki wa mafunzo wameelezea yale waliyojifunza na umuhimu wake katika shughuli zao za kila siku hususan katika sekta ya mafuta na gesi ambayo inakuwa kwa kasi hapa nchini.

“Nimejifunza mambo mengi sana, baada ya mafunzo haya sasa nitaweza kuwahudumia wenzangu endapo itatokea changamoto yoyote ya kiusalama na afya kama vile ajali ya kuungua, kupoteza fahamu au hata kuvunjika. Kiujumla tumepata mafunzo mazuri sana, nimefunza na nimepata cheti changu hadi hapa hakika tutaweza kufanya vizuri,” ameeleza Aneth Aman ambaye alishiriki mafunzo.

Zaidi wafanyakazi 400 wa maghala na vituo vya kuuzia nishati ya mafuta wamepatiwa mafunzo ya huduma ya kwanza katika Wilaya ya Kinondoni ambapo yataendelea kutolewa katika mikoa mingine nchi nzima kwa wafanyakazi wengine zaidi ya 6,000.Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...