Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amelitaka Jeshi la Polisi kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali za Taasisi hiyo, ili kulinda haki za msingi za raia na kupunguza matukio ya kihalifu nchini.

 Mhe. Rais Samia amesema hayo leo Agosti 25, 2021, wakati akifungua Kikao Kazi cha Maafisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi, na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi, kilichofanyika katika Ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi  Oysterbay Jijini Dar es Salaam.

 Mhe. Rais Samia amesema umefika wakati kwa Jeshi la Polisi nchini kukaa na wadau wengine kuangalia uwezekano wa kurekebisha Sheria zikiwemo ya kuweka watu mahabusu, pamoja na ile ya muda wa upelelezi.

 Amesema kwenye nchi nyingine mtu hakamatwi mpaka upelelezi uwe umekamilika lakini Tanzania kesi nyingi zinakwama Mahakamani kutokana na kucheleweshwa kwa upelelezi au kukosekana Ushahidi wa kutosha.

 Mhe. Rais Samia amesema takwimu zinaonyesha kuwa kuna idadi kubwa ya mahabusu magerezani ambao baadhi ya kesi zinazoonekana kukwama kwasabau ya ucheleweshaji wa upelelezi hivyo kukosesha watu haki zao, na kwamba kuna baadhi ya askari wanaotuhumiwa kwa kukosa uadilifu, nidhamu na maadili.

 Aidha, Mhe. Rais Samia amelipongeza Jeshi hilo la Polisi kwa uamuzi wao wa karibuni wa kuweka ukomo wa upelelezi wa miezi sita kwa kesi ndogo na mwaka mmoja kwa kesi kubwa. Hali hii itasababisha uharakishwaji wa utoaji haki na kuipunguzia Serikali mzigo wa kuwahudumia mahabusu.

 Hata hivyo, Mhe. Rais amelitaka Jeshi la Polisi kujenga uwezo kwenye masuala ya TEHAMA ili kukabiliana na aina na mbinu mpya za uhalifu na kuwahimiza kuimarisha uhusiano na Majeshi mengine ya Polisi na Taasisi za Polisi za Kimataifa.

Vilevile, amelitaka Jeshi la Polisi kuimarisha uhusiano na wananchi ili waweze kupata taarifa kwa urahisi kwasababu wahalifu  wanaishi nao uraiani.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Samia amepokea Hati za Utambulisho wa Mabalozi watano walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Mabalozi waliowasilisha Hati za Utambulisho ni:-

1.     Mhe. Hamisu Umar Takalmawa – Balozi wa Nigeria hapa nchini;

2.     Mhe. Binaya Srikanta Pradhan – Balozi wa India hapa nchini;

3.     Mhe. Wiebe Jakob De Boer – Balozi wa Uholanzi hapa nchini;

4.     Mhe. Madina Diaby Kassamba Ganou – Balozi wa Burkina Faso hapa nchini mwenye makazi yake Jijini Nairobi nchini Kenya; na

5.     Mhe. Gaussou Toure – Balozi wa Guinea hapa nchini mwenye makazi  yake Addis Ababa nchini Ethiopia.

Akizungumza na Mabalozi hao, Mhe. Rais Samia amewapongeza kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewahakikishia kuwa Serikali yake itaendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na nchi hizo uliodumu kwa muda mrefu sasa.

 

Jaffar Haniu

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akifungua Kikao cha kazi kwa ajili ya Tathmini ya mwaka mmoja 2020-21 kwa Maafisa Mbalimbali wa Jeshi la Polisi nchini, leo Agosti 25,2021 katika Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay Jijini Dar es salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Maofisa wa Jeshi la Polisi Wanawake muda mfupi baada ya kufungua Kikao cha kazi kwa ajili ya Tathmini ya mwaka mmoja 2020-21 kwa Maafisa Mbalimbali wa Jeshi la Polisi nchini, leo Agosti 25,2021 katika Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay Jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na Maofisa wa Jeshi la Polisi muda mfupi baada ya kufungua Kikao cha kazi kwa ajili ya Tathmini ya mwaka mmoja 2020-21 kwa Maafisa Mbalimbali wa Jeshi la Polisi nchini, leo Agosti 25,2021 katika Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay Jijini Dar es salaam. PICHA NA IKULU.

 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...