Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima (wa kwanza kutoka kulia) akiwa ameshika Barakoa wakati akipata maelekezo alipotembelea Kiwanda cha Mony kinachozalisha Barakoa za aina mbalimbali, Dkt. amewaasa Mony Industries kutengeneza bidhaa hizo za Barakoa na bidhaa mbalimbali za afya.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima (wa tatu kutoka kulia) akipewa maelekezo namna Barakoa zinavyofungashwa baada ya kutengenezwa katika Kiwanda cha Mony kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima akionesha Barakoa aina ya K95 ambayo inazalishwa katika Kiwanda cha Mony, Barakoa hiyo inavaliwa mahsusi maeneo hatarishi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Mony, Violet Mordichai akizungumza katika uzinduzi wa Kiwanda hicho Wilayani Kigamboni, Dar es Salaam.


WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa hatarajii kuona Bohari ya Dawa nchini (MSD) inaagiza Barakoa nje ya nchi endapo watakuwa na uhitaji wa Barakoa hizo licha ya wao kuzalisha bidhaa hiyo.

Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Kiwanda cha Mony (Mony Industries Factory) kinachozalisha Barakoa kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam. Ameagiza Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuimarisha usimamizi wa ubora wa bidhaa za Afya kwa Viwanda vya Dawa na bidhaa nyingine za Afya nchini.

Dkt. Gwajima amesema kuwa Serikali kupitia MSD hawana ushindani na Kiwanda hicho cha Mony sambamba na Sekta binafsi katika kutoa huduma kwa Wananchi, bali amesema Sekta binafsi na Serikali zinapaswa kukaa pamoja na kushirikiana ili kutoa huduma hizo kwa bei nafuu kwa Wananchi  ili kila mmoja apate kufikiwa kwa urahisi.

“Uzalishaji wa Barakoa katika Kiwanda cha Mony kutasaidia Serikali yetu kupunguza kuagiza Dawa na Vifaa Tiba nje ya nchi, hivyo itapunguza matumizi ya hela za kigeni, lakini hakikisheni mnazalisha bidhaa bora zinazoshindana nchini na Kimataifa kutokana na mahitaji ya bidhaa hizo ulimwenguni”, amesema Dkt. Gwajima.

Pia ameeleza Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ina hakikisha inaweka mazingira bora na wezeshi kwa Wawekezaji wa Sekta binafsi ili kuendelea kuwekeza Tanzania. Dkt. Gwajima amewahakikishia Kiwanda hicho mazingira bora ili waendelee kuzalisha bidhaa mbalimbali za Afya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Mony, Violet Mordichai amesema uzinduzi wa Kiwanda hicho ni jitihada za kuunga mkono Serikali ya Tanzania katika kuongeza Viwanda nchini, ikiwa ni pamoja na kurahisisha upatikanaji wa Vifaa Tiba na kufikia lengo la Afya bora kwa wote.

Mordichai amempongeza Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuboresha upatikanaji wa huduma bora za Afya kote nchini. Amewapongeza Mamlaka ya TMDA kutoa ushirikiano katika harakati na taratibu za kufanikisha kuwepo kwa Kiwanda hicho eneo hilo la Kigamboni, Dar es Salaam.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Almas Nyangasa ameeleza kuwa Uongozi wa Kigamboni utaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Wawekezaji wote na kuwapa huduma zote zinazostahili ili kufanikisha azma yao na azma ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Uchumi wa Viwanda.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...