Mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon na Klabu mbalimbali maarufu barani Ulaya, Samwel Eto’o rasmi ametangaza nia ya kuwania urais katika Shirikisho la Soka nchini humo (FECAFOOT), akinadi kuendeleza na kuboresha Soka la Cameroon kupitia nafasi hiyo ya urais.
Kupitia taarifa yake aliyotoa tamko la kuwania urais wa Shirikisho la Soka nchini humo, Eto’o amesema lengo lake kubwa, kutangaza na kukuza vipaji vya nchi hiyo ya Cameroon na kusaidia nguvu kubwa iliyowekwa na Kiongozi wa taifa hilo, Rais Paul Biya katika kusaidia maendeleo ya nchi yao ikiwemo maendeleo ya Soka.
Eto’o amesema haina maana kwa soka la nchi hiyo kushindwa kuendelea wakati wao waliowahi kucheza zamani wakishuhudia kudolola kwa vipaji na kushindwa kuitangazia dunia nchi yao ya Cameroon ambayo mara nyingi imefanya vizuri katika kanda ya Afrika na hata ulimwenguni kwenye mchezo wa Soka.
Kupitia taarifa hiyo, Eto’o ameeleza kwa Maafisa wanaoshughulika na masuala ya Soka nchini humo, kuondokana na ubinafsi na kuwapa fursa, kipaumbele wenye vipaji na Makocha wenye viwango nchini humo ili kulea vipaji na kuendeleza Soka. Hata hivyo amesema atatumia miradi yake ya aliyoianzisha miaka mitatu iliyopita kusaidia kuboresha soka la nchi hiyo.
Kwa upande wa timu ya taifa ya Wanawake ya nchi hiyo, Eto’o ameahidi kusaidia kikamilifu kuhakikisha wanafika mbali na kupata mafanikio ya kutwaa ubingwa wa Afrika kwa upande wa Wanawake. Eto’o amebainisha kuwa haina maana kwa timu ya Wanawake kufika Fainali mara nne kwenye Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) bila kutwaa Ubingwa huo.
Pia ameahidi kushiriki ipasavyo kuendeleza Soka la Ufukweni, ili kupata mafanikio bora kama ilivyofanya mwaka 2006 kutwaa Ubingwa wa Afrika katika mashindano ya Soka la Ufukweni.
Uchaguzi wa Shirikisho la Soka nchini Cameroon unatarajiwa kufanyika Desemba 11, 2021. Kwa sasa Shirikisho hilo linaongozwa na Rais wa muda, Seidou Mbombo Njoya. Wengine wanaowania urais wa Shirikisho hilo ni Jules Denis Onana na Emmanuel Maboang Kessack ambao waliwahi kucheza Kombe la Dunia mwaka 1990 wakiwa na timu ya taifa ya nchi hiyo.
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...