Na Said Mwishehe,Michuzi TV

WAPANDA baiskeli wa msafara wa Twende Butiama unatarajia kuondoka mkoani Dar es Salaam Oktoba 3 ,2021 kuelekea Butiama mkoani Mara, lengo likiwa ni kuungana na Watanzania kwenye kumbukizi ya miaka 22 tangu alipotutoka Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere Oktoba 14,mwaka 1999.

Akizungumza leo Septemba 30,2021 Mwenyekiti wa Msafara wa Twende Butiama kutoka Chama cha Baiskeli Tanzania Gabriel Landa amesema msafara huo utaanzia kwenye makazi ya Mwalimu Nyerere Msasani mkoani Dar es Salaam na kuhitimishwa Mwitongo ,Butiama Oktoba 14 mwaka huu.

"Msafara huu wa baiskeli ni wa takribani siku 10 zenye umbali wa kilometa zisizopungua 1400 kupitia katika mikoa 10 ,wilaya zisizopungua 20 na kuhusisha waendeshaji na washiriki wasiopungua 100.Huu ni mwaka wa nne mwaka wa nne sasa tulipoanza matembezi haya mwaka 2018.

"Msafara huu wa wapanda baiskeli kwenda Mwitongo ,Butiama  unalenga kukumbuka mchango wake kuhusu mapambano ya Uhuru kwa Waafrika kutoka Serikali za kikoloni ikiwa pamoja na kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja bila kujali kabila dini,jambo lililosababisha kudumisha mshikamano na amani kwa Watanzania,"amesema.

Amefafanua Twende Butiama ilianza mwaka 2018 na msafara huo umekuwa unahamasisha Watanzania kuendeleza juhudi za Baba wa Taifa ikiwa ni pamoja na kupambana na maadui watatu wa maendeleo ambao ni ujinga,maradhi na umasikini.Msafara huo pia umekuwa unahamasisha utunzaji mazingira ili kuepukana na madhara yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi

Amesema wamekuwa wakihamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye utalii wa ndani, na pia kuwahamasisha kufanya mazoezi kwa kuendesha baiskeli kama njia mojawapo ya kuimarisha afya ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo shinikizo la damu,saratani ,magonjwa ya moyo na kisukari.
Landa amesema katika kupambana na adui Ujinga mwaka huu wameamua kuhamasisha wananchi wapenda maendeleo ya nchi yetu kuchangia madawati kwa ajili ya shule za msingi mbili zilizopo Butiama ambazo ni shule ya msingi Mwibagi A na B.

"Hadi sasa tumekwishakusanya madawati yapatayo 115 ambayo yametolewa n wadau mbalimbali wa maendeleo ya elimu.Ni matumaini yetu watanzania wengine, wadau na wapenda maendeleo  wataunga mkono juhudi hizi za uchangiaji wa madawati kama njia pekee ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

"Katika kumuenzi Baba wa Taifa msafara una lengo la kusaidia kuwezeshwa Nyerere anaendelea kukumbukwa na kuishi ndani ya Watanzania.Katika kufanikisha hili msafara wa Twende Butiama utaendelea kuyatembelea maeneo ambayo Nyerere aliishi, alipata elimu au kufanya kazi au akiwa katika harakati zake za kudai Uhuru hata baada ya Uhuru.

"Ndio maana msafara wa TwendeButiama umekuwa kwenye makazi yake Msasani mkoani Dar es Salaam na kisha kupitia Pwani,Morogoro, Dodoma,Singida,Tabora ,Shinyanga,Mwanza , Simiyu na Mara.Tangu tumeanza wapanda baiskeli wasiopungua 500 wameshiriki, tumekuwa tukipata ushirikiano mkubwa,"amesema.

Kwa upande wake Katibu wa Twende Butiama Salum Kizoka amesema maandalizi yote kuhusu msafara huo yamekamilika na barabara ambayo itatumika nayo imekaguliwa, hivyo maandalizi yamekamilika kwa asilimia 95 hadi sasa.

  .

Viongozi wa Msafara wa Wapanda Baiskeli unaofahamika Twende Butiama wakiwa na bango linaoonesha  ramani ya barabara watakazopita kutoka Dar es Salaam kwenda Butiama mkoani Mara.Msafara huo utaondoka Oktoba 3,2021 ukiwa na wapanda baiskeli zaidi ya 120 na utatembea zaidi ya kilometa 1,400 .
 Katibu wa Msafara Twende Butiama Salum Kizoka( katikati) akielezea maandalizi ya safari ya kwenda Butiama mkoani Mara kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere .Maadhimisho ya kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Nyerere hufanyika Oktoba 14 ya kila mwaka

Mwenyiki wa Msafara wa Panda baiskeli wa Twende Butiama Gabriel Landa(katika) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu msafara huo ambao utaondoka Dar es Salaam Oktoba 3,2021 kwenda Butiama mkoani Mara.Wengine katika picha hiyo Makamu Mwenyekiti wa msafara huo (kushoto) na Katibu wao( kulia)
Makamu wa Rais wa Chama cha Baiskeli Tanzania(CHABATA) Hussein Ally( katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu safari ya Twende Butiama inayotarajiwa kufanywa na wapanda zaiskeli zaidi ya 120 kuanzia Dar es Salaam hadi Butiama mkoani Mara

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...