NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe amewataka wazalishaji wa bidhaa za viwandani kuzingatia ubora wa bidhaa hizo, ameyasema hayo leo tarehe 16 Septemba, 2021 alipotembelea kiwanda cha kutengeneza Nondo cha Kamal Steel kilichopo Chang’ombe jijini Dar es salaam nakujionea uzalishaji wa Nondo Kiwandani hapo.

Mhe. Kigahe amefurahishwa na shughuli zinazofanywa na Kiwanda hicho na kusema kuwa kiwanda cha Kamal ni kiwanda kikubwa ambacho kinazalisha bidhaa za chuma na kutumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya serikali na binafsi.

Mkurugenzi wa kiwanda cha Kamal Steel ndugu Sameer Santosh amesema kuwa uwekezaji wa kiwanda hicho ni dola za kimarekani zaidi ya Milioni 25 na kimeajiri wafanyakazi 350 wa kudumu na pia kiwanda hicho kimekuwa kikilipa kodi kwa serikali na kusaidia jamii inayowazunguka hasa katika shule mbalimbali, huduma za afya na sasa wameanza kutengeneza vifaa au Viungo saidizi kwa walemavu.

Mhe. Kigahe amesema kuwa kiwanda cha Kamal Steel kimefanya uwekezaji mkubwa hasa katika mitambo kwa kuhakikisha wanafuata viwango vya kimataifa na hii imepelekea kufanikiwa kutengeneza bidhaa bora ambazo zinauzika ndani na nje ya nchi, ''Rai yangu kubwa kwa wafanyabiashara wengine wenye Viwanda kuzingatia ubora katika uzalishaji wa bidhaa na kuandika majina ya kampuni katika bidhaa zao ukizingatia kwa sasa nchi yetu imeridhia kujiunga na soko huru la Afrika (AfCTA) hivyo nawasihi wafanyabiashara wote nchini kujipanga kutumia soko hili kwa nguvu zote.'' Amesema.

Aidha Mhe. Kigahe amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imejipanga kutatua changamoto zinawakabili wenye Viwanda hasa changamoto ya umeme kupitia mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere uliopo Rufiji, ili Viwanda vyetu viwe na umeme wa uhakika na kuongeza uzalishaji na kupunguza hasara.

Katika hatua nyingine Mhe. Kigahe amepata fursa kutembelea kiwanda cha kuzalisha chupa za Vinywaji baridi na vikali cha Kioo Limited ambapo amesikiliza taarifa ya kiwanda na kutembelea kiwanda kujionea uzalishaji wa chupa.

Kiwanda hicho cha Kioo Limited kimewekeza mtaji zaidi dola milioni 56 za kimarekani na kimeajiri wafanyakazi wa kudumu 500 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 300 na kusaidia watanzania kupata ajira kupitia kiwanda hicho.

Mhe. Kigahe amesema kuwa serikali inathamini sana mchango wa kiwanda hicho katika kuchangia uchumi wa nchi kwani kiwanda hiki kina masoko katika nchi mbalimbali barani Afrika na hii imesaidia ongezeko la fedha za kigeni katika nchi yetu.

“Kiwanda hiki kinalipa kodi kwa serikali hivyo kuchangia maendeleo ya Taifa, pia kimeweka teknolojia ya hali ya juu ambayo ni rafiki wa mazingira ukizingatia kipo katikati ya mji, kiwanda hiki kimeajiri vijana wengi na kutoa elimu kwa wafanyakazi wao kujiendeleza zaidi kuendana na teknolojia ya sasa”. Amesema Mhe. Kigahe.

Naye kaimu Mkurugenzi wa kiwanda cha Kioo Limited ndugu Kapil Dave amesema kuwa changamoto waliyonayo ni uhaba wa maeneo ya uwekezaji ili kuwekeza zaidi katika maeneo mengine ya nchi yetu.

Mhe. Kigahe amemaliza kwa kusema kuwa serikali imesikia ombi lao la kupatiwa maeneo Zaidi ya uwekezaji ili waendelee kuwekeza viwanda katika maeneo mengine ya nchi yetu.

Naibu Waziri wizara ya viwanda na biashara Mhe. Exaud Kigahe akipata Maelezo ya namna miguu bandia inavyotengezwa Kwa ajili ya walemavu katika kiwanda Cha Kamal Steel alipotembelea kiwanda hicho.
Naibu Waziri akipata Maelezo ya namna nondo inavyotengenezwa ktk kiwanda Cha Kamal steel.
Baadhi ya vifaa vinavyotumika kutengeza miguu bandia Kwa ajili ya walemavu katika kiwanda Cha Kamal Steel kilichopo chang'ombe Jijini DSM.
Mashine maalumu ya kufungasha chupa katika kiwanda Cha Kioo Limited Jijini DSM.
Muonekano wa kiwanda Cha kutengeneza chupa zinazotumika kuhifadhia vinywaji baridi na pombe Kali Cha Kioo Limited.
Naibu Waziri Mhe. Exaud Kigahe akipanda mti Kama ishara ya utunzaji wa mazingira ktk kiwanda Cha nondo Cha Kamal Steel chang'ombe Jijini DSM.
Bidhaa za nondo zinazotengenezwa na kiwanda Cha Kamal Steel chang'ombe Jijini DSM.
Naibu Waziri akipokea zawadi kutoka kwa mkurugenzi wa kiwanda Cha Kamal Steel ndugu Sameer.
Kiwanda Cha Kioo Limited.
Muonekano wa kiwanda Cha kutengeneza chupa zinazotumika kuhifadhia vinywaji baridi na pombe Kali Cha Kioo Limited.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...