· SBL yazindua kiwanda kipya cha kutengeneza pombe kali
Moshi, Septemba 23, 2021: Kampuni maarufu ya bia nchini Serengeti Breweries Limited (SBL), imeadhimisha safari yake ya uwekezaji wa miaka mitatu inayogharimu bilioni 166/- inayolenga kuongeza uwezo wake wa uzalishaji pamoja na kuzindua kiwanda kipya cha kutengeneza pombe kali.
Mpango huu ulianzishwa mwaka 2019 ambapo SBL ililenga kuongeza uzalishaji wake katika viwanda vyake vilivyopo Dar es Salaam, Mwanza na Moshi. SBL pia imezindua kiwanda kipya na cha kisasa cha kutengeneza pombe kali mjini Moshi ikiwa sehemu ya mpango wake wa uwekezaji
Akizingumza mbele ya mgeni rasmi wa shughuli hio ambae alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa. Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Mark Ocitti alinukuliwa akisema, ‘‘Upanuzi huu utasababisha kuongezeka kwa mahitaji ya nafaka za ndani ambazo SBL inanunua kwa wakulima nchini kama vile mahindi, shayiri na mtama kwa ajili ya kutengeneza bia. Vilevile itatengeneza fursa za ajira na kupanua uwezo wa kampuni kusambaza bidhaa zake nchini. Aidha, upanuzi huu umekusudia kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi ya Serikali na hivyo kuiongezea nchi mapato.’’
Ocitti aliendelea kusema, ‘‘Kiwanda hiki kipya kitatengeneza pombe kali za ndani katika viwango vya kimataifa na kuiwezesha SBL kuwa mshindani mkubwa katika uzalishaji wa pombe kali. Aidha kabla ya uanzishwaji wa kiwanda hiki, SBL ilikuwa inaagiza pombe kali kutoka nje’’.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa aliipongeza kampuni ya SBL kwa kuwekeza zaidi nchini, jambo ambalo litaisadia nchi kupata mapato zaidi na kuchochea ukuaji wa kiuchumi. Waziri Mkuu alisisitiza dhamira njema ya Serikali kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Kiwanda kipya cha kutengeneza pombe kali mjini Moshi kimejengwa kwa gharama za shilingi bilioni 15.6/-. Gharama hizi ni miongoni mwa safari ya uwekezaji wa miaka mitatu ambapo SBL imepanga kutumia bilioni 124/- kuongeza uzalishaji wake wa pombe, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa SBL.
Kiwanda hiki kipya kitatengeneza aina mbalimbali za pombe kali hadi zile zilizokuwa zinaingizwa kutoka nje ya nchi. Aidha, SBL ilishaanza kutengeneza pombe kali mpya nchini iitwayo, BONGO DON ambayo Mkurugenzi Mtendaji alisema kuwa utengenezaji wake umezingatia viwango vya kimataifa.
Kampuni ya bia SBL imeajiri wafanyakazi 800 na maelfu wengine wakifaidika katika mnyororo wake wa thamani. SBL ina mtandao wa wakulima zaidi ya 400 nchini ambao wanautumia kununua nafaka za kuzalisha bia kama mahindi, shayiri na mtama.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa akikagua kiwanda kipya cha kutengeneza vinywaji vikali katika kiwanda cha SBL Moshi kwenye maadhimisho ya uwekezaji wa miaka mitatu wa SBL. Kushoto ni Mkurugenzi wa Operesheni wa SBL, ndugu Anthony Njenga akitoa maelezo, kushoto kwake ni Naibu waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe.
Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania akisalimiana na viongozi wa SBL kwenye maadhimisho ya uwekezaji wa miaka mitatu wa SBL, tukio lililofanyika kiwanda cha SBL mkoani Kilimanjaro. Kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Mark Ocitti, Mwenyekiti wa Bodi ya SBL, John Ulanga na Mkurugenzi wa Operesheni wa SBL, Anthony Njenga.
Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, ndugu Mark Ocitti akizungumza kwenye maadhimisho ya uwekezaji wa miaka mitatu wa SBL, tukio lililofanyika kiwanda cha SBL mkoani Kilimanjaro. Kulia kwake ni Mary Majaliwa (Mke wa Waziri Mkuu), Mgeni Rasmi, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Waziri Mkuu wa Tanzania), Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe.
Mgeni rasmi, Waziri Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza kwenye maadhimisho ya uwekezaji wa SBL wa miaka mitatu nchini yaliyofanyika kwenye kiwanda cha SBL mkoani Kilimanjaro ambapo pia alizindua kiwanda kipya cha kutengeneza vinywaji vikali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...