Serikali imeelekeza wataalamu wa mazingira kufika katika Ziwa Jipe wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro na kufanya upembuzi yakinifu utakaosaidia kuyaondoa magugu maji yaliyozingira ziwa hilo.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande Chande ametoa maelekezo hayo Septemba 20, 2021 alipofanya ziara ya kikazi kukagua athari za kuenea kwa magugu maji hayo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo alitahadharisha kuwa kutoweka kwa ziwa hilo kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa Taifa kwani wananchi wanaweza wakapoteza fursa za uwekezaji.

“Nimejionea madhara ya magugu maji katika ziwa hili jambo ambalo linaweza kusababisha likapotea kabisa katika ramani hivyo naelekeza wataalamu wetu wa mazingira wajiridhishe kabla ya kuomba fedha kutoka kwa wahisani wa ndani na nje watusaidie fedha ili kuondoa magugu haya,” alisema.

Kutokana na changamoto ya kutofanyika kilimo endelevu, Chande aliutaka Uongozi wa Wilaya ya Mwanga pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhakikisha wanadhibiti kilimo kisicho endelevu kando ya ziwa ambacho husababisha athari za kimazingira ikiwemo mmomonyoko wa udongo.

Katika kuhakikisha mipaka ya ziwa hilo inalindwa aliwahakikishia wananchi kuwa suala hilo litafanyiwa kazi kwa kuhusisha nchi zote mbili yaani Tanzania na Kenya ili Watanzania wafaidi rasilimali zao.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Mhe. Joseph Tadayo aliiomba Serikali kutatua changamoto hiyo kwa kuondoa magugu hayo ndani ya ziwa akisema kuwa linategemewa kwa shughuli mbalimbali zikiwemo uvuvi, mradi mkubwa wa maji wa Same, Mwanga na Korogwe pamoja na kilimo cha umwagiliaji.

Tadayo alisema ziwa hilo litasaidia kuongeza ajira hususan kwa vijana na hivyo kunufaisha wakazi takriban 2,564 wanaolizunguka pamoja na baadhi ya wananchi wa Wilaya jirani ya Moshi Vijijini.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Lewis Nzali alisema kuna mradi umendaliwa kwa ajili ya kulinusuru Ziwa Jipe na hatua ya kutafuta wafadhili imeanza.

“Kwenye Kanda yetu kuna miradi mitatu ambayo ni Ziwa Babati na kule Hanang Ziwa Basoutu ambako kuna changamoto ya kujaa maji na tulikwenda kule mwa mwaka jana tulikuta baadhi ya nyumba zimezingirwa kwa maji. Ziara hii itahuisha kufuatilia kwa karibu miradi hii,” alisema Nzali.

Awali akisoma taarifa, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Bw. Elirehema Palanjo alisema ziwa hilo linakabiliwa n\a changamoto ya usimamizi wa kimazingira.

Alisema kuwa Wilaya itahamsisha jamii kusimamia vyanzo vya maji, kuhifadhi mazingira na mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kudhibiti shughuli zinazoweza kusababisha uharibifu wa mazingira.

Katika ziara ya Naibu Waziri Chande pia alitembelea na kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 katika kiwanda cha Kilimanjaro Biochem Limited (KBL) kinachozalisha kemikali kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Alionesha kuridhishwa namna ambavyo wamiliki wa kiwanda wanazingatia suala la utunzaji wa mazingira ikiwemo kuwa na mfumo thabiti wa majitaka yanayotoka kiwandani hapo.

Katika kuhamasisha hifadhi endelevu ya mazingira Naibu Waziri huyo akiwa na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Abdallah Mwaipaya alishiriki zoezi la upandaji mti kiwandani hapo.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande (wa nne kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa mtaalamu wa kiwanda cha Kilimanjaro Biochem Limited (KBL) kinachozalisha kemikali kwa ajili ya matumizi mbalimbali wilayani Mwanga. Wengine pichani kuanzia kushoto ni Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Lewis Nzali, Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Mhe. Joseph Tadayo na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Abdallah Mwaipaya.


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande na viongozi wengine wakiwa katika ziara kiwanda cha Kilimanjaro Biochem Limited (KBL) kinachozalisha kemikali kwa ajili ya matumizi mbalimbali wilayani Mwanga.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande akitoa maelekezo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua athari za magugu maji yaliyozingira Ziwa Jipe wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro Septemba 20, 2021. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Mhe. Joseph Tadayo na kulia ni Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Lewis Nzali.


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande akiwasili na viongozi wengine katika Ziwa Jipe wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro Septemba 20, 2021. Kukagua athari za magugu maji.


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Mhe. Joseph Tadayo kuhusu athari za magugu maji katika Ziwa Jipe wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro Septemba 20, 2021. Mbele yao yanaonekana magugu maji yakiwa yamezingira Ziwa Jipe.



Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande (kulia) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Stephen Kagaigai mara baada ya kuwasili mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya kikazi Septemba 20, 2021. Wengine pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Said Mtanda na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Abdallah Mwaipaya.



(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...