JESHI la Magereza hapa nchini limetakiwa kushirikiana na wadau wanaotoa msaada wa kisheria ikiwemo Asasi ya kiraia ya EnviroCare ili kulifanya jeshi hilo kupunguza msongamano wa wahalifu walioko kwenye vizuizi wakiwemo mahabusu na hivyo kuimarisha uchumi wa jeshi hilo na Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela Septemba 29 mwaka huu Wakati akifungua semina ya mafunzo ya utoaji wa huduma za msaada wa kisheria katika maeneo ya vizuizi wakiwemo mahabusu yanayofanyika kwa siku tatu katika Hoteli ya Kings way katika Halmashauri ya manispaa ya Morogoro.
Martine Shigela pamoja na kulipongeza jeshi hilo kwa kufanya kazi kwa karibu na InviroCare na amelitaka kuendeleza ushirikaiano huo ili mahabusu na wafungwa waweze kupata msaada wa kisheria hivyo kupunguza msongamano uliopo katika magereza kwani wengi wao wanaweza kupata dhamana kwa makosa yao na kupunguza misongamano hiyo.
Akifafanua zaidi Martine Shigela amesema takwimu zinaonesha kuwa ndani ya magereza hapa nchini mahabusu ni wengi kuliko wafungwa na kwa mujibu wa Sheria za Tanzania Mahabusu hawaruhusiwi kufanya kazi za uzalishaji isipokuwa mfungwa, hivyo, wafungwa wamekuwa wakifanya kazi ya ziada katika kuzalisha kwa ajili yao na kwa ajili ya mahabusu jambo linalorudisha nyuma kiuchumi Jeshi hilo.
“…Ni kwamba tuna mahabusu wengi ambao hawazalishi ukilinganisha kati ya wafungwa wanaofanya kazi na mahabusu pamoja na walioko kwenye vizuizi 40% ni wafungwa wakati 60% ni mahabusu… kundi hili kwa mujibu wa Sheria zetu hawatakiwi kufanya kazi” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Naye Msajiri wa watoa huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Felista Mushi amesema kwa sasa msaada wa kisheria umevuka kutoka kuwa huduma kwa watu walioko vizuizini kuwa ni haki kwao kama zilivyo haki nyingine bila kujali mhusika amefanya makosa na yuko kizuizini.
Amesema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bado inamruhusu mtu huyo kupata haki yake ya Msaada wa kisheria ikiwemo kukata rufaa au kudhaminiwa na kwa kupitia msaada huo mtuhumiwa anaweza kufikia malengo anayoyatarajia ya kupata haki yake.
Katika hatua nyingine Bi. Felista ametumia fursa hiyo kwa niaba ya Wizara ya Katiba na Sheria kulipongeza Jeshi la Magereza hapa nchini kwa kuonesha ushirikiano mkubwa katika kuwafikishia Msaada wa Kisheria watu walioko katika vizuizi hususan wakati wa maadhimisho ya msaada wa kisheria wakiwemo mahabusu na wafungwa magerezani na hivyo husaidia kupunguza msongamano magerezani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa InviroCare ambao ndio walioandaa mafunzo hayo Bi. Catherine Jarome ametaja mafanikio ya Asasi hiyo kuwa ni pamoja na kuazisha mitandao ya wasaidizi wa kisheria kikanda, kutoa mafunzo kwa wasaidizi wa Kisheria 272 wakiwemo Askari Polisi, Askari magereza na Mahakimu 40 huku msaada wa kisheria ukiwa umetolewa kwa mahabusu zaidi ya elfu thelathini.
Akitoa shukrani mara baada ya Hotuba ya Mkuu wa Mkoa, Kamanda wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Morogoro SACT Rajab Hamza, amesema jeshi la Magereza wanakubaliana kabisa na wito uliotolewa na Mkuu wa Mkoa kuwa moja ya njia ya kupunguza Msongamano wa mahabusu utoaji wa huduma ya Msaada wa kisheria.
Aidha, amesema Jeshi hilo halifurahishwi kuwa na mahabusu wengi ambao kimsingi wanazuiliwa kisheria kufanya kazi zozote za uzalishaji hivyo wangefurahishwa kuona watuhumiwa hao ama wanaachiwa kuwa huru kwa mujibu wa taratibu ili kwenda kuzalisha wakiwa uraiani ama wanatiwa hatiani kwa mujibu na kufungwa ili waingizwe kwenye utaratibu wa uzalishaji na hatimae jeshi hilo kujitegemea.
Mradi huu wa kutoa Msaada wa Kisheria ulianza mwaka 2012 na shirika lisilo la Kiserikali la InviroCare lengo likiwa ni kutoa msaada wa kisheria kwa walio maeneo ya vizuizi, na mwaka 2017 Serikali ilitunga sheria ya msaada wa kisheria kwa lengo la kuratibu na kusimamia masuala yote yanayohusu utoaji wa msaada wa kisheria hapa nchini. Ndani ya sheria hii kuna kipengele kinachotaka maeneo yote ya vizuizi ikiwemo Polisi na magereza kutoa mazingira rafiki kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa wahitaji.
Kikao hicho kinalenga kutoa mafunzo kwa Wakuu wa Magereza na wanasheria wa magaraeza hayo kwa mikoa 9 ya mradi ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Geita, Mawanza, Tabora, Kilimanjaro, Tanga na mwenyeji wao Mkoa wa Morogoro.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...