Na Dorina G. Makaya na Janeth Mesomapya – Tanga.

Waziri wa Nishati, Mh. January Yusuf Makamba ameeleza kuwa Wakuu wa Mikoa minane (8) ambapo utapita mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) wanajukumu kubwa katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuhakikisha fursa zitakazopatikana zinanufaisha wananchi wa mikoa yao husika.

Waziri Makamba ameyasema hayo leo, Septemba 27, 2021 wakati wa semina kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa minane itakayopitiwa na mradi huo, inayofanyika jijini Tanga.

“Moja ya sababu za bomba hili kupita nchini kwetu ni uhakika wa ulinzi na usalama uliopo. Usalama huo utaendelea kuwepo kama wanaosimamia usalama huo kwenye maeneo linapopita bomba wana uelewa kuhusu mradi na kile kinachohitajika kufanywa ili walioamua bomba hili lipitie kwetu wawe na imani kwamba walifanya uamuzi sahihi”, alisema Waziri Makamba.

Ameongeza kuwa semina hiyo inalenga kutengeneza uelewa mpana kwa viongozi hao kuhusu mradi na kujadili fursa mbalimbali zitakazopatikana kwenye utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato ametoa rai kwa viongozi hao kuhakikisha wanatengeneza mazingira mazuri ili fursa zitakazotokana na utekelezaji wa mradi huo zinufaishe wananchi wa mikoa husika.

Mh. Byabato amesema kuwa Bomba hilo litapita katika mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga,Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Ameeleza kuwa Mkataba Hodhi wa Mradi (HGA) baina ya Serikali na Kampuni ya Bomba umeainisha baadhi ya bidhaa na huduma zitakazotolewe na Watanzania pekee (Reserved Contracts).

Naibu Waziri Byabato ameongeza kuwa, bidhaa na huduma hizo ni pamoja na usafirishaji, ulinzi, chakula na vinywaji, huduma ya malazi, mafuta kwa ajili ya magari na mitambo, shajala, bidhaa za ujenzi zinazopatikana hapa nchini, shughuli za ujenzi (civil works), huduma za mawasiliano, na ukodishaji wa mitambo ya ujenzi.

Bidhaa na huduma nyingine za manunuzi tofauti na zile zilizotengwa kwa Watanzania tu zitapatikana kwa njia ya ushindani na Watanzania wenye uwezo, vigezo na sifa stahiki wataweza kushiriki.

Ameongeza kuwa bidhaa na huduma nyingine za manunuzi tofauti na zile zilizotengwa kwa Watanzania tu zitapatikana kwa njia ya ushindani na Watanzania wenye uwezo, vigezo na sifa stahiki wataweza kushiriki.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) Dkt. James Mataragio ameeleza kuwa serikali kupitia shirika hilo inamiliki hisa asilimia 15% ya utekelezwaji wa mradi huo, huku asilimia 62% ikishikiliwa na kampuni ya Total Energies, asilimia 15% ya UNOC ya Uganda huku CNOOC ikishikilia asilimia 8%.

“Majukumu ya TPDC kwenye mradi huu ni pamoja na kuwa mbia kwenye mradi wenyewe, kushughulikia masuala ya ardhi, kusimamia mikataba yote ya EACOP, kuwa na uwakilishi wa asilimia 15% kwenye uongozi na kuwa na mjumbe kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya EACOP pamoja na kuratibu ushirikishwaji wa wadau mbalimbali watakaofanikisha utekelezaji wa mradi huu”, aliongeza.

Semina hiyo iliyowakutanidha wakuu wa mikoa minane jijini Tanga pamoja na baadhi ya viongozi wa Serikali, Bunge, Wizara ya Nishati na Taasisi zake itafanyika kwa siku tatu hadi tarehe 29 Septemba, 2021.




Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba akizungumza na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa minane ambayo itapitiwa na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga wakati wa semina kuhusu fursa zitakazopatikana kutokana na Mradi huo, inayoendelea jijini Tanga tarehe 27 hadi 29 Septemba, 2021.



Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akizungumza na Wakuu wa mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa minane ambayo itapitiwa na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga, kuhusu umuhimu wa kutengeneza mazingira mazuri ili kupata fursa zitakazotokana na utekelezaji wa Mradi huo, wakati wa semina, inayoendelea jijini Tanga tarehe 27 hadi 29 Septemba, 2021



Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Adam Malima akiwakaribisha Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa minane ambayo itapitiwa na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga wakati wa semina kuhusu fursa zitakazopatikana kutokana na Mradi huo, inayoendelea jijini Tanga tarehe 27 hadi 29 Septemba, 2021.

 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...