Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Watani wa Jadi, Yanga na Simba wameendelea kuunga mkono kutangaza Utalii wa Tanzania katika nyanja tofauti ikiwemo Mlima maarufu duniani, Mlima Kilimanjaro, visiwa vya Zanzibar na utajiri wake wa Ndege za ATCL kwa kushawishi wa Watalii kote duniani.
Yanga SC wanatangaza utalii wa nchi kupitia utalii wa michezo (Sports Tourism) wakiweka Nembo ya Mlima Kilimanjaro na Visiwa vya Zanzibar katik Jezi zao, ikiwa sambamba na kuunga mkono kampeni ya Rais wa Jamhuri ya ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii wa nchi kupitia kipindi maarufu cha Royal Tour.
Akizungumza leo Septemba 17,2021 jijini Dar es Salaam Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumaro amewapongeza Yanga SC kuleta wazo hilo la kuutangaza Utalii wa Taifa, kupitia safari zake za Kimataifa katika mchezo wake wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United FC ya Nigeria na michezo mingine kama itafanikiwa kufuzu raundi inayofuata.
“Yanga SC wameweka nembo ya Mlima Kilimanjaro, visiwa vya Zanzibar katika Jezi zao zote, ili kutangaza utalii wa Tanzania bure kabisa bila hata malipo, lakini kama wangetaka pesa basi ingekuwa zaidi ya Bilioni 1 za Kitanzania kuweka nembo hii kwenye Jezi hizo”, amesema Dkt. Ndumbaro.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga SC, Haji Mfikirwa amesema Yanga inafanya hayo yote kuunga mkono jitihada za Tanzania kuendelea kutangaza utalii wake, na kwamba hiyo ni kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mashabiki ndani na nje ya nchi kitendo kinachoweza kuvutia idadi kubwa ya Watalii duniani.
Wakati huo huo Klabu ya Simba ambayo nayo iliingia mkataba na Wizara ya Maliasili na Utalii kuutangaza utalii wa Tanzania kupitia Kampeni ya Visit Tanzania, leo Septemba 17 wameingia mkataba na Shirika la Ndege Tanzania( ATCL) .
Katika mkataba huo Simba SC itatumia Shirika la ATCL kufanya safar zake za ndani na nje ambapo mkataba unaeleza kutakuwa na fursa ya Simba kupata baadhi ya Tiketi za bure za Klabu hiyo pindi inaposafiri. Sambamba na kila mmoja kupata faida katika huduma zake. Mkataba huo wa miaka miwili na umegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 400.
Akizungumzia mkataba huo Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi amesema mkataba huo utatoa fursa kwa kila Kampuni kufaidika katika huduma zake, amesema ATCL watatoa baadhi ya Tiketi za safari bure kwa Simba SC na kutangaza baadhi ya kampeni za Shirika hilo.
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez ameeleza makubaliano hayo ya mkataba yalianza mapema Aprili, na kwamba watafaidika kupata punguzo kwa baadhi ya Tiketi na kupata nyingine bure katika safari zao kuelekea kwenye mashindano mbalimbali.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro (kushoto) akionesha Nembo ya Mlima Kilimanjaro na visiwa vya Zanzibar katika Jezi ya Klabu ya Yanga, kulia ni Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Eng. Hersi Said. Nembo hiyo itakuwa kwenye Jezi ya Yanga SC kwa ajili ya kutangaza Utalii wa Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi (kushoto) akikabidhi mkataba wa ushirikiano kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez, mkataba huo wa miaka miwili kila Kampuni itafaidika na mashirikiano hayo ikiwa pamoja na Tiketi, Kampeni mbalimbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...