Na Joseph Lyimo
WANANCHI wa Mitaa mitano ya Kata ya Kaloleni Mji mdogo wa Kibaya Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, wanatarajia kunufaika na mradi wa maji kupitia fedha za Uviko-19 zilizotolewa na Serikali.
Kwa hali ya sasa ilivyo upatikanaji wa maji kwenye wilaya ya Kiteto kwa wananchi wake ni asilimia 52 na mji mdogo wa Kibaya ni asilimia 44.
Mbunge wa Jimbo la Kiteto, wakili Edward Ole Lekaita akizungumza juu ya mradi huo amesema kiasi cha shilingi milioni 400 zimetolewa na Serikali kupitia fedha za Uviko-19 ili zisambaze maji kwa wananchi.
Ole Lekaita amesema ujenzi wa tenki la maji la mita za ujazo 300 (lita 300,000) litajengwa katika Mlima wa Seriani (Majengo Mapya), kwenye Kata ya Kaloleni.
“Usambazaji wa mabomba ya maji utakuwa takribani kilomita 10.6 kwenda mitaa ya Kaloleni, Majengo mapya, Msikitini, Vumilia na Shilangaa,” amesema Ole Lekaita.
Amesema fedha hizo pia zitatumika kwenye ununuzi na ufungaji wa pampu mbili, ujenzi wa nyumba ya mitambo na uzio, ujenzi wa vituo vitatu vya kuchotea maji.
Amesema kuhusu chanzo cha maji ya bomba katika mitaa hiyo mitano ni mwaka 2019/2020, ahadi ya Waziri wa Maji kuongeza vyanzo vya maji mji wa Kibaya, kisima cha majengo Mapya kilichimbwa.
Amesema kisima hicho kina urefu wa mita 160 na kina uwezo wa kuzalisha maji mita za ujazo 18 kwa saa (Lita 18,000 kwa saa).
Wakati wa kampeni ya uchaguzi 2020, Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Ole Lekaita alimuomba aliyekuwa Makamu wa Rais wa wakati huo Samia Suluhu Hassan ambaye hivi sasa ni Rais alipotembelea Kiteto Septemba 27 mwaka 2020 asaidie juu ya tatizo la uhaba wa maji katika mjini wa Kibaya.
“Lakini vile vile wakati nachangia bajeti ya maji mwaka wa fedha wa 2021/2022 nimweleza Waziri wa Maji Juma Awezo kuhusu tatizo la maji katika mji wa Kibaya,” amesema Ole Lekaita.
Hata hivyo, Mbunge huyo amewaomba wananchi wa mitaa yote mitano kutoa ushirikiano wa kurahisisha upatikanaji wa maeneo ya kutandaza mabomba ya kusafirisha maji yatakayo kuwa kwenye tenki moja Mlimani Seriani na mitaani kutakapolazwa mabomba.
“Wananchi wanaombwa kuchangia nguvukazi ambayo italipiwa kuchimba mitaro ya kutandaza mabomba ya maji, tujitolee na tuchangie upatikanaji wa maji ya bomba mitaani mwetu,” amesema Ole Lekaita.
Amesema kukamilika kwa mradi huo imepangwa kuwa, ifikapo Mei 30 mwaka 2022 na maji ya bomba yaanze kutumika ndani ya mitaa hiyo mitano.
Ametoa shukrani zake za dhati kwa wananchi wa Jimbo la Kiteto kwenda kwa Serikal ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha za Uviko-19 na nyingine kwa manufaa ya Taifa.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Kiteto, wamempongeza mbunge huyo kwa kuwasemea Bungeni juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Mkazi wa kata wa Kaloleni Sabebe amesema baada ya mradi huo kukamilika wanamuomba mbunge huyo afanikishe upatikanaji wa kituo cha afya ili wanawake na watoto wapate huduma kwa ukaribu.
Mkazi wa wilaya hiyo Sisca Seuta amesema wananchi wa Kiteto wanapaswa kumpa ushirikiano mbunge huyo kwenye kipindi hiki cha miaka mitano ili aweze kupambania maendeleo.
“Kwa namna moja au nyingine mradi huo wa maji utawanufaisha wananchi wa eneo hilo hasa wanawake ambao kwa kawaida wao ndiyo huwa na wakati mgumu kwa kufuata huduma hiyo mbali na nyumbani,” amesema Seuta.
Mkazi wa kata ya Kaloleni Seleman Hassan amesema wanashukuru kupitia fedha hizo za Uviko-19 ambazo zimewanufaisha kwenye mradi wa maji hivyo jamii kunufaika.
Mwanafunzi wa shule ya msingi Kaloleni Mussa Hamis amesema mradi huo wa maji ukikamilika utakuwa msaada mkubwa kwao na jamii nzima ya eneo hilo.
"Tatizo la kufuata mbali huduma ya maji litafikia ukingoni na sasa hatutateseka tena kama awali, tunamshukuru mbunge kwa hatua hii ya kufanikisha mradi wa maji kupitia fedha za Covid-19," amesema.
Mwanafunzi wa darasa la tano wa shule ya msingi Kaloleni Asha Idd amesema mradi huo utawanufaisha na kuwapa muda mzuri wa kusoma kuliko kutembelea umbali mrefu kufuata huduma ya maji.
"Kiwango cha ufaulu kitapanda kwa sisi wanafunzi kwani hatutatembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji hivyo tunaishukuru mno serikali kwa mradi huu," amesema Asha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...