Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO  

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka Wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kujiepusha kutumia usafiri wa wananchi wanaoshitakiana wakati wa kwenda uwandani ili kuepuka tuhuma za kufanya upendeleo wakati wa kusikiliza mashauri.

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo tarehe 27 Oktoba 2021 mkoani Morogoro wakati akishuhudia uapishwaji wajumbe wapya wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Morogoro uliofanywa na Mkuu wa mkoa huo Martine Shigela.  Baraza la Ardhi na Nyumba la Morogoro linahudumia halmashauri tatu za Mvomero, Morogoro Vijijini na Manispaa ya Morogoro.

‘’Ninaomba hili mliepuke sana maana linaleta changamoto kubwa, na mwingine anaweza akakata rufaa akidai mwenzake alikuwa anawapeleka wajumbe uwandani, suala hilo limekuwa likileta shida sana’’ alisema Dkt Mabula.

Wajumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya wana jukumu la kusikiliza kesi na kutoa maoni juu ya shauri husika kwa maandishi na wakati wa kusikiliza shauri wana wajibu wa kuhoji maswali ya ufafanuzi ili kupata uelewa zaidi.

Maoni ya wajumbe yanatumika kumsaidia Mwenyekiti wa Baraza kutoa maamuzi ingawa ni lazima Mwenyekiti ajikite katika sheria hivyo anaweza kuyakubali maoni hayo au kuyakataa lakini lazima atoe sababu za kuyakataa.

Dkt Mabula alisema, Wizara inachoshauri ni Mwenyekiti wa Baraza awe na ratiba ya mwezi mzima kuhusiana na safari za kwenda uwandani  na taarifa iwasilishwe kwa Mkuu wa wilaya pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri husika ili inapofika siku ya kwenda uwandani basi watumie usafiri wa serikali.

Aliongeza kwa kusema kuwa, kutumia usafiri wa serikali kutaepusha minong’ono na kumkosesha amani mmoja wa miongoni mwa wanaoshitakiana kwa kuhisi kuwa anaweza kuwa anaonewa.

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ametaka mashauri katika Mabaraza ya Ardhi kumalizika katika kipindi kisichozidi miezi sita labda kwa yale mashauri ambayo yanaweza kucheleweshwa kwa sababu za mawakili.

‘’Naomba katika kupangilia kesi zisiwe zinapelekwa mbali sana kiasi cha kujikuta mtu anasota mwaka mmoja, miaka miwili kesi haijaisha tutakuwa hatiujawatendea haki’’ alisema Dkt Mabula.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela aliwapongeza wajumbe wa Baraza walioteuliwa na kuwaeleza kuwa uteuzi walioupata umezingatia uadilifu na weledi wao na ana matumaini wajumbe hao wataenda kutenda haki kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

‘’Nina matumaini katika nafasi hii mliyoipata mtaenda kutenda haki katika mashauri kwa watu watakaofika kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba na hatutarajii kuona uadilifu unapungua mahali ambapo wananchi wanaenda kupata haki kuwa sehemu ya kuilalamikia’’ alisema Shigela.

Jumla ya wajumbe wanne wa Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Morogoro waliapishwa kuhudumu kwenye baraza hilo na sababu ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba kuketi na wajumbe katika kusikiliza mashauri ni kushirikisha jamii kwenye utatuzi wa migogoro ya ardhi na wajumbe hao wana msaada mkubwa katika utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Morogoro Mwanahawa Kassim hadi kufikia septemba 2021 katika wilaya ya morogoro Manispaa, Morogoro Vijijini na Mvomero kuna jumla ya mashauri 1,220 ambapo kati ya mashauri hayo  yaliyofunguliwa kwa mwezi septemba pekee ni 57 na yaliyoisha mwezi huo ni mashauri 114.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Wa tatu kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela wakishuhudia kuapa kwa mmoja wa Wajumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Morogoro tarehe 27 Oktoba 2021 baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo.

Mmoja wa Wajumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Morogoro (kulia) akiapa wakati wa uapisho wa wajumbe wanne wa Baraza hilo uliofanywa na Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela 

Mjumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Morogoro Elia Petro Mpesa akisaini baada ya kuapa kuwa mjumbe wa baraza hilo

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (kushoto aliyekaa) na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela wakiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Morogoro tarehe 27 Oktoba 2021. Kushoto ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro Frank Minzikunte na wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba wilaya ya Morogoro Mwanahawa Kassim.

……………………………………………………

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...