Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amefanya ziara ya kushtukiza ofisi ya ardhi ya halmashauri ya jiji la Dodoma na kuagiza maombi 521 ya umilikishaji ardhi katika ofisi hiyo kukamilishwa ndani ya siku tatu.
Akiwa ameambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo na Menejimenti ya Wizara katika ziara hiyo tarehe 25 Oktoba 2021 jiji Dodoma, Dkt Mabula alisema, pamoja na kuwepo changamoto lakini anachohitaji maombi 521 yawe yamekamilika katika kipindi cha siku tatu.
‘’Kuanzia sasa tunahitaji zile ‘application’ zote ambazo hati zake watu wameomba zitoke ndani ya siku tatu kama ni kutoka saa nane za usiku tunahitaji hiyo kazi ikamilike ndani ya siku tatu’’ alisema Dkt Mabula.
Aidha,aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi katika jiji la Dodoma kuandaa hati zisizopungua mia moja kwa siku moja sambamba na kuwataka kumhakikishia kwa maandishi ahadi walizompa katika kutekeleza maagizo yake.
Uamuzi wa Naibu Waziri wa Ardhi kufanya ziara ya kushtukiza ofisi ya ardhi katika jiji la Dodoma unafuatia kujitokeza baadhi ya malalamiko ucheleweshaji umilikishaji ardhi kwa wananchi wa mkoa wa Dodoma jambo lililofanya wizara kuanza mkakati maalum wa ukwamuaji na uharakishaji utoaji hati kwenye jiji hilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...