Charles James, Michuzi TV
MBUNGE wa Jimbo la Chamwino Mkoani Dodoma ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maji kwa kutoa kiasi cha Sh Milioni 32 kwa ajili ya kukamilisha mradi mkubwa wa maji utakaohudumia wananchi wa Kata ya Izava na vijiji vyake.
Ndejembi pia ameeleza kuwa katika jitihada zake za kuinua kiwango cha elimu jimboni kwake pia amepatiwa kiasi cha Sh Milioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu ambapo fedha hizo amezielekeza katika ujenzi wa Maabara kwenye Shule ya Sekondari ya Segala iliyopo katika Kata hiyo.
Hayo ameyasema akiwa kwenye ziara yake ya Kata kwa Kata katika Jimbo lake hilo ambapo amezungumza na wananchi wa Kata ya Segala na Izava na kuwaeleza mafanikio ambayo ndani ya kipindi chake cha miezi nane toka ateuliwa ameyapata.
"Ndugu zangu katika jambo ambalo kwangu nalipa uzito na kipaumbele zaidi kwenye Jimbo langu ni suala la Elimu, ni lazima tuandae kizazi kilicho bora ambacho kitakua na elimu bora, Nimshukuru sana Rais Samia kwa kutupatia Sh Milioni 30 ambazo tumezielekeza kwenye ujenzi wa Maabara hapa Sekondari ya Segala.
Lakini pia tumepata mradi wa Maji utakaogharimu kiasi cha Sh Milioni 32 ambapo tutachimba kisima kikubwa kitakachohudumia wananchi wa Kata ya Izava na vijiji vyake, Nimshukuru sana Rais kupitia Wizara ya Maji Waziri Jumaa Aweso ameidhinisha fedha hizo na sasa changamoto ya Maji Izava inakwenda kuwa historia,"Amesema Ndejembi.
Akiwa kwenye ziara hiyo Mbunge Ndejembi amewahamasisha pia wananchi wake kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa UVIKO-19 huku akiwataka kuacha kuwasikiliza watu wanaopotosha kuhusu Chanjo ambapo ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kupata Chanjo inayotolewa bure na Serikali.
"Pamoja na jitihada za kufanya maendeleo niwashauri sana kuchukua tahadhari ya Corona kwa kujitokeza kuchoma chanjo, wapo watu wanaopotosha kuwa Chanjo ni mbaya msiwasikilize hakuna mtu aliyechoma chanjo hii akadhurika jitokezeni kuchanja.
Serikali ya Rais Samia inajali wananchi wake ndio maana imeleta chanjo hizi na zinapatikana bure kuanzia kwenye Zahanati zetu Vituo vya Afya na Hospitali, Mimi Mbunge wenu nimechanja tuchukue tahadhari huu ugonjwa upo na unaua, tujikinge sisi wenyewe na wenzetu kwa kuchoma chanjo,"Amesema Ndejembi.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi akisalimiana na wananchi wa Kata ya Segala jimboni kwake.
Mbunge wa Jimbo la Chamwino Mkoani Dodoma Deo Ndejembi akikagua miradi ya elimu kwenye Kata yake ya Segala.Mbunge wa Jimbo la Chamwino Mkoani Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi akizungumza na wananchi wa Kata ya Izava katika Jimbo lake la Chamwino alipofika kuzungumza nao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...