Na. John Mapepele, WUSM
Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amesema Tamasha la 40 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo lililomalizika Oktoba 30, 2021 mjini Bagamoyo limetia fora kutokana na uratibu mzuri uliofanywa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na wadau wengine.
Mhe Kikwete ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo Oktoba 31, 2021 wakati akifunga Tamasha hilo ambapo amesisitiza kuwa limeunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kutangaza utamaduni wa Tanzania ambapo pia amepongeza kwa kushirikisha mataifa mbalimbali na kulifanya kuwa la kihistoria na kimataifa zaidi.
Amefafanua kwamba, hivi karibuni Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliandaa filamu ya Royal Tour iliyohusisha ziara kwenye mji wa Bagamoyo kwa ajili ya kutangaza utamaduni wa mtanzania.
Pia, amesifu uratibu wa siku ya mwisho la Tamasha la Kimataifa la Bagamoyo wa kuandaa ziara kama ya mama Samia iliyoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Abdallah, iliyoitwa jina la “Bagamoyo Royal Tour” iliyowajumuisha wasanii wa fani mbalimbali kama vile muziki, filamu, sanaa za ufundi, urembo na waandishi wa habari kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii katika mji wa Bagamoyo na baadaye mbuga ya Saadan.
Dkt. Abbasi ndiye pia aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kuandaa Royal Tour ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan
Aidha, Mhe. Kikwete ameipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kutumia Tamasha hili kutoa huduma ya ushauri na kuchanja ugonjwa wa Uviko -19 na kupima UKIMWI kwa hiari kwenye Tamasha hilo.
Katika Tamasha hilo Mhe. Kikwete amefafanua umuhimu wa sekta hizi kwa Taifa letu ambapo amesema kutokana na umuhimu wa Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo, haijawahi kutokea kuachwa kuundiwa Wizara katika awamu zote toka enzi ya Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere na kwamba kutokana na umuhimu huo Rais Samia ameendelea kuzibakiza na kuiziboresha.
“Wizara iliundwa kuukuza utamaduni wetu na utamaduni wetu ndiyo kielelezo cha Mtanzania”. Ameongeza Mhe. Kikwete
Ameipongeza Wizara kwa kuendelea kuboresha sekta za Sanaa na Utamaduni kupitia taasisi zake za Bodi ya Filamu, COSOTA, BASATA na BAKITA na kuzitaka ziendelee kusimamia na kusaidia kazi za Wasanii ili waweze kunufaika nazo.
“Nimefurahi kuona siku hizi mnawatengenezea Wasanii mazingira bora zaidi hivyo watafaidi matunda ya kazi zao”. Ameongeza Mhe. Kikwete.
Amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kutambua na kuthamini kazi nzuri ya kutwaa Kombe la COSAFA iliyofanywa na Timu ya Taifa ya Wanawake ya Mpira wa Miguu (Twiga Stars)
Siku ya mwisho ya Tamasha la Bagamoyo ilikuwa ni maalum kwa ajili ya Muziki wa Singeli ambao amesema yeye ni miongoni mwa wapenzi wa muziki huo wenye asili ya utamaduni wa nchi yetu.
Wasanii mbalimbali wa Muziki wa Singeli wakiongozwa na Sholo Mwamba wametamatisha Tamasha hilo kwa kutumbuiza nyimbo mbalimbali za singeli zilizowapagaisha washiriki na wananchi waliokuja kushuhudia Tamasha hilo na kujikuta wamekuwa sehemu ya wachezaji ya singeli badala ya wasikilizaji na watazamaji.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapa moyo Wizara kuendeleza Tamasha hilo lenye historia katika Taifa la Tanzania.
“Pia kwa dhati kabisa nitumie fursa hii adhimu kumshukuru mama yetu, Mhe. Rais kwa kuona changamoto ya ufinyu wa bajeti unaoikabili Wizara yetu, hivi karibuni ameelekeza Wizara yetu na Wizara ya Fedha kukaa pamoja ili kufanyia kazi changamoto hii” ameongeza Mhe. Gekul
Amefafanua kuwa Tamasha hili ndiyo Tamasha kongwe zaidi nchini na limebeba historia ya Taasisi ya Chuo cha Sanaa Bagamoyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge
ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuthamini mchango wa Tamasha hili ambapo
ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara kuboresha tamasha hilo ambalo
amesisitiza kuwa lina faida kubwa siyo tu kwa wakazi wa Bagamoyo bali kwa taifa
zima.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...