Benki
ya Biashara ya Tanzania (TCB) imedhamiria kuinua hadhi ya wanawake
nchini kifedha kwa kuwawezesha kiuchumi na kuwasaidia kuwa wajasiriamali
shupavu kupitia mikakati mbalimbali endelevu.
Taasisi hiyo
kongwe ya fedha nchini imeweka bayana dhamira hiyo wakati wa Kongamano
la Wanawake na Biashara la tatu ililoliandaa hapa jana kuwasaidia
akinamama kuzing’amua na kuzitumia fursa za kibenki kwa ajili ya
maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.
TCB imesema
itatekeleza jukumu hilo adhimu kwa kuwa kinara wa huduma jumuishi za
kifedha za akinamama na kiongozi mbunifu wa huduma hizo sokoni.
Wakiongea
kwenye kongamano hilo, maofisa wake waandamizi walisema mafanikio ya
jitihada hizo yatatokana na mpango mkakati wa TCB wa kufanya mapinduzi
makubwa ya kuwahudumia akinamama.
Aidha, benki hiyo itawaonyesha
fursa zinazopatikana TCB na kuwaelimisha jinsi ya kufanya biashara
zenye tija. Pia suluhishi za kibenki zilizopo na mpya za kisasa zaidi
zitatumika kumkomboa mwanamke kifedha na kumshirikisha kikamilifu katika
ujenzi wa taifa.
Wataalamu hao walisema benki hiyo imejiandaa
vizuri kwa hilo. Iko imara kifedha, ni uhodari kidijitali na bingwa wa
ubunifu ikiwa na wigo mpana wa huduma na mtandao mkubwa wa kuzifikisha
popote kwa wakati.
“Tuna mtandao wa matawi makubwa 46, matawi
madogo 36, ofisi za wakala za Shirika la Posta Tanzania 120, ATM 84
ambazo zimeunganishwa na ATM 350 za mtandao wa Umoja Switch,” Kaimu
Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Bw Moses Manyatta alibainisha.
Alisema
itakuwa rahisi kuwafikia wanawake wengi na kusaidia kuwawezesha kupitia
matawi na vituo vyake vya huduma vilivyosambaa kote Tanzania Bara na
Visiwani.
"Pamoja na vikwazo vingi vya kiuchumi wanavyokumbana
navyo wanawake na changamoto za kifedha walizonazo, tutahakikisha ajenda
ya kuwezesha kiuchumi inafikia malengo yaliyokusudiwa," Bw Manyatta
alitabainisha.
"Kupitia makongamano haya, tunataka kubainisha
mahitaji maalumu ya kifedha ya akinamama na kuihudumia sehemu hii kubwa
ya soko kwa namna ya kipekee,” aliongeza.
Mikutano kama hiyo pia
itaandaliwa Zanzibar, Tanga, Arusha na Dar es Salaam kama jukwaa la
kuwakutanisha akinamama kujifunza mambo mbalimbali na kuijua zaidi Benki
ya TCB na huduma zake.
Kongamano la Wanawake na Biashara la TCB
la ufunguzi lilifanyika mwanzoni mwa mwezi huu jijini Dodoma. La jana
lililofunguliwa rasmi na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Mhe. Angeline Mabula (MB), na liliwajumuisha washiriki wapatao
400 waliotumia mijadala ya pamoja kubadilishana uzoefu, kujuana na
kujifunza kutoka kwa wajasiriamali waliofanikiwa.
“Lengo kuu la
kuwa na utaratibu huu wa makongamano ya akinamama ni kusaidia kuongeza
mchango wao katika uchumi wa taifa kupitia fursa mbalimbali hasa zile
zinazopatikana TCB,” Bw Manyatta alifafanua katika wasilisho lake.
Kiongozi
huyo alitumia takwimu za mafanikio ya TCB kwa kipindi cha mwaka 2007
hadi 2020 kuonyesha uwezo wa kifedha wa benki hiyo kutimiza jukumu hilo.
Mizania ya TCB ilikua kwa zaidi ya asilimia 1,000 hadi
takribani TZS trilioni 1.04 huku mikopo ikiongezeka kwa zaidi ya TZS
bilioni 580. Hadi sasa akinamama ambao ni nusu ya wateja milioni moja wa
TCB wamekopeshwa zaidi ya TZS bilioni 120.
Kuhusu makongamano
hayo ambayo mada yake kuu ni “Nafasi ya Mwanamke katika Kukuza Uchumi wa
Taifa”, Mhe. Mabula alisema yamekuja wakati muafaka na yataisadia
serikali kuhakikisha hakuna mwanamke anayeachwa nyuma kiuchumi na
kimaendeleo.
"Kupitia mpango huu, TCB itatoa mchango mkubwa
katika kubadilisha hadhi ya wanawake nchini kifedha na kiuchumi.
Nawapongeza kwa kuja na wazo hili na kuwekeza muda na rasilimali
kuhakikisha linafanikiwa," alisema Mhe. Mabula.
Aidha, aliitaka
benki hiyo isitoe mikopo yake kiholela bila kuhakiki miradi tarajiwa na
kutoa miongozo ya kuitumia mikopo hiyo vizuri.
Wachokoza mada
ambao wote walikuwa wafanyakazi wanawake wa TCB walisema mikutano hiyo
inalenga kuonyesha utayari na uwezo wa benki hiyo kuwasaidia wanawake
wajasiriamali.
Walisema TCB inazo fursa lukuki za kibiashara na
uwezeshaji kwa ajili yao kupitia huduma maalumu kama akaunti ya Tabasamu
na suluhishi mbalimbali kama zile za bima za Nishike Mkono Bima na
Kinamama Policy (sera). Naibu
Waziri, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi Angelina
Mabula (wapili kulia), pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa wa Benki ya
Biashara ya Tanzania TCB Bw Moses Manyatta, wakikata utepe kuashiria
uzinduzi rasmi wa kongamano lenye lengo la kutoa elimu ya ujasiriamali
lililoandaliwa na Benki ya TCB kwaajilio yakuwainua na kuwawezesha
wanawake wafanya biashara Mkoa wa Mwanza, wengine pichani kutoka kushoto
ni Meneja Masoko wa Benki hiyo Grace Majige na Meneja wa Bima wa TCB
Emanuel Kaganda na kulia ni Mkurugenzi wa Sheria wa Benki ya Biashara
ya Tanzania TCB Bi Mystica Mapunda Ngongi, hafla hiyo imefanyika leo
jijini Mwanza.
Naibu
Waziri, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi Angelina
Mabula, akikagua bidhaa alipotembelea moja ya banda la mfanya biashara
na mjasiriamali na mteja wa Benki ya TCB wakati wa uzinduzi rasmi wa
kongamano lenye lengo la kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake
wafanya biashara lililoandaliwa na Benki ya TCB kwaajili ya kuwainua na
kuwawezesha wanawake wajasiriamali Mkoa wa Mwanza, wengine ni maofisa
wa Benki hiyo.
Naibu
Waziri, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi Angelina
Mabula akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa kongamano lenye
lengo la kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake wafanya biashara
lililoandaliwa na Benki ya TCB kwaajili ya kuwainua na kuwawezesha
wanawake wajasiriamali Mkoa wa Mwanza Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa wa Benki ya Biashara ya Tanzania TCB Bw Moses
Manyatta, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa kongamano
lenye lengo la kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake wafanya biashara
lililoandaliwa na Benki ya TCB kwaajili ya kuwainua na kuwawezesha
wanawake wajasiriamali Mkoa wa Mwanza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...