Afisa Msimamizi kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Bakari Kapera (mwenye tisheti ya njano) akiwaelimisha wafanyabiashara wa soko kuu la Sumbawanga kuhusu matumizi ya mashine za EFD na masuala ya VAT wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango inayoendelea mkoani Rukwa.
Afisa Msimamizi kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Morgan Isdor (Kulia) akimuelimisha mfanyabiashara wa soko la Sabasaba mjini Sumbawanga kuhusu umuhimu wa kutumia mashine za EFD na masuala mengine yanayohusu kodi wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango inayoendelea mkoani Rukwa.
Afisa Msimamizi kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Joel Frael (Kulia) akimuelimisha mfanyabiashara wa duka la nguo za wasichana mjini Sumbawanga kuhusu umuhimu wa kutumia mashine za EFD na kusikiliza changamoto zake za kibiashara wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango inayoendelea mkoani Rukwa.
Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Salome Mwandalanga (Kulia) akisikiliza malalamiko ya mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango inayoendelea mkoani Rukwa.
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imewataka wafanyabiashara mkoani Rukwa kuhakikisha kwamba wanatumia ipasavyo mashine za kutolea risiti za kielektroniki za EFD ili kurahisisha utunzaji wa kumbukumbu za biashara zao.
Hayo yamesemwa leo na Afisa Msimamizi wa Kodi wa TRA, Bw. Morgan Isdor wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango inayoendelea mkoani hapo ambapo amebainisha kuwa katika zoezi la kuwatembelea wafanyabiashara katika eneo la soko la Sabasaba wamebaini matumizi hafifu ya mashine za EFD hususani kwa wafanyabiashara wenye maduka madukwa.
“Katika mambo tuliyoyaona katika soko la Sabasaba hapa Sumbawanga ni matumizi hafifu yam ashine za EFD lakini pia wafanyabiashara wengi hawatundiki TIN namba zaio sehemu sahihi inayopaswa kutundikwa, kwahiyo tumewaelimisha kwamba wanapaswa kutumia vizuri mashine za EFD kwa kutoa risiti halali kwa kila manunuzi ya bidhaa ama huduma inayotolewa”, alisema Morgan.
Aliongeza kuwa, ni wajibu wa kisheria kwa kila mfanyabiashara anayetumia mashine ya EFD kuhakikisha kwamba risiti inayotelewa iendane na kiwango kile kilicholipwa na mteja na wateja nao sharia inawataka kuhakikisha kuwa wanadai risiti sahihi kulingana na bidhaa au huduma waliyopokea kutoka kwa wafanyabiashara.
Kwa upande wao walipakodi mkoani hapo wametoa maoni yao kuhusu huduma ya kutembelewa madukani mwao na TRA na kuelimishwa kuhusu masuala mbalimbali ya kodi na ambapo wamesema kwamba, zoezi la TRA kupita katika maduka yao kwa kutoa elimu, kusikiliza kero zao kumewarahisishia wafanyabiashara wengi kwasababu kunaokoa muda mwingi ambao ungepotea wa wao kwenda katika ofisi za TRA.
Bwana Mhena Said ambaye ni mfanyabiashara anayejishughulisha na masuala ya usafirishaji mkoani Rukwa anaeleza namna gani alivyoipokea kampeni ya elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango ambapo anasema kuwa, elimu inayotolewa na TRA inaridhisha tofauti na hapo mwanzo ambapo Maafisa wa TRA walikua wanaogopwa.
“Zamani sisi tulikua tukiwaona maafisa wa TRA au gari zao tulikua tunakimbia kujificha na maduka tunafunga, lakini kwa sasa hivi hiyo hali haipo na kodi tunalipa kwasabau hatuna woga tena, tunakaa nao mezani tunakadiriwa kodi na tunalipa, kwahiyo hili zoezi la utoaji elimu kwa sisi wafanyabiashara ni zuri sana”, alisema Mhena.
Kampeni ya elimu kwa mlipakodi ni zoezi endelevu ambalo TRA inaendesha katika mikoa mbalimbali nchini ambapo kwa sasa zoezi hilo lipo katika mikoa ya Rukwa, Ruvuma na Njombe na lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba elimu ya kodi inawafikia walipakodi wote katika maeneo yao ili kodi stahiki iweze kukusanywa ikiwemo kuwafanya walipakodi waweze kulipa kodi zao kwa hiari.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...