Mmoja wa wafaidika wa Mafunzo ya wadada wa kazi akitoa Mafunzo kwa wasichana wengine wa Kata ya chanika
Mmoja wa wasichana aliyepatiwa mkataba Ramla Nassoro akiendelea na kazi zake nyumbani kwao eneo la Pugu Station.
Na Humphrey Shao, Michuzi TV
WITO umetolewa kwa waajiri kuweza kuwapatia mikataba wadada wanaofanya kazi za ndani hili waweze kupata stahili zao hata wanapoamua kuachana na kazi hiyo.
Baadhi ya wasichana wa kazi za nyumbani katika Kata ya Kipunguni Jijini Dar es Salaam wameanza kupatiwa mikataba ya kazi na waajiri wao ili kulinda usalama wa ajira zao.
Mmoja wa wasichana aliyepatiwa mkataba Ramla Nassoro (18) amesema baada ya kuhudhuria semina hiyo alimshirikisha mwajiri wake ambaye alikubali kumpatia mkataba wa kazi.
"Mkataba nimeridhika nao na nimefarijika kwa sababu sasa hivi naishi na kufanya kazi kwa uhuru, najua haki zangu na majukumu yangu. Nawashauri waajiri wengine kuwapa mikataba ya kazi wafanyakazi wao," amesema Ramla.
Mwajiri wa msichana huyo, Asha Dilangale, amesema alihamasika kumpa mkataba mfanyakazi wake baada ya kuelimishwa kuhusu umuhimu wa mkataba wa kazi kwani unamlinda mfanyakazi na mwajiri pia.
"Nilimruhusu msichana wangu kwenda kupata mafunzo alivyorudi alinieleza aliyojifunza akaniambia kwamba tunatakiwa tuishi kimkataba. Mimi niliona ni jambo sahihi nilimchukulia kama mfanyakazi mwingine nikaamua kumuandalia mkataba," amesema Asha.
Hatua hiyo ni matokeo ya mradi wa Wezesha Uelewa wa Haki zuia rusha ya ngono ndani ya jamii unaotekelezwa na Sauti ya Jamii Kipunguni na kufadhiliwa na Women Fund Tanzania Trust.
Kupitia mradi huo Sauti ya Jamii Kipunguni iliendesha mafunzo kwa wafanyakazi wa kazi za majumbani juu ya uelewa wa haki, madhara ya rushwa ya ngono na kuripoti vitendo vya ukatili kwenye mamlaka husika.
Aidha amesema anaendelea kuwahamasisha waajiri wengie wenye wasichana wa kazi za ndani waweze kuwapatia mikataba ili waishi kwa amani na uhuru.
Aidha kupitia mradi huo hamasa ya kudai haki imeongezeka ambapo Ratifa Mussa ambaye pia alihudhuria mafunzo hayo amehamasika kwa kuanza kuwapa elimu wasichana wengine waweze kutambua haki zao na kutambua madhara ya rushwa ya ngono.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Selemani Bishangazi, amesema walitoa semina ya madhara ya rushwa ya ngono na uelewa wa haki kwa wadada wa kazi 120 kutoka Kata ya Kipunguni.
"Wafanyakazi wa majumbani wana haki ya kuthaminiwa ndiyo maana tunawahamasisha wawe na nguvu ya kupambana na unyanyasaji kwa sababu wengi wanafanya kazi katika mazingira magumu na hawana mikataba ya ajira," amesema Bishangazi.
Mradi huo unalenga kuendeleza kampeni ya kuzuia rushwa ya ngono kwa wafanyakazi wa kazi za majumbani na wanawake wenye ndoto za kuwa viongozi, umuhimu wa kuripoti vitendo vya ukatili kwenye mamlaka husika na kudai haki na kuwajibika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...