Na Jane Edward, Arusha
Baadhi ya viongozi na wanasiasa mkoani Arusha wameelezwa kuwa kikwazo katika ukusanyaji wa Maduhuli ya maji kwa kuwashawishi wananchi wasichangie gharama za Maji Kwa madai kwamba Maji yanaletwa na mungu hali inayofifisha jitihada za serikali katika kutoa huduma ya maji vijijini.
Akifungua kikao kazi Cha vyombo vya watoaji Huduma ya maji ngazi ya Jamii (CBWSOs)na wadau wa sekta ya maji vijijini ,mkoani hapa ,Katibu Tawala msaidizi Mkoa wa Arusha David Lyamongi alisema uchangiaji wa Huduma za Maji ni muhimu katika kukamilisha miradi endelevu ya Maji inayojengwa.
Alisema Serikali imekuwa ikitekeleza miradi mingi ya Maji Kwa gharama kubwa ,lakini kumekuwepo na changamoto ya uendelevu wa miradi hiyo ,hivyo Serikali ikaona umuhimu wa kuunda vyombo vya watoa huduma za maji ngazi ya Jamii ili kukabili changamoto hizo.
Alisema malengo ya Serikali ni kuhakikisha upatikanaji wa Maji vijijini unafikia asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.
Lyamongi amewataka Ruwasa na kamati ya watoa huduma za Maji ngazi ya Jamii kuendelea kutoa Elimu Kwa Jamii juu ya ulindaji na uhifadhi wa vyanzo vya Maji ,usimamizi Bora wa miradi ya maji,pamoja na ukusanyaji na matumizi ya maduhuli ya maji.
Alisema Mkoa wa Arusha ulikuwa na kamati za usimamizi na utoaji wa huduma ya maji katika vijiji 99 vilivyoundwa katika Sheria namba 12 ya mwaka 2009 na mwaka 2019 bunge lilipitisha sheria namba 5 kuhusu sera ya Maji iliyoanzisha wakala wa Maji na usafi wa mazingira vijijini( RUWASA) na kufanikiwa kuhuisha kamati 85 hadi oktoba mwaka huu.
Awali meneja wa Ruwasa Mkoa wa Arusha ,mhandisi Joseph Makaidi alisema Ruwasa imefanikiwa kuhuisha na kusajili vyombo vya watoa huduma za maji ngazi ya Jamii CBWSOs kufikia 85 sawa na asilimia 88.8 .
Alisema CBWSOs inakuwa na jukumu la kusimamia skimu za Maji zipatazo 212 zenye jumla ya vituo 5676 Kati ya hivyo 4386 vinatoa huduma na 768 havitoi huduma na 522 vinatoa huduma lakini vinahitaji matengenezo.
Mhandisi Makaidi alisema changamoto kubwa zinazowakabili ni pamoja na viongozi kutohamasisha wananchi kuhusu uhuishaji wa Vyombo Kwa kuwa wanufaika na maduhuli ya maji na hivyo kukosesha Mapato.Pia alisema baadhi ya wananchi wamekosa Elimu ya uchangiaji wa gharama za Maji wakiamini kwamba Maji yameletwa na mungu hivyo hawahitaji kuchangia.
Kwa upande wake meneja wa Ruwasa wilaya ya Monduli Mhandisi Neville Msaki alisema kuwa wilaya ya Monduli inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vyanzo vya maji hali iliyopelekea vijiji 13 kukosa Maji kabisa Kutokana na tatizo hilo .
Katika kukabiliana na changamoto hiyo Ruwasa imeamua kukaa na Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Arusha (AUWSA)na kukubaliana kupeleka Maji katika baadhi ya vijiji ambavyo avina vyanzo vya maji ambapo alibainisha kuwa wamekubaliana vijiji 13 vitapatiwa maji yanayotokana na Mradi mkubwa wa Maji wa shilingi bilioni 520 uliopo jiji Arusha.
Alisema mapato yameanza kuongezeka tofauti na zamani kwani awali mapato ya jumuiya moja yalikuwa hayaridhishi kwani kabla ya kuanzishwa Kwa Ruwasa wilayani humo jumuiya moja ilikuwa ikikusanya laki tano hadi sita Kwa mwezi lakini baada ya kuanzishwa Ruwasa kumekuwa na ongezeko kubwa kwa sasa jumuiya Moja inakusanya hadi milioni mbili hadi tatu kwa mwezi.
Mhandisi Joseph Makaidi Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa wadau wa maji.
Wadau wa RUWASA wakiwa katika picha ya pamoja jijini Arusha.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...