Na Said Mwishehe, Michuzi TV 

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA) imesema iko katika mkakati wa kuhamasisha wanawake ambao wamekuwa wakitumia dawa za kulevya wanakwenda vituo vya matibabu kwa ajili ya kupata tiba.

Akizungumza leo Novemba 11,2021 na waandishi wa habari za mitandao ya kijamii walioko kwenye kikao kazi kilichaondaliwa na Mamlaka hiyo, Kamishna wa Kinga na Tiba Dk.Peter Mfisi ameeleza kwa sasa idadi ya wanawake wanaotumia dawa za kulevya wanaokwenda katika vituo vya matibabu ni wachache.

 "Kwa mfano ukiangalia katika Sober House unakuta kiwango cha wanawake wanaojitokeza kupata matibabu ni kidogo sana na hata ukichukua ile jumla ya matibabu wanawake bado wako chini ya asilimia tano. Katika kliniki nyingine unakuta wako asilimia tatu au asilimia nne kwa uwakilishi wa wanawake ni mdogo,"amesema Dk.Mfisi.

Hivyo amesema Serikali kupitia Mamlaka hiyo wanajaribu kutafuta njia itakayosaidia kuwahamasisha wajitokeze kwa wingi.Hawana uhakika wa kueleza wanawake wanaotumia wako asilimia ngapi lakini wanachojua wanaume wanaotumia ni wengi kuliko wanawake.

"Hawaendi kwenye vituo vya matibabu kwa hiyo mamlaka tunakila sababu ya kuweka vivuto maalum ili kuwafanya wanawake nao wajitokeze katika matibabu kwa wale ambao wamekuwa na uraibu wa dawa za kulevya, sehemu ya vivutio hivyo labda kutafuta kliniki itakayokuwa na mahitaji maalum ya wanawake ili wajitokeze kwa wingi.

"Hivyo tumeamua kuwaita waandishi wa habari katika kikao kazi hiki ili kusaidia kutafuta mbinu za kuwashawishi wanawake wafike kwenye maeneo ya tiba na kujiunga na vituo vya matibabu, maana tunajua wapo na wameathirika na dawa za kulevya lakini kwasababu ya unyanyapa wanaogopa kujitokeza,"amesisitiza.

Aidha amesema kuna baadhi ya wanawake wanashindwa kwenda kupata matibabu kwasababu ya muda kwani mara nyingi matibabu yanaanza saa 12 asubuhi hadi saa tano asubuhi, hivyo wanadhani ni vema wakaangalia na muda mwingine , yaani wawepo wanaokwenda asubuhi lakini wawepo wanaokwenda jioni kulingana na ratiba zao.

Dk.Mfisi amesema kimsingi tatizo lililopo wanawake hawajitokezi kwenda kutafuta matibabu na kama wanavyojua mtu anatafuta matibabu kwenye vituo vya Methadon haendi pale kwa ajili tu ya kupewa Methadon ili aachane na kutumia Heroine , bali wanawaangalia na matatizo mengine.

"Hawa wanawake wanaotumia dawa za kulevya wengine wana matatizo ya uzazi , hawawezi kupata watoto kwasababu ya kutumia dawa , lakini pia huenda baadhi yao labba wana tatizo la malezi kwa watoto waliona wakati mwingine hata akipata mimba mtoto aliyezaliwa naye anakuwa na uraibu.

"Mtoto anapozaliwa kwenye kituo cha matibabu yule mtoto anatibiwa , kwa hiyo tunahisi tutapokuwa na wanawake wengi kwenye hizi kliniki zetu tutawasaidia, wale wanaozaa watoto weye urabu watoto wao watatibiwa na watakuwa na afya njema,"amesisitiza.

VIPI KUHUSU MAMA ANAYETUMIA DAWA ZA KULEVYA?

Dk.Mfisi amesema iwapo mama mjamzito atakuwa anatumia dawa za kulevya inakwenda mpaka inafika kwa mtoto, kwa hiyo kila mama anapotumia na ile dawa inafika kwa mtoto anapokuwa tumboni, matokeo yake ni mtoto atakapozaliwa atakuwa anataka kupata dawa maana mwanzoni alikuwa anaipata kupitia kwa mama yake.

"Kwa hiyo mtoto atatakiwa kupewa dawa, hivyo anapozaliwa hospitali mtoto yule atapata matibabu , kwa hiyo atapewa dawa na ile hali itaisha, kwa hiyo tunasema mtoto anapozaliwa kwenye mazingira ya kliniki kama vile anasaidiwa.Hivyo ishu sio lazima tuwe na majengo mapya , tunaweza kutumia majengo yaliyopo lakin katika utaratibu maalum."

"Na hii kliniki inaweza kuwa na meneo ya kucheza watoto, kama mama amekuja na mtoto basi anampeleka kucheza au kunakuwa na elimu ya mama na mtoto, inakuwa zaidi ya ile kliniki ambayo mama anakwenda na kondoka , ukiacha kutibu hiyo arosto ambayo mtoto anakuwa nayo lakini kunakuwa na vitu vingine,"amesisitiza.

Kamishna wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Do.Peter Mfisi akifafanua jambo wakati wa kikao kazi kilichoandaliwa na Mamlaka hiyo kwa ajili ya waandishi wa habari hasa wanaoandika habari za mtandaoni.
Baadhi ya Waandishi wa habari wakiwa katika kikao kazi kilichoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambacho kinaendelea mkoani Morogoro
Kamishna wa Kinga na Tiba Dk.Peter Mfisi( wa kwanza kushoto)akifuatilia kikao kazi hicho.Wengine katika picha hiyo waandishi wa habari

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...