KAMATI ya Ulinzi na Usalama pamoja na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es Salaam wamepatiwa mafunzo kuhusu mfumo wa Maegesho Kidigitali
Mafunzo hayo yameendeshwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kuwajengea uwezo Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Madiwani hao kuhusu Mfumo wa malipo ya Maegesho kwa njia ya Kielektroniki (TeRMIS) unaotarajiwa kuanza kutumika Desemba 1, 2021 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Singida na Mwanza.
Mfumo wa Maegesho Kidigitali (TeRMIS) ni mfumo wa Kielektroniki wa usimamizi na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na maegesho ya vyombo vya moto (parking fee), matumizi ya Hifadhi za barabara (Road Reserve User Charges) pamoja na Adhabu kutokana na Ukiukwaji wa matumizi ya hifadhi za barabara.
Wameelezwa kwamba Mfumo wa Maegesho Kidigitali utadhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali kwani umeunganishwa na mfumo wa GePG (malipo ni kwa njia ya Control Number).
Pia mfumo huo umetoa muda muafaka kwa mtumiaji wa maegesho kulipia maegesho ndani ya Siku 14 baada ya kutumia maegesho endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo atatakiwa kulipa Ushuru wa Maegesho pmoja na faini ya Sh.10,000/=.
Kwa mujibu wa maelezo ya watalaam hao wamewaambia madiwani kwamba iwapo mtumiaji wa maegesho anapaswa kulipia Ushuru wa Maegesho Kidigitali baada ya kupatiwa namba ya malipo (control number) ambapo atatumia Kumbukumbu namba hiyo kulipia maegesho kwa kutumia mtandao wowote wa simu ya mkononi, Benki ya NMB na CRDB au kupitia kwa Mawakala wa Huduma za fedha.
Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, mtumiaji wa maegesho anatakiwa kulipa Sh.500 kwa Saa na Sh.2,500 kwa Siku. Mkoa wa Mwanza mtumiaji wa maegesho anatakiwa kulipa Sh.500 kwa Saa na Sh.1,500 kwa Siku.
Mkoa wa Iringa mtumiaji wa maegesho anatakiwa kulipa Sh. 300 kwa Saa na Sh.1,000 kwa Siku. Mkoa wa Dodoma mtumiaji wa maegesho anatakiwa kulipa Sh.300 kwa Saa na Sh.1,000 kwa Siku. Mkoa wa Singida mtumiaji wa maegesho anatakiwa kulipa Sh.300 kwa Saa na Sh.1,000 kwa Siku.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...