Na Mwandishi wetu
KITUO cha Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi cha Kahama (KEEC) ambacho kipo chini ya Baraza la Uwezeshaji Ofisi ya Waziri Mkuu kimeendesha mafunzo ya siku moja kwa wajasiriamali wenye ulemavu wa kusikia.
Washiriki 56 waliohudhuria mafunzo wametokea Manispaa ya Kahama na Wilaya ya Ushetu Mkoani Shinyanga ambapo baadhi yao walifika na bidhaa zao kwenye Ukumbi wa Kituo cha (KEEC).
Mafunzo hayo yameendeshwa kwa kushirikisha Ofisi tano za Uwezeshaji ambazo ni Baraza La Uwezeshaji, Halmashauri ya Ushetu, Mfuko wa Kilimo wa Pass Trust, Chama cha walemavu wa kusikia (CHAVITA) na Taasisi ya GS1.
Lengo la mafunzo hayo ni kuhamasisha wajasirialiamali kurasimisha biashara zao ili kukidhi viwango vya ushindani wa soko la Kimataifa.
Wakati wa ufunguzi, Mkuu wa Kituo hicho Bw.Jozaka Bukuku aliwahimiza wajasiriamali kuchangamkia fursa zinazopatikana ndani kituo ikiwemo mikopo yenye masharti nafuu,urasimishaji wa biashara, elimu ya mlipa kodi, dhamana za mikopo, taarifa za masoko n.k.
Bw.Jozaka Bukuku alizitaja Taasisi zilizopo kwenye Kituo kuwa ni pamoja na Baraza la Uwezeshaji, Benki ya NBC, Self-Microfinance MF, Mfuko wa Kilimo wa Pass trust, Mfuko wa Pembejeo (AGTF),Chuo cha ufundi stadi (VETA), Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO),Shirika la viwango TBS,Chuo Kikuu Huria (OUT),VICOBA FETA,Chemba ya Biashara (TCCIA) na Taasisi ya usalama kazini (OSHA).
Katika mazungumzo yake alihimiza wajasiriamali kutembelea kituo hicho kinachojumuisha Taasisi za Umma na binafsi ili kujifunza na kupata taarifa sahihi za masuala ya uwezeshaji.
“Kituo hiki ni cha mfano Kitaifa na hapa ndio sehemu sahihi kwenu kupata taarifa za uwezeshaji, kujifunza lakini pia kuna fursa za mikopo na dhamana za mikopo zenye mashari nafuu”alisema Jozaka Bukuku.
Nae Afisa masoko wa GS1 Tanzania, Shaban Mikongoti alieleza wajasiriamali umuhimu wa kurasimisha biashara zao kwa kuwa na misimbomilia ambazo zinatolewa na Taasisi yake.
“Misimbomilia ndio njia pekee inayoweza kusaidia bidhaa yako kupenya kwenye soko la ushindani wa Kimataifa na kujiongezea kipato”alisema Shaban.
“GS1 Tanzania tupo hapa Kituoni kwasababu hiyo kwani mbali na kuwasajilia Misimbomilia lakini tunawajibika kuwatafutia masoko yenye tija ili kunadi bidhaa zenu”aliongeza.
Bw.Shaban alimalizia kwa kuwataka wajasiriamali kuongezea thamani bidhaa zao ili kuziendesha biashara kisasa zaidi.
Kituo cha Kahama kimekuwa cha mfano kwa Halmashauri zote nchini katika kutekeleza agizo la Ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2020 2025 juu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia vituo vya Uwezeshaji.
Kituo kimekuwa jawabu la kuondoa adha ya Wananchi kutafuta taarifa sahihi za biashara,ujuzi wa mambo ya kiuchumi, taratibu za urasimishaji wa biashara, taarifa za masoko, kuongeza thamani ya mazao, kufahamu fursa za hifadhi ya jamii, kupata elimu ya kodi na kufahamu fursa za mitaji.
KEEC imekuwa nyenzo muhimu inayosaidia baadhi ya Taasisi za Serikali ambazo zinatoa huduma mbalimbali kupata urahisi wa kuwafikia wananchi.
Walengwa wa kituo ni wananchi wote na wajasiriamali wakiwemo wadogo, wakati na wakubwa, Vikundi na Makampuni yaliyopo katika Sekta zote za kiuchumi.
Picha ya pamoja kati ya wawezeshaji na wajasiriamali baada ya kuisha kwa mafunzo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...