Na Grace Semfuko, MAELEZO Dar.
MAMLAKA ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya Tanzania DCEA, imeyataka makampuni ya usafirishaji wa mizigo kukagua kwa makini mizigo wanayoisafirisha ili kuepukana na udanganyifu unaoweza kufanywa na wateja wao wa kusafirisha dawa hizo.
Mamlaka hiyo pia imewataka wasafirishaji wa mizigo kupitia Kampuni mbalimbali Nchini,kuwa wazalendo na waaminifu kwa kutojiingiza katika shughuli za dawa za kulevya ili kulinda Afya za watanzania.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo Bw. Gerald Kusaya amebainisha hayo wakati wa ziara yake kwenye Shirika la Posta Tanzania aliyoifanya ili kujionea namna ambavyo Shirika hilo linadhibiti usafirishaji wa dawa za kulevya ambapo amesema, Mamlaka yake imejipanga vyema kuhakikisha hakuna chembe ya dawa hizo zitakazosafirishwa nchini na kwamba atakaebainika atachukuliwa hatua za kisheria.
Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya tunahakikisha tunapambana na wanaoshughulika na uuzaji na usambazaji wa dawa hizi, tunahakikisha hakuna dawa inayoingia nchini na ndio maana tumekuja hapa kuangalia mifumo ya usafirishaji wa mizigo ya Posta, nimejionea na kwa kweli wanadhibiti hali hiyo, wana mashine za kisasa amesema Kamishna Kusaya.
Naye Kaimu Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo amesema Shirika la Posta limejipanga katika kuhakikisha hakuna dawa ya kulevya inayosafirishwa kupitia Shirika hilo.
Naomba niwaambie wanaodhani hapa Posta ni mlango wa kupitishia dawa za kulevya, hapa sio mahali pake, tupo makini sana, tuna vifaa vya kisasa, tuna wataalamu wa kutosha,na ukijaribu tutakubaini haraka sana, pia tunashirikiana na mashirika ya Posta Duniani kudhibiti usafirishaji wa dawa hizi amesema Bw. Mbodo.
Shirika la Posta Tanzania na Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya Nchini wanashirikiana katika mapambano dhidi ya dawa hizo ambapo wamewafaka wafasirishaji mizigo kushirikiana nao katika mapambano hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...