Ongezeko hili la joto linatokana na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi yetu, hali inaonyesha vipindi vya jua la utosi hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari
wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa).
Katika taarifa iliyotolewa na Meneja kituo cha Utabiri (TMA) Samwel Mbuya inasema, Jua la utosi huambatana na hali ya Joto kali kwa sababu uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine. Vilevile, hali ya joto kali hujitokeza zaidi kunapokuwa na upungufu wa mvua kama ilivyo katika kipindi hiki.
Mbuya amesema, katika kipindi hiki viwango vya joto vilivyoripotiwa katika maeneo mbalimbali ni vikubwaambapo mkoa wa Kilimanjaro umeripoti kiwango cha juu cha joto kilichofikia nyuzi joto 36.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.6 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba.
"Vilevile, kiwango cha juu cha joto katika mkoa wa Dar es salaam kimefikia nyuzi joto 33.8 sawa na ongezeko la nyuzi joto 2.2 wakati katika mkoa wa Ruvuma kimefikia nyuzi joto 34.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.3.
"Hali kama hii imejitokeza pia katika mikoa yote nchini ambapo kiwango cha joto kimekuwa kikubwa
kuliko wastani wa muda mrefu huku vipindi vya joto kali vikitarajiwa kuendelea kujitokeza katika mwezi Novemba, 2021 na kupungua kidogo ifikapo mwezi Disemba, 2021 ambapo mtawanyiko wa mvua unatarajiwa kuongezeka sambamba na mionzi ya jua la utosi kuwa imeondoka katika maeneo ya nchi yetu.
Hata hivyo, Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini imetoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za mwenendo wa hali ya hewa ili kujiepusha na madhara yanayoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa ikiwemo joto kali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...