Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesisitiza haja ya mazungumzo ya wanasiasa ili kujenga maridhiano yatakayoweka mazingira bora ya kuendeleza amani na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Landmark jijini Dar es Salaam, akishiriki Kikao cha Siku mbili cha Kamati na Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo.
Amesema kama inavyostahiki kuwepo mazingira bora ya maendeleo na kujikwamua kiuchumi, taifa linahitaji amani na maridhiano ya kweli, na kwamba suala la mazungumzo baina ya wanasiasa pia likistahiki umuhimu wa pekee.
Akiongelea umuhimu wa kikao hicho, Mheshimiwa Othman ameeleza kujisikia faraja kwani ni cha kwanza kufanyika tangu Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na pia tokea alipofariki Mwenyekiti wao, Maalim Seif Sharif Hamad, huku akiutakia heri na baraka mkutano huo.
Naye Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ndugu Zitto Zuberi Kabwe ameeleza wajibu wa Chama chake katika kutetea na kuhamasisha demokrasia ndani ya Nchi, hasa kwa nafasi wanayoishikilia sasa ya kuongoza Jumuiya ya Vyama vyenye Wabunge ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayojulikana kwa jina la Taasisi ya Demokrasia.
Kikao hicho kimefunguliwa rasmi na Kaimu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Mama Dorothy Semu, ambaye amesisitiza haja ya umakini wa wajumbe hao wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Chama hicho, kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, katika kujadili mambo ya msingi yakiwemo Sera na Maamuzi muhimu pia katika kutetea umma wa Watanzania.
Wengine walioshiriki katika Mkutano huo ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wake, Ndugu Juma Duni Haji, Katibu Mkuu, Bw. Addo Shaibu, Manaibu Katibu Wakuu Tanzania Bara na Zanzibar, Bw. Joram Bashange na Bw. Nassor Ahmed Mazrui, Mwanasheria Mkuu wa ACT-Wazalendo, Bw. Omar Said Shaaban, na Mshauri wa Chama hicho, Bw. Juma Said Sanani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...