SERIKALI imesema takwimu za uwiano wa ukuzaji rasilimali kwa Pato la Taifa umekua kutoka asilimia 14.7 mwaka 1997 hadi asilimia 39.7 mwaka 2019 kiasi ambacho ni kikubwa ukilinganisha na wastani wa nchi za Afrika wa asilimia 21 – 22 na nchi zilizoendelea wa asilimia 23 hadi 25.
Hayo yameelezwa jana Jijini hapa na Waziri wa nchi,Ofisi ya waziri Mkuu (uwekezaji) Geoffrey Mwambe wakati alieleza mafanikio ya uwekezaji katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru.
Alisema,uwekezaji kutoka nje ya Nchi umekuwa ukiongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 0.73 mwaka 1996 hadi Dola za Marekani bilioni 2.18 mwaka 2013 na hadi Dola za Marekani bilioni 1.01 mwaka 2020.
Licha ya hayo amesema mafanikio katika Sekta hiyo imetokana na jitihada zake za kuweka mazingira wezeshi ya kwa uwekezaji wa ndani na ule wa kutoka nje umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka na kuleta uwiano wa pato la Taifa Tangu Serikali ilipoanza kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwekezaji na Sheria ya Uwekezaji Tanzania.
"Katika kipindi cha mwaka 1961 hadi 1996 baada ya Tanzania kupata Uhuru Mwaka 1961, Sera za Uwekezaji za Tanzania Bara zilihamasisha uwekezaji wa sekta binafsi ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria ya kuhamasisha Uwekezaji wa Kutoka Nje ya nchi ya Mwaka 1963 hadi ilipofika mwaka 1967 ilipotangaza Azimio la Arusha ambapo Serikali ilisimamia na kuendesha shughuli kuu za uzalishaji na kusababisha mvuto mdogo wa uwekezaji binafsi ikiwemo ule wa kutoka nje,"alisema.
Mbali na hayo Waziri huyo alieleza kuwa kufikia mwaka 1970 Tanzania ilikuwa inazalisha tani 202,000, mwaka 1974 tani 174,000 na mwaka 1984 tani 47,000 tu ambapo baadae ikaamriwa mashamba 12 yaliyokuwa na hali mbaya zaidi yauzwe kwa watu binafsi na wasipopatikana wanunuzi yagawiwe kwa wananchi.
"Kutokana na matatizo ya kiuchumi yaliyotokea kati ya miaka ya 1970 hadi miaka ya 1980, Serikali iliamua kurejesha Sera zinazohamasisha uwekezaji binafsi kuanzia Mwaka 1986,tija halisi ya uwekezaji (Net Investment Productivity) iliyofikia asilimia 48.6 miaka ya 1996 – 1970 ikaanza kushuka na kuwa asilimia 31.6 (1971 – 1975), 1.8 (1976 – 1980) na 18.4 (1981 – 1983),"alisema.
Alizitaja baadhi ya sababu ya kushuka huko kwa tija kuwa ilikuwa uhaba wa fedha za kigeni na matumizi haba ya uwezo wa uzalishaji (low capacity utilisation) hasa kuanzia katikati ya miaka ya 1970.
Aidha vpo Viwanda vipya vilivyowahi kujengwa ambavyo havikuzalisha kabisa, au vilichelewa sana kuanza kuzalisha na hatimaye pia vikazalisha chini ya kiwango cha uwezo kilichowekezwa.
"Uamuzi wa kusambaza Viwanda nchini ili kusawazisha maendeleo ulisababisha mara nyingine Viwanda kujengwa mahali ambapo hakuna maji, au umeme, au vyote viwili, bila kusahau hali duni ya miundombinu ya usafiri na usafirishaji,kutokana na maamuzi hayo ya kurudisha uendeshaji wa shughuli za kiuchumi kwa sekta binafsi, yalichangia ukuaji mzuri wa uchumi ambao ulifikia asilimia 4 kwa mwaka katika kipindi cha mwaka 1986 – 1995 ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 2 kwa mwaka katika kipindi cha mwaka 1981 – 1985,"Alifafanua
Waziri Mwambe pia alieleza namna Uwekezaji ulivyokuwa kuanzia Miaka ya 1990 Tanzania kuwa Serikali imefanya jitihada kubwa katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa lengo la kuvutia uwekezaji binafsi wa ndani na kutoka nje na kwamba mabadiliko makubwa ya kisera na kimiundo yalifanyika tangu miaka ya 1980.
"Maboresho hayo yanajumuisha kutungwa kwa Sheria ya Kuhamasisha na Kulinda Uwekezaji ya Mwaka 1990 (National Investment Promotion and Protection) Act 1990, ambayo ilianzisha Taasisi iliyokuwa ikishughulika na suala la kuhamasisha uwekezaji iliyojulikana kama Investment Promotion Centre (IPC),Sheria hii ilifuta Sheria ya Kuhamasisha uwekezaji wa kutoka Nje ya Nchi (Foreign Investment Protection Act of 1963),"alisema Mwambe.
Aidha alieleza kuwa Ili kuboresha zaidi sekta ya uwekezaji ,Serikali iliamua kutunga Sera ya Taifa ya Kuhamasisha Uwekezaji kwa lengo la kuvutia uwekezaji zaidi wa ndani na wa kutoka nje kwa kuongeza imani kwa wawekezaji na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji lengo likiwa ni kuimarisha matumizi ya uwezo wa nchi yetu katika kuvutia uwekezaji ikiwa ni pamoja na kushirikiana na nchi mbalimbali zilizoendelea na zinazoendelea.
"Hapa Wizara ya Mambo ya Nje na Mabalozi wana majukumu yanayosaidia moja kwa moja katika kuhamasisha uwekezaji; Kuhamasisha uzalishaji unaolenga kuchochea mauzo nje ya nchi (Export promotion) na kuhakikisha kuwa sekta ya nje inakuwa shindani na inayobadilika kulingana na mahitaji,"alisema.
Alieleza pia Majukumu ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania kuwa ni kuwahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza kwenye sekta muhimu zitakazokuza uchumi kwa haraka; Kuandaa na kusambaza taarifa sahihi kwa wawekezaji kuhusu fursa za uwekezaji pamoja na upatikanaji wa mitaji na wabia na kuwasaidia wawekezaji kupata vibali na hati mbalimbali za kisheria ili waweze kuwekeza hapa nchini.
Majukumu mengine ni kubuni mbinu za kujenga mazingira bora ya uwekezaji nchini kwa lengo la kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje; Kushirikiana na Serikali kutafuta maeneo yenye ardhi kwa ajili ya uwekezaji; Kuwasaidia wajasiriamali wadogo na wa kati katika kuibua fursa za uwekezaji kwa lengo la kukuza biashara zao na kuongeza kipato; Kufanya tafiti za uwekezaji ili kuwezesha kushauri maboresho ya mazingira ya uwekezaji; na Kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Kituo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...