Mbio
za hisani za kimataifa zilizoandaliwa na Benki ya Taifa ya Biashara
(NBC) “NBC Dodoma Marathon” zimefanikiwa kukusanya fedha zaidi ya Mil
200 kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya Saratani ya mlango wa
Kizazi kwa akina mama huku ikishuhudiwa wanariadha kutoka Tanzania
wakifanya vizuri zaidi kwenye mashindano hayo kwa kuibuka vinara kwenye
mbio za km 42 na km 21.
Katika
mbio hizo zilizofanyika jijini Dodoma hii leo na kupambwa na uwepo wa
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ilishuhudiwa
Mwanariadha Mtanzania Tumaini Habie akiiibuka mshindi wa kwanza kwenye
mbio za KM 42 upande wa wanaume baada ya kumaliza kwa muda wa saa
02:17:15, akifuatiwa na mshiriki kutoka nchini Kenya Eyanae Paul
aliyetumia muda wa saa 02:18:31.
Mtanzania Abrahamu Too alimaliza katika nafasi ya tatu kwa kutumia muda wa saa 02:19:04
Upande
wa wanawake mshindi wa kwanza katika mbio za km 42 ni Mkenya Cheruto
Isgah aliyetumia muda wa saa 02:45:03 akifuatiwa na Watanzania Jackline
Sakilu na Sara Ramadhani waliotumia muda wa saa 02:45:46 na 02:46:13
kila mmoja.
Mwariadha
wa Kimataifa kutoka Tanzania Alphonce Simbu aliibuka mshindi wa kwanza
kwenye mbio za KM 21 hizo baada ya kumaliza kwa muda wa saa 01:03:46,
akifuatiwa na watanzania wengine katika nafasi ya pili na ya tatu ambao
ni Joseph Panga pamoja na Daniel Giniki waliotumia muda wa saa 01:04:18
na 01:05:37 kila mmoja.
Upande
wa wanawake mshindi wa kwanza katika mbio za km 21 ni Mtanzania Failuna
Abdi aliyetumia muda wa saa 01:14:50 akifuatiwa na Wakenya Lelei
Jepkemboi na Tanui Euliter waliotumia waliotumia muda wa saa 01:15:18 na
01:17:21
Katika
mbio hizo ilishuhudiwa mshindi wa kwanza wa kilometa 42 kwa wanaume na
wanawake kila mmoja akiondoka na Sh milioni 5.5 huku upande wa kilometa
21, mshindi akiondoka na kitita cha Sh milioni 3.5, wakati katika
kilometa 10, mshindi alipewa Sh milioni 1.5 na mshindi wa kilometa tano
alipewa Sh milioni 1.
Akikabidhi
hundi ya mchango huo yenye thamani ya sh mil 200 kwa Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Julius Mwaiselage
pamoja na zawadi kwa washindi wa mbio hizo, Waziri Bashungwa pamoja na
kuipongeza benki hiyo kwa kuandaa vema mbio hizo alisema licha ya faida
nyingine za kimichezo umuhimu wa mbio hizo unapimwa zaidi katika lengo
lake la kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi kwa
kina mama.
“Tangu
kuanzishwa kwa mbio hizi huu ukiwa ni msimu wa pili sasa, serikali
imekuwa mstari wa mbele kuziunga mkono kutokana na dhima yake kuu ya
kuwasaidia kina mama dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi. Tunashukuru
kuona nia hiyo imefanikiwa na sasa tunakwenda kuokoa maisha ya maelfu ya
kina mama kupitia jitihada za kimichezo.’’ Alisema.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi
aliwashukuru washiriki pamoja na wadhamini wa mbio hizo kwa kufanikisha
lengo kuu la mbio hizo la kuchangia huduma za afya katika Hospitali ya
Ocean Road, hasusani matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi, ambayo
ndiyo inayoongoza kwa vifo vitokanavyo na saratani nchini.
Alisema
kupitia mbio hizo mwaka jana waliweza kukusanya fedha kiasi cha sh mil
100 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hiyo na mwaka huu lengo
lilikuwa ni kukusanya kiasi cha sh mil 200 zilizopatikana kupitia
usajili wa washiriki wa mbio hizo pamoja na michango mbalimbali kutoka
kwa wadhamini wa mbio hizo.
“Ndio
maana pamoja na yote tunatumia fursa hii kujipongeza sisi sote tukiwemo
waandaaji, washiriki pamoja na wadhamini wetu kwa kufanikisha lengo
hili muhimu. Pamoja na kwamba tumepata washindi wa mbio hizi lakini bado
kila mshiriki ni mshindi kwasababu amefanikisha kuokoa maisha ya mama
zetu,’’ alisema.
Akipokea
msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road
(ORCI), Dk. Julius Mwaiselage aliishukuru benki hiyo kwa jitihada hizo
huku akibaisha kuwa msaada huo unakwenda kusaidia mapambano hayo katika
maeneo mbalimbali hususani mikoani ili kuwahi matibabu kwa wagonjwa
ambao wamekuwa wakifika hospitalini wakiwa katika hatua ya mwisho ya
ugonjwa huo.
Awali
akizungumzia matokeo hayo Rais wa Shirikisho la Riadha Taifa (RT) Bw
Silas Isangi alisema kufanya vizuri kwa watanzania katika mbio
mbalimbali hapa nchini ni kutokana na maandalizi mazuri yanayofanywa na
wanariadha hao huku akibainisha kuwa huo ni mwanzo tu kwa kuwa matokeo
hayo mazuri ya watanzania yanatarajiwa hadi kimataifa.
Waziri wa
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa (wa tatu kushoto) akikabidhi
hundi yenye thamani ya Tsh mil 200 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Julius Mwaiselage ikiwa
ni mchangp wa mbio za NBC Dodoma Marathon ili kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa
saratani ya mlango wa uzazi kwa kina mama. Wengine ni pamoja na Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa tano kushoto)
Mshindi wa kwanza mbio za km 42 wanaume NBC Dodoma Marathon Mtanzania Tumaini Habie akiiibuka akimaliza
mbio hizo baada ya kutumia muda wa saa 02:17:15.
Waziri wa
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa (kushoto) akikabidhi zawadi ya
fedha taslimu kwa mshindi wa mbio za Km 21wanawake katika mbio za NBC Dodoma
Marathon Failuna Abdi (Kulia) zilizofanyika hii leo jijini Dodoma.
Waziri wa
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa (kushoto) akikabidhi zawadi ya
fedha taslimu kwa mshindi wa mbio za Km 21 wanaume katika mbio za NBC Dodoma
Marathon Alphonce Simbu (Kulia) zilizofanyika hii leo jijini Dodoma. Kulia ni
mshindi wa tatu wa mbio hizo Daniel Giniki kutoka Tanzania.
Waziri wa
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa (wa tatu kushoto) akikabidhi
zawadi ya fedha taslimu kwa mshindi wa mbio za Km 21 katika mbio za NBC Dodoma
Marathon Alphonce Simbu (wa pili Kulia) zilizofanyika hii leo jijini Dodoma.
Wanaoshuhudia ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na
Michezo Dkt Hassan Abbasi (Kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw
Theobald Sabi (wa tatu kulia) Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya
Michezo Bw. Yusuph Singo (wa pili kulia) na Rais wa Shirikisho la Riadha Taifa
(RT) Bw Silas Isangi (Kulia)
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa (kulia)
akikabidhi zawadi ya fedha taslimu kwa mmoja wa washindi wa mbio za walemavu katika
mbio za NBC Dodoma Marathon zilizofanyika hii leo jijini Dodoma.
Tupo tayari
kuanza mbio!
Washiriki wa mbio
za NBC Dodoma Marathon wakipoza miili yao kwenye moja ya kituo cha maji wakati
wakiendelea na mbio zao.
Waziri wa
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa akiwa kwenye picha ya pamoja na
wadau mbalimbali wa mbio za NBC Dodoma Marathon wakiwemo wadhamini wa mbio hizo
Baada ya mbio washiriki
walipata fursa ya kujipumzisha, kufahamiana na kubadilishana mawazo wakati
wakisubiri zawadi zao.
Baadhi ya
washiriki wa mbio hizo wakiendelea na mashindano
Mmoja wa
washiriki wa mbio hizo upande wa walemavu akiendelea na mashindano.
Msemaji wa Benki
ya NBC Bw William Kallaghe akitoa neno la shukrani kwa washiriki na wadhamini
wa mbio hizo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi akiwashukuru washiriki pamoja na
wadhamini wa mbio hizo kwa kufanikisha lengo kuu la kuchangia huduma za afya
katika Hospitali ya Ocean Road, hasusani matibabu ya saratani ya shingo ya
kizazi, ambayo ndiyo inayoongoza kwa vifo vitokanavyo na saratani nchini.
Mwariadha wa Kimataifa kutoka Tanzania Alphonce Simbu aliibuka
mshindi wa kwanza kwenye mbio za KM 21 wanaume NBC Dodoma Marathon baada ya
kumaliza kwa muda wa saa 01:03:46
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...