Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba J.A.M. Kabudi ametambua mchango wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto katika kutoa mafunzo ya utoaji haki nchini.

Waziri Kabudi ameongea hayo alipokuwa akihutubia kwenye mahafali ya Ishirini na Moja ya Chuo hicho yaliyofanyika tarehe 12 Novemba, 2021 Chuoni Lushoto.

Waziri Kabudi alisisitiza kuwa umuhimu wa Chuo kuwa kitovu cha kutoa mafunzo sio tu kwa Mhimili wa Mahakama, bali pia kwa Taasisi za Umma zinazohitaji elimu endelevu inayolenga kuboresha utoaji haki na usawa katika jamii.

Waziri Kabudi amewaomba wahitimu katika mahafali hayo kutumia hatua waliyofikia kuwa chachu ya kujiendeleza zaidi kwenye elimu kwani ulimwengu wa sasa unahitaji zaidi watu wenye ujuzi na maarifa ya kutosha.

Waziri Kabudi aliendelea kwa kusema kuwa tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho, mhimili wa Mahakama ndiyo mnufaika mkubwa wa zao la kitaaluma la Chuo hicho kwani mhimili huu umeweza kuendeleza watumishi wake pamoja na kuajiri mahakimu na watumishi wengine kutoka katika Chuo hiki. Aliongeza kwa kusema pamoja na hayo yote Chuo pia kimekuwa kikiratibu na kufanya mafunzo endelevu ya kujengea uwezo watumishi mbalimbali wa mahakama.

Waziri Kabudi aliongeoza maandamano na kutunuku stashahada na astashahada kwa wahitimu wa Chuo hicho pamoja na kutaja mambo sita ambayo yameipaisha Tanzania duniani na kuibuka kuwa nchi ya mfano wa kuigwa inapoelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wake.

Mambo yaliyotajwa na Waziri Kabudi ni pamoja na misingi iliyoachwa na baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kuondoa ukabila nchini na kuifanya Tanzania kuwa taifa badala ya mkusanyiko wa makabila, taifa kuingia katika uchumi wa kati kabla ya muda uliotazamiwa yaani mwaka 2025, uwezo wa taifa kudumisha na kuenzi tunu ambazo ni amani,umoja,mshikamano,utu,haki,heshima ya mwanadamu, uhuru na demokrasia. Mambo mengine aliyotaja Waziri ni uthubutu wanchi yetu kuendesha miradi mikubwa kwa kutumia rasilimali na fedha zake za ndani, uwezo wa taifa kuzifanya rasilimali zilizokuwa za Watanzania ikiwemo kuvunja mikataba mibovu ambayo haikuwa na tija kwa taifa na jambo la mwisho lililotajwa na Mhe. Prof. Kabudi ni ukomavu wa kisiasa na ukatiba katika taifa letu.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mheshimiwa Dkt. Gerald A. M. Ndika amesema Chuo kimekabidhiwa majukumu ambayo ni kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kutoa huduma za kitaalamu majukumu ambayo Chuo kinamudu kuyatekeleza kwa ufanisi.

“Sera ya mafunzo ya mahakama ya mwaka 2019 imebainisha kuwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ni kitovu na wakala wa mafunzo na utafiti wa Mahakama Tanzania na kutokana na hilo tumeendelea kuboresha utendaji kazi wa Chuo ikiwemo kurugenzi ya mafunzo endelevu ya kimahakama” amesema Dkt. Ndika.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ametaja changamoto zinazokikabili Chuo ikiwepo ufinyu wa bajeti,kutopewa kibali cha kuajiri, uchakavu wa miundombinu na uchache wa mabweni ya wanachuo.

Mkuu huyo wa Chuo aliendelea kwa kusema kuwa uchakavu wa miundombinu unatokana na majengo ya chuo kuwa makongwe ambapo yanalazimika kukarabatiwa ili kutumika kwa usalama.

Hata hivyo Mhe. Dkt. Kihwelo alieleza kwamba pamoja na changamoto zilizopo Chuo kimeendelea kufanya majukumu yake ya kitaaluma kama Chuo kilivyokusudiwa kuyafanya. Na pia aliupongeza uongozi mzima wa Mahakama ya Tanzania kwa kukiamini Chuo.


Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba J.A.M. Kabudi akiwa na wageni wengine waliohudhuria kwenye mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba J.A.M. Kabudi akihutubia kwenye mahafali ya 21 ya wahitimu wa Stashahada na astashahada ya sheria wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto

Baadhi ya wahitimu wa stashahada ya Sheria kwenye mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba J.A.M. Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa astashahada ya Sheria waliofanya vizuri kitaaluma katika masomo yao wakati wa mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
***

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...