Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WATANZANIA sote tunafahamu hatua ambazo zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha tukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akihutubia katika Mkutano Mkuu wa 26 wa athari za mabadiliko ya tabianchi (COP26) uliofanyika Glasgow, Uskochi Rais Samia Samia pamoja na mambo mengine akaiambia Dunia: "Tuko katika kipindi ambacho wakati tunapambana na athari za mabadiliko ya tabianchi bado tunataabika na changamoto kubwa ya sasa ambayo ni ugonjwa wa UVICO-19 ambayo imeangusha uchumi na kufuta mafanikio yaliyokwishafikiwa katika miongo kadhaa ya kujenga jamii zetu."
Rais Samia akasisitiza ingawa watu wengi wanachukulia kirahisi kupanda kwa hali ya joto taka Dunia wa kama moja ya athari za mabadiliko ya tabianchi bado hali ni ya kutisha kwa nchi kama Tanzania kwani hali hiyo husababisha ukame ambao ni athari mbaya kwa sekta zinazotegemea maliasili kama vile kilimo,uvuvi na misitu ambazo zinachangia asilimia 30 ya pato la Taifa na kuathiri takribani asilimia 60 ya wananchi.
Kwa kukumbusha tu wakati wa mkutano huo washiriki wamejadili umuhimu wa kutilia mkazo hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi yanayoikumbuka dunia kwa kuwa athari zake na uharibifu wa mazingira hupunguza kasi ya nchi katika ukuaji kiuchumi na hata kuhatarisha usalama wa nchi.
Rais Samia, Mama ambaye tangu umekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hakika kwa lugha ya mjini tunasema umekuwa ukiupiga mwingi sana katika kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa.Iko hivi hotuba yake kuhusu kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi Watanzania wameisikia, Afrika wameisikia na Dunia wameisikia.
Hata hivyo wakati Rais Samia akijiandaa kwenda kwenye mkutano huo mkubwa na kisha kutoa hotuba yake Oktoba 20 mwaka huu, Shirika la HakiMadini ambalo ni shirika lisilo la kiserikali liliamua kuandaa semina ya mafunzo kwa waandishi wa habari nchini Tanzania kwa lengo la kubadilishana mawazo na kujengeana uelewa kuhusu namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kuhakikisa Watanzania wanatumia nishati jadidifu zaidi kama hatua muhimu ya kupunguza uharibifu wa mazingira.
Tunafahamu namna ambavyo uharibifu wa misitu ya asili, misitu ya kupandwa inavyotekekea kwa watu kukata miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa.Tunafahamu namna ambavyo bado tunaendelea kutumia nishati ambazo zimekuwa zikichangia kuharibu maumbile ya dunia.
Hivyo, Shirika la HakiMadini kupitia watalaam wake na wadau mbalimbali wakaamua kukaa na waandishi wa habari kwa ajili ya kuwajenga uwezo na kisha tumia kalamu zao kuhamaisha jamii ya Watanzania kutumia zaidi nishati jadidifu.
Kwa mfano badala ya kutumia nishati ya mafuta mazito kuzalisha umeme, basi ni vema tukatumia nishati maji, upepo na jua kwa ajili ya kuzalisha umeme.Tunapozungumzia maji, upepo na jua maana yake tunazungumzia nishati jadidifu, nishati ambayo ni salama katika kutunza mazingira yetu, nishati jadidifu ni rafiki wa mazingira.
Mbali ya kutumia jua, upepo na maji katika kuzalisha umeme , pia kuna umeme ambao unaweza kuzalishwa kwa kutumia jotoardhi, bahati nzuri maeneo mengi ya Tanzania ambayo yamefanyiwa utafiti yamebainika kuwa na joto ardhi, upepo, maji na jua la kutosha ambalo tukiamua tunaweza kuzalisha umeme mwingi.Tena mwingi haswaa, hayo yoote tulielezwa wakati wa mafunzo hayo.
Kwa mujibu wa watalaam kutoka Wizara ya Nishati, HakiMadini na wadau wengine kutoka taasisi za umma na mashirika yasiyo ya kiserikali walieleza wazi wazi kuwa Tanzania Mungu ameibariki kuwa na nishati jadidifu katika mikoa mbalimbali, hivyo ni wakati wa kuendelea kuweka mikakati itakayofanikisha kuwa na umeme mwingi unaotokana na nishati hiyo ambayo ni endelevu na haina madhara katika sayari ya dunia.
Waandishi kama kawaida yao, walipata nafasi ya kuuliza maswali kwa lengo la kujifunza zaidi, yaliulizwa maswali mengi na katika makala haya nitaweka maswali machache tu pamoja na majibu yake yaliyokuwa yakitolewa na Kamishna wa Nishati wa Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba aliyekuja kufunga mafunzo hayo.
Miongoni mwa maswali yaliyoulizwa na waandishi wakati mafunzo hayo ,walitaka kufahamu kwanini nchi za Afrika zijikite kutumia nishati jadidifu wakati uharibifu wao ni mdogo ukilinganisha na mataifa makubwa?
Majibu ya swali hiyo kutoka kwa Mhandisi Mramba ni kwamba japo mchango wa Afrika ni mdogo katika kuharibu mazingira lakini hatua yoyote ambayo tutatua inamchango katika kuboresha mazingira ya dunia zima, hivyo ni vema tukachukua hatua ili tusipite ambako wenzetu wamepita.
Swali lingine likawa kwanini Nishati haijaingizwa gridi ya taifa?Jibu lake likawa hatua za kuhama kutoka nishati ya kawaida kwenda nishati jadidifu, kwa mtazamo wa kawaida kuwa na mchanganyiko wa aina mbalimbali za nishati ili kuwa na uwiano.Asilimia 60 inatokana na gesi, aslimia 30 maji na zilizobakia mafuta, na mchango wa nishati jadidifu ni chini ya asilimia moja, hivyo tunapaswa kuwa na mchanganyiko.
Sababu za Tanzania kuelekea katika vyanzo vingine vikiwemo vya nishati jadidifu, Mhandisi Mramba anaeleza hivi: "Tunakwenda huko kwasababu vyanzo vingine vinauharibifu mkubwa katika mazingira , nishati jadidifu inaweza kukaa muda mrefu.
Kwa mfano nishati ya gesi ina mwisho, kiwango cha maji kinapungua, hivyo kwenye mafuta yanaelekea mwisho.Iko wazi umeme unaotoka kwenye jua hautakwisha,upepo na joto ardhi vitandelea kuwepo, hivyo ni vyanzo vya uhakika vya kuzalisha umeme.
Katika majibu ya Mhandisi Mramba anasema ni kweli kuna vyanzo vipingi, upepo, jotoardhi na jua lakini ukweli umeme unaozalishwa kwa vyanzo hivi uko juu huku akifafanua , kuna kampuni siku za nyuma alikuja nchini Tanzania na kutaka kuwekeza katika jua lakini uniti moja walitaka kutoza Dola Senti 25. Hivyo umeme ulikuwa juu na haukuwa na faida.
"Ulinganisho wa bei ya umeme wa maji ambao umekuwa ukitumika kwa muda mrefu ni senti tano, gesi senti sita ,upepo senti 17 na umeme wa jua senti 20, ingawa kwa sasa bei ndio zimeanza kushuka, kwa hiyo kwa wakati huo hakukua na na sababu ya kutumia vyanzo hivyo.Lakini kwa sasa mazingira yanaruhusu."
Swali lingine likawa je watu binafsi wanaruhusiwa kuzalisha umeme unatokana na nishati jadidifu, jibu ni kwamba wote wanaruhusiwa kwani pamoja na TANESCO kuzalisha na kusafirisha umeme nchi nzima lakini ukweli kuna maeneo ambayo hadi sasa hajafikiwa,akitoa mfano hata Dar es Salaam tu kuna maeneo ambayo hajafikiwa, hivyo ni vema wakaruhusu wawekezaji binafsi wakawekeza.
Waandishi wauliza hadi sasa ni Megawati 58 tu ambazo zimeingizwa katika gridi ya Taifa na Rais Samia ameahidi ifikapo mwaka 2025 kutakuwa na Megawati 1100 ya nishati jadidifu, je itawezekana?
Mhandisi Mramba aliyekuwa mgeni rasmi katika mafunzo hayo alijibu kuna juhudi mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa. Kutakuwa na umeme mwingi unaozalisha na jua lakini katika mwaka 2022 hadi mwaka 2023 kampuni ya jotoardhi itakuwa na Megawati 300 na wakati huo huo wanahamasisha watu binafsi kuwekeza katika nishati jadidifu.
Amefafanua katika umeme unaotokana na jua walifanya utafiti kwa kuchukua ramani ya ramani ya Tanzania kuangalia maeneo yenye nishati jadidifu, karibu kila mahali nchini wanaweza kuzalisha umeme wa jua na wa kiwango kikubwa kati ya saa tisa hadi saa 10 kwa siku, na kwenye upepo mikoa mingi inzalisha ikiwemo ya Mara, Shinyanga, Mwanza , Singida, Dodoma, Njombe, Mbeya, Kilimanjaro na Arusha.
Alipoulizwa kwanini katika baadhi ya nchi matumizi ya nishati jadidifu yakiwemo sola ni kidogo , amejibu jkwenye gridi ya taifa unapoingiza umeme wa jua au upepo maana yake ni kwamba jua likiwa kubwa unaingia umeme mwingi zaidi, likipungua na umeme unapungua, ndio maana unaingizwa kidogo katika gridi.
Vipi kuhusu Nyukilia kutumika kama chanzo cha nishati ya kuzalisha umeme, amejibu kwa Tanzania hakuna sababu ya kutumia nyukilia kuzalisha umeme kwani kuna vyanzo vingine vingi vinavyotumika kuzalisha umeme."Kuna miradi ya upepo, jua, jiothemo ambazo zinakaribia megawati 5000, tuna makaa ya mawe ambayo hayajatumika kabisa, hivyo hadi kwenda kwenye nyukilia itachukua muda kidogo.
"Ni chanzo kizuri cha umeme lakini changamoto yake ni usalama, ajali inapotokea inakuwa mkubwa, kuna mahali ambapo hadi leo hata mimea haioti, hivyo ni changamoto kutumia umeme wa nyuklia.Afrika Kusini wamefunga mitambo ya nyuklia na kutumia makaa ya mawe, hivyo kwa Tanzania sioni kama kuna ulazima huo."
Katika mafunzo hayo yaliyojikita katika kuhamasisha matumizi ya nishati jadidifu kama hatua mojawapo ya kukabiliana na uharibu wa mazingira na hatimaye kusababisha mabadiliko ya tabianchi, washiriki walipata nafasi ya kushuhudia mifano mbalimbali jinsi Tanzania inavyoingia katika uharibifu mkubwa wa mazingira.
Hivyo kupitia mafunzo yale na wingi ule wa waandishi wa habari ni matumaini yetu, nchi yetu tutashirikiana na Rais Samia kukomesha uharibu wa mazingira.
Tujikite katika kutumia nishati jadidifu zaidi badala ya kutumia aina nyingine za nishati ambazo zinachangia kuharibu mazingira yetu.
Nihitimishe hivi kabla ya Rais wagu Samia kuhutubia Umoja wa Mataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi, sisi(waandishi) na Shirika la HakiMadini tulipiga kambi Bagamoyo mkoani Pwani, tulijikuta kuangalia namna bora ya kutumia nishati jadidifu kutunza mazingira kwa mustakabali mwema wa Tanzania yetu nzuri lakini na kwa Dunia kwa ujumla.
Simu 0713833822


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...