Na Amiri Kilagalila,Njombe

Wakurugenzi mkoani Njombe wameagizwa kusimamia ipasavyo fedha ambazo zimetolewa na serikali kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuhakikisha miundombunu hiyo inaendana na thamani ya fedha ambazo zimetolewa.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya katika tamasha la Njombe ya mama Samia ambalo limeandaliwa na mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa linalofanyika katika uwanja wa kituo cha zamani cha mabisi mjini Njombe,ambapo ameeleza kuwa miradi ya maendeleo ambayo inaenda kutekelezwa kupitia fedha ambazo zimetolewa ni manufaa kwa wananchi wote.

“Wakurugenzi wa halmashauri zetu zote,Madiwani tusimamie kwa karibu na kwa makini fedha hizi.Ni lazima tuypate miradi yenye kuakisi thamani ya fedha ambayo itakuwa imetumik,na wananchi katika maeneo yote tujue tuna haki ya kushiriki katika miradi hii kuhakikisha inapotokea wizi au udokozi basi taarifa zitolewe mapema ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa”amesema Rubirya

Rubirya amesema mkoa wa Njombe umepokea fedha zaidi ya bilion 20 kwaajili ya miundombinu ya barabara,huku sekta ya afya ikipokea zaidi ya bilion 15 na sekta ya elimu imepokea zaidi ya bilion 4.

“Bajeti ya matengenezo ya barabara za vijijini imeongezeka kutoa bilioni nane na milioni mi nne arobaini na nne za mwaka jana na mwaka wa fedha huu ambao tumeuanza tutakuwa na takribani bilioni ishirini na milioni mia mbili hamsini na tisa,hizi ni fedha nyingi sana”alisema Marwa Rubirya

Ameongeza kuwa “Kwenye sekta ya afya tumepokea zaidi ya bilioni kumi na tano na zaidi ya bilioni nane zinatumika kukamilisha ujenzi wa majengo katika hospitali ya rufaa,hospitali za wilaya zinaendelea kujengwa lakini zipo bilioni mbili na milioni ishirini ambazo tumezipokea kutoka sehemu ya mkopo wa fedha wa mashariti naafuu kutoka IMF ambazo zitatumika kugharamia uimarishaji wa huduma za afya,lakini kwenye sekta ya elimu tumepokea zaidi ya bilioni nne na milioni mia saba arobaini na katika mkoa mzima tutakuwa na ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya mia moja tisini na mbili”

Awali akizungumzia kuhusiana na lengo la kufanyika kwa tamasha hilo la Njombe ya mama samia,Mkuu wa wilaya ya Njombe Bi.Kissa Kasongwa amesema kuwa tamasha hilo limelenga kutoa huduma za kisheria kwa wananchi,kuhamasisha watu kupata chanjo ya corona,kutangaza vivutio vya utalii vya wilaya ya Njombe pamoja na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa fedha ambazo amezitoa kwa wilaya hiyo.

“Katika tamasha letu la siku tatu tutakuwa na dhima nne ikiwemo ya utoaji wa huduma ya kisheria pili ni uhamasishaji wa Chanjo ya Corona la tatu kutangaza uhamasishaji wa utalii Njombe na kumshukuru Rais wetu kwa fedha nyingi ambazo ametuletea wilaya ya Njombe”

Wakizungumza katika tamasha hilo Mbunge wa jimbo la Makambako DEO Sanga na Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Makambako Hanana Mfikwa wamekiri kupokea fedha kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo kwenye sekta ya afya na elimu.

Tamasha la Njombe ya Mama Samia litafanyika kwa siku tatu kuanzia leo tarehe 15 hadi tarehe 17,ambapo wananchi wenye changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi watapata nafasi ya kusikilizwa na kutatuliwa changamoto zao kupitia wanasheria zaidi ya 20 waliofika katika tamasha.
Mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya akizungumza na mamia ya wananchi wa wilaya ya Njombe waliohudhuria katika tamasha la Njombe ya mama samia linaloendela kufanyika mjini Njombe
Baadhi ya wananchi mjini Njombe waliojitokeza katika tamasha la Njombe ya Mama Samia wakiendelea kufuatilia baadhi ajenda zinazoendelea katika tamasha hilo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...