Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dkt. Juma Malik Akili amepongeza jitihada zinazoendelea kufanywa na Shirika la Bima Zanzibar (ZIC)kwa kuendelea kubuni namna mbalimbali katika kurahisisha upatikanaji wa huduma ya bima kwa wateja wake na jamii kwa ujumla, hatua aliyoitaja kuwa inakwenda sambamba na nia ya serikali katika kuboresha sekta ya Bima nchini kwa kupanua ushiriki wa wananchi katika shughuli za kibima.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa huduma ya kidijitali ya VodaBima kupitia ushirikiano wa kiutendaji baina ya Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) na Kampuni ya Vodacom Tanzania iliyofanyika visiwani Zanzibar jana, Dkt. Akili alisema hatua hiyo inadhihirisha nia ya Shirika hilo ya kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi na kuwapatia huduma ya bima karibu zaidi na maeneo yao kulingana na azma ya serikali.
“Kupitia huduma hii ya Vodabima wananachi sasa watapata huduma za kibima kwa ukaribu zaidi kupitia simu zao za mkononi na hivyo kuongeza urahisi katika upatikanaji wa huduma hiyo na kuongeza wigo wa kuwafikia wateja na wanachi kwa ujumla na hivyo kukuza sekta ya bima nchini.”
“Na hii ndio sababu nawapongeza sana ZIC kwa juhudi zao za kuendelea kuwafikia wanachi na wateja wao kwa ukaribu na huu ukiwa ni muendelezo wa jitihada walizozifanya hivi karibuni kwa kuingia kwenye makubaliano ya kiuendaji kama haya na Shirika la Posta Tanzania. Nadiriki kusema hii ni heshima na moja ya mafanikio kwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoadhimisha mwaka mmoja tangu Rais Dokta Hussen Ali Mwinyi aingie madarakani.’’ Alisema.
Zaidi, Dkt. Akili aliipongeza kampuni ya Vodacom Tanzania kwa ushirikiano huo huku akiiomba kampuni hiyo kuendelea kujitanua zaidi katika visiwa hivyo ili wananchi waendelee kufaidi zaidi huduma za shirika hilo zikiwemo zile za kibiashara na kijamii kupitia simu za mkononi.
Kwa upande wake Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dkt. Mussa Juma pamoja na kupongeza taasisi hizo mbili kwa ushirikiano huo kupitia ubunifu, alitoa wito kwa makampuni ya bima nchini kuendelea kubuni zaidi huduma mbalimbali za kibima ili kuongeza wigo wa huduma za kibima sambambana na njia (distribution channels) za kuwafikia wateja wao.
“Hiki nachokishuhudia hii leo ni mwanzo mzuri kwasababu tulianza ushirikiano na mabenki kupitia huduma za bancassurance na sasa tunaingia kwenye kampuni za simu na Vodacom wanakuwa wa kwanza kufanikisha hili nawapongeza sana! Pongezi pia kwa ZIC kwa kuchangamkia fursa hii naomba na wengine waendelee kuiga na kubuni namna zaidi ya kuwafikia wananchi kwasababu bado tupo nyuma katika ufikiaji wa huduma za kibima kwa wananchi,’’ alisema.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar(ZIC) Bw Arafat Haji alisema mbali na kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya Bima hapa nchini, hatua hiyo ni mwendelezo wa mkakati wa Shirika hilo katika kusaidia jamii kufikiwa na huduma za bima kwa ukaribu zaidi na kuongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma hiyo na kukuza sekta ya bima nchini kwa ujumla.
“Mkakati huu unakuja tukitambua fika kwamba kwasasa ufikiwaji wa huduma ya bima kwa wananchi ni asilimia 30 tu hivyo jitihada zaidi zinahitajika. Tunaamini kupitia huduma hii ya VodaBima inayotumia miundombinu bora ya teknolojia ya M-Pesa na mtandao mpana wa Vodacom ambayo inapatikana katika maduka ya Vodacom nchini kote tunakwenda kuwafikia wateja wetu kwa urahisi zaidi huku pia tukiwahakikishia usalama zaidi katika utoaji wa huduma zetu za kibima…tunaomba sana watuunge mkono!’’ alisema.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Biashara M-Pesa Bw Rashid Tulisindo alisema kupitia huduma hiyo ya VodaBima kampuni hiyo inakusudia kuziba pengo la upatikanaji wa huduma za bima kwa kutoa suluhisho la kidijitali ambalo litapunguza gharama na kuongeza upatikanaji wa bidhaa za Bima.
Alisema VodaBima inatumia miundombinu bora ya teknolojia ya M-Pesa na mtandao mpana wa Vodacom ambayo inapatikana katika maduka Vodacom nchini kote kuhakikisha usalama, urahisi wa upatikanaji wa huduma za bima.
“VodaBima ni huduma ya kwanza ya aina yake sokoni, kupitia huduma hii tunakwenda kurahisisha upatikanaji wa huduma za bima za Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) pamoja na mfumo wa kufanya madai. Kwa sasa tunatoa bima ya vyombo vya moto ikiwemo magari na pikipiki lakini tunapanga kuleta bidhaa zingine ili kukidhi mahitaji ya wateja na kwenda sambamba na mabadiliko ya soko,” alisema Tulisindo.
Hafla ya uzinduzi huo ilihudhuliwa na wadau mbalimbali akiwemo Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Kusimamia Shughuli za Bima Tanzania(TIRA) Bi. Khadija Issa Said, baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali, wafanyakazi wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) na wafanyakazi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dkt. Juma Malik Akili (wa watu kushoto) akiongoza zoezi la uzinduzi wa huduma ya kidijitali ya VodaBima kupitia ushirikiano wa kiutendaji baina ya Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) na Kampuni ya Vodacom Tanzania wakati wa hafla fupi iliyofanyika visiwani Zanzibar jana. Wengine ni pamoja na Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dkt. Mussa Juma (wa kwanza kulia), Naibu Kamishna wa TIRA Bi. Khadija Issa Said (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar(ZIC) Bw Arafat Haji (wa pili kulia) na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Biashara M-Pesa Bw Rashid Tulisindo (wa pili kushoto).
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dkt. Juma Malik Akili akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa huduma ya kidijitali ya VodaBima kupitia ushirikiano wa kiutendaji baina ya Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) na Kampuni ya Vodacom Tanzania wakati wa hafla fupi iliyofanyika visiwani Zanzibar jana.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar(ZIC) Bw Arafat Haji akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa huduma ya kidijitali ya VodaBima kupitia ushirikiano wa kiutendaji baina ya Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) na Kampuni ya Vodacom Tanzania wakati wa hafla fupi iliyofanyika visiwani Zanzibar jana.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dkt. Juma Malik Akili akionesha tuzo maalum aliyokabidhiwa na wafanyakazi wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika jitihada za kuleta maendeleo na uboreshaji huduma za shirika hilo wakati wa hafla fupi iliyofanyika visiwani Zanzibar jana.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Biashara M-Pesa Bw Rashid Tulisindo (kulia) akipokea tuzo kwa niaba ya uongozi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania kutoka kwa wafanyakazi wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) ikiwa ni pongezi kwa kampuni hiyo kwa kuunga mkono jitihada za kuleta maendeleo na uboreshaji huduma za shirika la Shirika la Bima Zanzibar kupitia huduma ya VodaBima wakati wa hafla fupi iliyofanyika visiwani Zanzibar jana.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Biashara M-Pesa Bw Rashid Tulisindo (kulia) akipokea tuzo kwa niaba ya uongozi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania kutoka kwa wafanyakazi wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) ikiwa ni pongezi kwa kampuni hiyo kwa kuunga mkono jitihada za kuleta maendeleo na uboreshaji huduma za shirika la Shirika la Bima Zanzibar kupitia huduma ya VodaBima wakati wa hafla fupi iliyofanyika visiwani Zanzibar jana.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar(ZIC) Bw Arafat Haji (kulia) akipokea tuzo kutoka kwa wafanyakazi wa shirika hilo ikiwa ni ishara ya kutambua na kushukuru jitihada zake katika kuleta maendeleo na uboreshaji huduma za shirika hilo wakati wa hafla fupi iliyofanyika visiwani Zanzibar jana.
Baadhi ya wageni waalikwa wakiwemo wafanyakazi wa Shirika la Bima Zanzibar(ZIC) na wafanyakazi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania wakifuatilia uzinduzi huo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dkt. Juma Malik Akili (Katikati walioketi) Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dkt. Mussa Juma (wa pili kushoto walioketi), Naibu Kamishna wa TIRA Bi. Khadija Issa Said (wa kwanza kulia walioketi) na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Biashara M-Pesa Bw Rashid Tulisindo (wa pili kulia walioketi) wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi pamoja na wafanyakazi wa Shirika la Bima Zanzibar(ZIC) mara baada ya kumalizika kwa hafla hiyo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dkt. Juma Malik Akili (Katikati walioketi) Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dkt. Mussa Juma (wa pili kushoto walioketi), Naibu Kamishna wa TIRA Bi. Khadija Issa Said (wa kwanza kulia walioketi) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar(ZIC) Bw Arafat Haji (kushoto walioketi) wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi pamoja na wafanyakazi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania mara baada ya kumalizika kwa hafla hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...