Na. Farida Ramadhani, MoFP, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imeipatia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kuzikopesha Halmashauri 55 kutekeleza Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi nchini.
Hafla ya utiaji Saini wa hati ya makubaliano ya fedha hizo imefanyika Jijini Dodoma kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi (Mb) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Ummy Mwalimu (Mb).
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alisema utekelezaji wa programu hiyo ni muhimu kwa Serikali hususani Wizara ya Fedha kwa kuwa utatengeneza chanzo kipya cha kodi kwa miaka inayokuja.
“Mpango huu utatupeleka katika hatua kubwa zaidi, tutaimarisha shughuli za uzalishaji kwa kutumia ardhi pamoja na kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekuwa kero kwa muda mrefu”, alifafanua Dkt. Nchemba.
Aidha aliziagiza Halmashauri zote zilizopata mkopo huo kuzitumia fedha hizo kwa kufuata miongozo, sheria na maelekezo yaliyowekwa ili kufanikisha malengo yaliyo kusudiwa na kuwa mfano bora kwa wengine wanaohitaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) aliipongeza Serikali kwa kutoa fedha hizo ambazo zitawezesha utekelezaji wa kipaumbele cha wizara hiyo cha kuendeleza miji na vijiji.
Aliahidi kuzisimamia fedha hizo kikamilifu kwa kuhakikisha zinatumika kwa malengo kusudiwa na kubainisha kuwa programu hiyo italeta matokeo chanya kwa kupunguza uendelezaji na ukuaji holela wa miji, kupendezesha mitaa na kuwa safi na salama pamoja na kuongeza maeneo ya ardhi kwa ajili ya miundombinu ya kijamii na kiuchumi.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi (Mb) alisema fedha hizo zikitumika vizuri zitalipwa kwa wakati kwa kuwa zitaziwezesha Halmashauri kiuchumi na kupata faida ya takribani shilingi bilioni 41 ndani ya miezi sita.
alisema pamoja na kuziwezesha halmashauri, fedha hizo pia zitatumika kutatua kero na dhuluma kwa wananchi na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwa wamiliki wa maeneo yaliyopimwa na kupangwa ni rahisi kukopesha kuliko wanaomiliki maeneo yasiyo rasmi.
Aliwaagiza Wakurugenzi wote wanaopata fedha hizo kutatua changamoto mbalimbali za fidia kwa wananchi wanaochukuliwa ardhi na kuwataka kuhakikisha wanatumia fedha hizo kuwalipa wananchi fidia kabla ya kuchukua maeneo yao.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanueli Tutuba alisema utoaji wa fedha hizo ni utekelezaji wa majukumu ya wizara na kubainisha kuwa miongoni mwa majukumu ya msingi ya Wizara ya Fedha na Mipango ni kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mipango ya Serikali inayowezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kuimarisha shughuli za uchumi na ustawi wa jamii, pamoja na kusimamia matumizi bora ya fedha za umma.
Fedha hizo zimetolewa kwa Halmashauri 55 zilizokidhi vigezo kati ya 78 zilipeleka mapendekezo, zilizopata fedha hizo ni pamoja na Dodoma Jiji shilingi bilioni tatu, Ilemela shilingi bilioni 3.5, Chalinze shilingi bilioni mbili na Meru shilingi bilioni 6.5.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba (katikati) akisaini
makubaliano ya utoaji wa Fedha za mikopo ya utekelezaji wa programu ya
kupanga,kupima na kumilikisha ardhi nchini.Kulia ni Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi.kushoto ni Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Ummy Mwalimu
hafla hiyo imefanyika leo November 8,2021 jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Mwigulu Nchemba akiwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi (kulia) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Ummy Mwalimu (kushoto) wakionyesha mikataba mara baada ya kusaini makubaliano ya utoaji wa Fedha za mikopo ya utekelezaji wa programu ya kupanga,kupima na kumilikisha ardhi nchini hafla iliyofanyika hiyo leo November 8,2021 jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...