MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kuwepo kwa mfumo wa udhibiti wa takataka kupitia Jaa Kuu la Kibele, ni hatua muhimu kuelekea uwekaji wa mazingira bora ya uwekezaji na maendeleo ya nchi.
Mhe. Othman ameyasema hayo leo Ofisini kwake Migombani, Jijini hapa, katika Kikao Maalum cha Tathmini ya Ziara yake ya hivi karibuni alipotembelea Jaa la Kisasa la Kibele, Wilaya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema msingi wa kuwepo mfumo huo siyo tu kuasisi sehemu ya kutupia takataka, bali pia ni kuhakikisha mbinu za kisasa zinatumika, ili kuiweka Zanzibar katika mazingira bora na kivutio kwa wawekezaji, na hatimaye kufanikisha ndoto za kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa mamlaka na wadau wote wa mfumo huo, kutumia vyema nyenzo na vifaa viliopo, pamoja na kuhamasisha upatikanaji wa raslimali muhimu, zitakazokuza ufanisi katika uendeshaji na usimamizi wa Jaa hilo, ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa, yakiwemo kuikuza Zanzibar kiuchumi yanafikiwa.
Akitoa ufafanuzi Katika namna ya kuleta ufanisi na utendaji katika jaa hilo, Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar, Mheshimiwa Mahmoud Mohamed Mussa, amesema ipo haja ya Serikali kuandaa bajeti maalum ya uwezeshaji pamoja na kuandaa mipango stahiki ili kusaidia kudumisha shughuli za usafi wa jiji.
Naye Meneja Mkuu wa Jaa la Kibele, Bw. Hassan Mohamed Ali, amesema kitengo chake ni katika fursa muhimu, hasa baada ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa katika Ripoti yake ya hivi karibuni kulitaja kuwa ni miongoni mwa majaa bora ulimwenguni, bali kutokana na changamoto nyingi zikiwemo za moto, uhaba wa vifaa, rasilimali na mfumo dhaifu wa ukusanyaji wa taka mitaani, kunapelekea kushindwa kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao.
Wengine walioshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Dokta Khalid Salum Mohamed, akishiriki pia kama Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dokta Omar Dadi Shajak, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendeshaji na Usimamizi wa Mazingira, Bw Sheha Mjaja Juma, Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa katika Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara maalum, Bw. Omar Haji Gora, Mkurugenzi wa Jiji la Zanzibar, Bw Salmin Amour Abdalla, na Mkurugenzi wa Baraza la Jiji la Zanzibar, Bw. Fadhil Abdalla.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...