Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed akikagua maeneo mbali mbali akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya Kiwanda cha Basra Textile Mills Limeted Kilichopo Chumbuni.
Wafanyakazi wa Kiwanda cha Basra Textile Mills Limeted Kilichopo Chumbuni wakiwa katika harakati za kufungasha bidhaa zinazozalishwa Kiwandani hapo.
Meneja wa Kiwanda cha Basra kinachozalisha bidhaa za vitenge na kanga akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais juu ya hatua mbali mbali zinazotumika kuzalisha bidhaa ndani ya kiwanda hicho.
UWEPO wa viwanda mbali mbali nchini vinavyozalisha bidhaa bora kutasaidia kuitangaza Zanzibar katika soko la kimaitafa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleeza hayo alipotembelea kiwanda cha Basra Textile Mills Limited kinachozalisha bidhaa za vitenge na kanga kilichopo chumbuni Jijini Zanzibar .
Mhe. Hemed alifurahishwa na hatua ya maendeleo ya kiwanda hicho katika uzalishaji wa bidhaa hizo jambo ambalo linaipelekea Serikali kuwa na Imani Zaidi na uendeshaji wa kiwanda hicho ikiwa ni miongoni mikakati ya mpango wa kukuza sekta ya viwanda Nchini.
Aidha, aliwataka wamiliki wa kiwanda hicho kuwa wabunifu ili kuongeza kasi ya ushindani sambamba na kuongeza uzalishaji Zaidi kwa maendeleo ya kiwanda hicho.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema ni jambo la faraja kuona bidhaa zinazozalishwa katika kiwanda zina kiwango bora na zinauzika katika soko la ukanda wa Afrika Mashariki hatua ambayo inaendana na kasi yaserikali ya Awamu ya Nane.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed alimtaka Meneja rasilimali watu katika kiwanda hicho kuhakikisha kuwa haki za wafanyakazi zinapatikana bila ya ubaguzi, ikiwemo suala la maslahi pamoja na kupata mapumziko kwa mujibu kanuni za kamisheni ya kazi.
Katika hatua nyengine Makamu wa Pili wa Rais alimuagiza kamishna wa kazi kuhakikisha kuwa anayafatilia malalamiko ya wafanya kazi wa kiwanda hicho na kuyapatia ufumbuzi kwa haraka ili kukuza uzalishaji na kuleta mafanikio kwa kiwanda hicho na serikali kwa ujumla.
Kwa upande wa wafanyakazi Mhe.Hemed aliwataka wafanyakazi wa kiwanda hicho kuwajibika vyema kwa kufata taratibu, sheria , kanuni na kufanyakazi kwa bidii ili kiwanda hicho kiendelee kuzalisha kama ilivyokusudiwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliahidi kuwa serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk. Mwinyi itandelea kutoa ushirikiano wake katika kutatua changamoto mbali mbali zitakazojitokeza.
Nae, Meneja wa kiwanda hicho Bwana Saleh Suleiman alisema kiwanda kinazalisha bidhaa nzuri zenye ubora ndani ya nchi za afrika mashariki, pamoja na soko la uhakika katika ukanda huo hali ambayo inapelekea hamasa zaidi kwa uzalishaji katika kiwanda hicho.
Alifafanua kwamb, licha ya mafanikio hayo bado wanakabiliwa na changamoto ya kusafirisha makaa ya mawe kutoka Songea hadi Zanzibar ambapo inawagharimu Dollar elfu mbili (2000$) sawa na million nne na nusu shilingi za kitanzania.
Akielezea hali ya ajira Kamishna wa kazi Zanzibar Fatma Iddi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa ni jambo la kuridhisha kuona Asilimia thamini ya wafanyakazi katika kiwanda hicho ni wazanzibari jambo ambalo limesaidia kufikia shabaha ya serikali kupitia ilani ya chama cha Mapinduzi ya kutoa ajira Laki Tatu.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa kiwanda hicho ndugu Said Hamza Muhamed alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa, licha ya kazi wanazoendelea kufanya kiwandani hapo bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kutokuwa na mapumziko, ukosefu wa mikataba kwa baadhi ya wafanyakazi pamoja kupewa barua za onyo mara kwa mara bila ya sababu za msingi.
Ziara hiyo ya kukagua maendeleo ya kiwanda hicho inalenga kufuatilia maagizo aliyoyatoa April 14, mwaka huu wakati alipofanya ziara kiwandani hapo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...