Mwenyekiti wa  Malkia Ladies Group, Charity Mwakalonge akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusu kuwakaribisha  wanawake kwenye Tamasha la uzinduzi rasmi wa kikundi cha Malkia Ladie Group litakalofanyika katika Ukumbi wa PTA  Sabasaba Barabara ya Kilwa siku ya jumamosi. Kulia ni Kaimu Mwenyekiti kamati ya Jamii Malkia Ladies Group, Husna Mkupete na wa pili kutoka  (kushoto) ni Mwenyekiti Kamati ya Uwekezaji, Chevawe Mberesero na wa kwanza kushotoni ni  Mwanamuziki  wa muziki wa dansi atakayetumbuiza siku ya Tamasha, Aneth Kusha.



NA MWANDISHI WETU

 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, anatarajia kuwa Mgeni Rasmi wa Kongamano la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, litakalo fanyika Jumamosi Novemba 20, kwenye Ukumbi wa PTA Sabasaba, jijini Dar es Salaam.

 

Kongamano hilo lililoratibiwa na Kikundi cha Malkia Ladies, litahusisha washiriki wanawake, na litafanyika kwa kaulimbiu ya 'Mwanamke ni Nguzo ya Uchumi, Amka Uwekeze,' huku likitumika kuzindua kikundi hicho, Kampuni ya Bima, ramani ya jengo la biashara (Malkia Woman Market Mall) na Chaneli ya YouTube (Malkia Ladies Tv).

 

Malkia Ladies ni Kikundi cha Kikoba chenye Wajumbe 34, kilichosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa lengo la kuwasaidia wanawake kupitia elimu ya fedha kwa maana ya uwekaji akiba na uwekezaji kwa maendeleo yao na familia zao.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Malkia Ladies Group, Charity Mwakalonge, alisema kongamano hilo linalenga kuwanoa wanawake juu ya namna bora ya kuanzisha na kuviendeleza vikundi kwa ustawi wa biashara na miradi wanayofanya na kuiendesha, ili vilete tija miongoni mwao.

 

"Sisi kwa mfano tuko wajumbe 34, ambako mzunguko wetu wa fedha kwa mwaka ni takribani Sh. Milioni 250 na hii imetokana na Kikundi chetu kuwa na nidhamu ya uwekaji akiba na kuanza uwekezaji kupitia fursa mbalimbali na ndipo tukaja na wazo la Kongamano hili, ili kuwasaidia wanawake wengine.

 

"Tunawakaribisha wanawake wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla, kushiriki tamasha hilo litalofanyika kwa mfumo wa Kongamano. Lengo ni kuwasaidia kujua namna sahihi ya kuanzisha na kuendeleza vikundi, pia tutachagua vikundi vitatu bora vitakavyoshiriki ambavyo kwa kuanzia tutavilea hadi vifikie kiwango kikubwa zaidi yetu.

 

"Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Jenista Mhagama, atakayeambatana na Mlezi wetu Getrude Mongella. Tuko tayari kuwapokea na kuwapa elimu wanawake wote watakaojitokeza na wito wangu kwao ni kuja kwa wingi na tunawakikishia hawatotoka bure, wataondoka na elimu kubwa itakayowasaidia kujenga na kubadili maisha yao," alisema Mwakalonge.

 

Alifafanua kuwa pia watazindua Kampuni ya Bima itakayoanza kutoa huduma hivi karibuni, ramani ya jengo la maduka 100 ya wanawake kuuzia bidhaa zao, kitabu cha fursa 50, pamoja na Chaneli ya Malkia Ladies Tv ambayo itakuwa chachu ya akina mama kupata elimu ya masuala ya vikundi na uwekezaji, itakayotolewa kupitia mada na watoa mada tofauti, akiwamo Aunt Sadaka.

 

Kwa nyakati tofauti, Husna Mkupete ambaye ni Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Jamii na Chevawe Mberesero ambaye ni Mwenyekiti Kamati ya Uwekezaji, walitoa wito kwa Wanawake mmoja mmoja ama vikundi kujitokeza kwa wingi PTA Jumamosi, ili kupigwa msasa utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao kibiashara na kijasiriamali kwa weredi na kukuza pato lao na vikundi vyao.

 

Kongamano hilo linalotarajia kuwakutanisha pamoja zaidi ya wanawake 6,000 kuanzia asubuhi hadi jioni, litapambwa na burudani kamambe kutoka kwa msanii mkali wa dansi Aneth Kushaba na The Star Band, pamoja nyota wa Bongo Fleva, Peter Msechu.




Mwenyekiti wa  Malkia Ladies Group, Charity Mwakalonge akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusu kuwakaribisha  wanawake kwenye Tamasha la uzinduzi rasmi wa kikundi cha Malkia Ladie Group litakalofanyika katika Ukumbi wa PTA  Sabasaba Barabara ya Kilwa siku ya jumamosi. Kulia ni Kaimu Mwenyekiti kamati ya Jamii Malkia Ladies Group, Husna Mkupete na kushoto ni Mwenyekiti Kamati ya Uwekezaji, Chevawe Mberesero.


 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...