Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekuwa mshindi na kupata tuzo mbili ambazo zinatolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania ( NBAA), huku Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo Jerald Kusaya akifichua siri ya ushindi huo.
Tuzo hizo ambazo Mamlaka hiyo imezipata , ya kwanza ni katika kundi la Wizara na Idara zinazojitegemea ( MDAs) za Serikali iliyoandaa vizuri Hesabu kwa viwango vya kimataifa kwa sekta za Umma( IPSAS)kwa mwaka 2020 na ya pili ni mshindi wa jumla kwa MDAs zinazotumia IPSAS kuandaa hesabu zake.
Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa washindi na kupata tuzo hizo zilizotolewa Desemba 3 ,2021 jijini Dar es Salaam ,Kamishna Jenerali Kusaya amesema mamlaka hiyo ambayo ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kazi yao siyo tu kudhihiti na kupambana na dawa za kulevya peke yake bali moja ya kazi ya msingi ni kuangalia jinsi ambavyo wanatumia vizuri rasilimali fedha zinatolewa na Rais kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.
"Haya kwetu ni mafanikio makubwa ambayo yametokana na kuweka vizuri kumbukumbu zetu za mahesabu na ndizo haswa zimetufanya tuwe washindi, "amesema Kusaya na kuongeza kuwa Mamlaka imekuwa ikipata ushindi huo kwa mara nne mfululizo.
Kuhusu siri ya ushindi,Kamishna Jenerali Kusaya amesema yeye ndiye Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo, hivyo anapotoa maelekezo yake yanasikilizwa na kutekelezwa vizuri zaidi na wale walioko chini yake kwa maana ya wahasibu na watu wote wanaohusika kutunza kumbukumbu ndani ya mamlaka na ndio maana wameendelea kufanya vizuri.
Aidha amesema kuwa jambo la msingi kwanza watu lazima wafuate maadili ya watumishi wa umma ikiwa pamoja na taratibu zote za kiofisi.
"Unapokuwa na matumizi mazuri ya kifedha ndio yanayosababisha taasisi kuwa na hesabu nzuri za kifedha, kwa watendaji wakuu tunachotakiwa kufanya kwanza kuifahamu taasisi unayoiongoza na kisha kutoa maelekezo na kuyafauatilia kwa karibu kuona kama yanafanyiwa kazi," amesema na kuongeza:
"Lazima tuzingatie sheria na miongozo ya umma.Malengo ya mamlaka hii ni kuendelea kuibuka na ushindi na kama nilivyotangulia kueleza hii ni mara ya nne mfululizo tunaibuka washindi na kwa jinsi tulivyojipanga na kuweka malengo tutachukua tena mwakani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...