CRDBii heko, vitendo mmeonyesha,
Kwa hili lenu tamko, riba hizo kuzishusha,
Kwa sasa kukopa huko, kweli kunatamanisha,
Hongera kuwa kinara, punguzo hili la riba.

Maneno ni kwa vitendo, wenzetu mmeonyesha,
Maneno bila matendo, kwa kweli huwa yachosha,
Wakopaji anza mwendo, riba zinafurahisha,
Hongera kuwa kinara, punguzo hili la riba.

Mama Samia sikia, vitendo wameonyesha,
Yale ulowaambia, riba kuanza zishusha,
Kuweza kuwavutia, wakopaji kujirusha,
Hongera kuwa kinara, punguzo hili la riba.

Wekeza kwenye kilimo, riba wameshazishusha,
Silimia tisa imo, kwa kweli yafurahisha,
Uzalishaji kilimo, uwe ni wa kuridhisha,
Hongera kuwa kinara, punguzo hili la riba.

Rais alishauri, mwezi Juni nakumbusha,
Ya kwamba kitu kizuri, riba kuweza kushusha,
Kukopa iwe fahari, kuzalisha kurudisha,
Hongera kuwa kinara, punguzo hili la riba.

Benki Kuu lisikia, mama alivyofundisha,
Kazini wakaingia, kutengeneza motisha,
Ambao unavutia, benki riba kuzishusha,
Hongera kuwa kinara, punguzo hili la riba.

Benki ziliposikia, uliosemwa motisha,
Nazo zikaahidia, mambo kuyaharakisha,
Ona sasa twasikia, benki imelianzisha,
Hongera kuwa kinara, punguzo hili la riba.

Wenye kazi si tetesi, riba huko wameshusha,
Ni jambo chanya si hasi, moyoni lafurahisha,
Wakopaji nenda kasi, kopa nenda kuzalisha,
Hongera kuwa kinara, punguzo hili la riba.

Mnaokwenda kukopa, kulipa twawakumbusha,
Msije enda kukopa, pasipo ya kurudisha,
Mikopo chechefu hapa, tusije kuizalisha,
Hongera kuwa kinara, punguzo hili la riba.

Ukichukua mkopo, katumie kuzalisha,
Ukienda kunywa dompo, hapo unajikomesha,
Kwa benki hiyo ni simpo, dhamana watatowesha,
Hongera kuwa kinara, punguzo hili la riba.

Benki nyingine zinduka, sasa tunawakumbusha,
Kokotoa kisha weka, punguzo la kuridhisha,
Pesa ziweze tumika, kukopa na kuzalisha,
Hongera kuwa kinara, punguzo hili la riba.

Kongole Mama Samia, jambo hili kukumbusha,
Hata Benki Kuu pia, kwa huo wenu motisha,
CRDBii njia, wamekwishaionesha,
Hongera kuwa kinara, punguzo hili la riba.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
 
lwagha@gmail.com 0767223602

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...