*Afafanua hatua kwa hatua ukubwa nafasi ya Rais wa nchi
*Aahidi Bunge kuisimamia na kuishauri Serikali kwa staha

Na Said Mwishehe, Michuzi TV
NAIBU Spika wa Bunge Dk.Tulia Ackson amefafanua hatua kwa hatua ukubwa wa nafasi ya Rai wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo amewataka Watanzania kufahamu kuwa nafasi hiyo ndio kubwa kuliko ya muhimili mwingine wowote uliopo nchini.

Akizungumza leo mbele ya Rais Samia wakati wa shughuli ya kuapishwa kwa mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu pamoja na viongozi wengine wateule waliapa leo Januri 10,2022, Dk.Tulia amesema kumekuwepo na upotoshaji kuhusu nafasi ya Rais.

"Mihimili yote ina kazi zake na hapa naomba nisisitize jambo moja Rais ni Mkuu wa Nchi , sasa wako watu wanachua sehemu ambayo inasema Rais ni Kiongozi wa Serikali lakini Rais ana mambo yote ni Mmkuu wa Nchi, ni Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu wa Nchi hii

"Mheshimiwa Rais nakushukuru kwa kunipa fursa hii , naamini kwa ufafanuzi huu watu watafahamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan sio tu kiongozi wa Serikali lakini yeye ni Mkuu wa Nchi kwa hiyo yeye uongozi wake hauko sawasawa na muhimili mwingine wowote uliopo hapa nchini, nimalizie kama nilivyosema tuko tayari kama Bunge kukupa ushirikiano wetu wewe kama Rais,"amesema Dk.Tulia wakati akifafanua nafasi ya Rais.

Awali Dkt.Tulia wakati akianza kutoa salamu za Bunge mbele ya Rais Samia amesema anashukuru kwa fursa hiyo ya kutoa salamu kwa niaba ya Bunge baada ya kiapo cha viongozi mbalimbali ambao wameteuliwa na Rais ili kukusaidia katika majukumu yake mbalimbali.

"Mheshimiwa Rais katika salamu zangu hizi nianze kwa kuwapongeza sana viongozi ambao umewapa heshima ya kukusaidia wewe katika majukumu yako ambayo umepewa kisheria.Watu hawa ninawapongeza sana kwasababu nyingi tu lakini leo kwasababu ya muda sitataja zote, niiseme moja.

"Kila mmoja aliyeteuliwa katika nafasi yoyote aliyoipata. Mheshimiwa Rais ameshafanya kazi katika maeneo hayo, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Afya tayari tumepata fedha nyingi katika maeneo mbalimbali ambazo tushazifanyia kazi, aliyeteuliwa katika elimu fedha zimeshakuja nyingi, kwenye utumishi mheshimiwa Rais changamoto nyingi umeshazifanyia kazi.

"Na kwenye maeneo yote nisiyoyataja, kwa hiyo ninawapongeza kwasababu mnayo sehemu ya kuanzia kusema mazuri ya Awamu ya Sita na kazi nzuri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ameifanya kwa nchi hii, lakin mheshimiwa Rais pongezi hizi nilizowapa ndugu zangu hawa ambao wamepata nafasi labda niwape ushauri mmoja, niwaombe sana kwasababu Rais amewaamini kumsaidia.

"Hizo kazi ni kazi zake na ninyi mnapoenda kuzifanya hizo kazi fanyeni kama wasaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , na si vinginevyo. Jambo la pili ambalo ningependa kulisema ni uhusiano mzuri uliopo kati ya taasisi yetu na Serikali, tumeshuhudia mambo mbalimbali tukishirikiana," amesema Dk.Tulia.

Amefafanua kwa mujibu wa Katiba ni kazi ya Bunge kutunga sheria, kuishauri Serikali, lakini pia ni kazi yao kuisimamia Serikali.Sasa yapo mazingira ambayo pengine wanatokea na watu wanafikiri kazi ya Bunge kila wakati ni kuikosoa Serikali.

"Kazi ya Bunge iko kubwa kwani uko wakati Bunge tunatakiwa kuishauri Serikali, uko wakati Bunge tunatakiwa kutunga sheria , lakini upo wakati Bunge linaisimamia Serikali, kwa hiyo kazi ya Bunge si tu kuisimamia serikali ni pamoa na hayo mengine.

"Na Mheshimiwa Rais katika kipindi chako chote tumeshuhudia namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita ikisikiliza ushauri ambao wanatoa wabunge, imekuwa ikisikiliza changamoto zinazotolewa na wabunge na imekuwa ikizifanyia kazi na kwa muktadha huo Rais mimi niseme hivi Bunge liko tayari kabisa kushirikiana na Serikali yako mambo yote utakayoleta Bungeni ili tuweze kutoa ushauri, ili tuisimamie Serikali, ili tuyatungie sheria pale panapohitajika.

"Mheshimiwa Rais baadhi ya hawa viongozi ambao wameapa leo ni mawaziri nao ni wabunge, kama sehemu ya watu wanaokuwakilisha bungeni wakisimamiwa na Waziri Mkuu tutawapa ushirikiano , pale ambapo tutaikosoa Serikali basi tutaikosoa kwa heshima lakini pia itakasolewa kwa muktadha wa Katiba inavyoelekeza."

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...