Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde amewataka Maafisa Ugani kuwa wabunifu kutumia mafunzo rejea waliyopatiwa ili kuleta matokeo chanya na tija kwa wakulima na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Mhe. Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 27 Januari, 2022 Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi alipokuwa akihitimisha programu ya Kitaifa ya mafunzo kwa maafisa ugani.

Aidha, Mhe. Mavunde alieleza kuwa programu hiyo ambayo imehusisha mafunzo rejea kwa maafisa ugani 1,350 katika Halmashauri 46 kwenye Mikoa takribani 18 nchi nzima, ni sehemu ya utekelezaji wa kipaumbele kimojawajapo cha Wizara ya Kilimo cha kuimarisha huduma za ugani nchini.

"Sisi Wizara ya Kilimo tuna imani kubwa na nyinyi maafisa ugani, hivyo niwaombe imani hiyo mkaiweke kwa vitendo katika kuwaletea matokeo chanya wakulima wetu nchini. Mimi na Mhe. Waziri wa Kilimo hatutaki kuwa viongozi wa kutoa mifano ya nchi zingine, tunaamini tunao wajibu na uwezo wa kuleta mabadiliko na tija kwa wakulima wetu. Sisi hatutaweza bila kushirikiana nanyi kwa ukaribu" alibainisha Mhe. Mavunde.

Mhe. Mavunde aliongeza kuwa suala la kuimarisha huduma za ugani ni maelekezo ya Mh Rais Samia Suluhu Hassan na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ndio maana Wizara imeongeza fedha za ugani kutoka shilingi milioni 603 kwa bajeti ya mwaka 2020/2021 hadi kufikia shilingi bilioni 11.5 mwaka 2021/2022. Aidha, alieleza kuwa changamoto ya uhaba wa vitendea kazi kwa wakulima Wizara inaifahamu, na hivi karibuni kupitia kwa Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe utaanza kufanyika utaratibu wa kuelekea kumaliza changamoto hiyo.

Vilevile, Mhe. Mavunde alitoa shukrani kwa Taasisi ya Agricultural Market Development Trust (AMDT) na kuahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na Taasisi hiyo katika kufanya mageuzi na kuboresha sekta ya kilimo nchini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma aliishukuru Serikali kwa jitihada inazoendelea kuzifanya kwenye huduma za ugani na kuwaasa Maafisa ugani kuipenda kazi yao na kuifanya kwa kujituma ili tija kwa wakulima iweze kuonekana. 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...