Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja leo ametembelea Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere lengo likiwa ni kukagua matumizi ya fedha za Mradi wa Kusimamia  na Kuendeleza Utalii Nyanda za Juu Kusini (REGROW) pamoja na kuangalia changamoto zinazoikabili hifadhi hiyo ili kuzipatia ufumbuzi.


Akiwa katika ziara hiyo amesema mradi wa REGROW ulipata fedha za mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia jumla dola za kimarekani milioni 150 kwa ajili ya kuboresha hifadhi nne ikiwamo Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa na Hifadhi ya Taifa Ruaha ambapo pia fedha hizo zitatumika kuendeleza maliasili zilizopo na kukuza utalii.

“Kwa sasa mradi huu umepokea fedha kiasi cha shilingi bilioni 7.3 ambazo zimetumika katika ununuzi wa mitambo, vifaa, magari na vitendea kazi na pia zitatumika katika kuboresha miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na shughuli nyingine za kiuhifadhi” Mhe. Masanja amefafanua.

Aidha, amewaelekeza wataalam kuhakikisha wanatumia fedha hizo ipasavyo ili kufikia malengo.

“Tumekagua na tumeridhika na matumizi ya fedha hizi lakini nawaasa wataalam kuhakikisha mnatumia vizuri fedha hizi na sisi kama wasimamizi wa Wizara hii tutahakikisha tunasimamia fedha hizi kwa nguvu zote ili thamani yake ionekane”

Sambamba na hilo Mhe. Masanja amekagua matumizi ya fedha za UVICO 19 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambapo katika Sekta ya Utalii imepata bilioni 90.2 zitakazotumika kuboresha maeneo mbalimbali ya hifadhi likiwemo eneo la Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambalo limetengewa kiasi cha shilingi bilioni 10.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masanja amewaomba watanzania kuwa wazalendo kwa kutembelea vivutio vya utalii akitolea mfano Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ambayo ina utalii wa kuvua samaki, utalii wa michezo pamoja na Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere.

Mhe. Mary Masanja yupo mkoani Morogoro kwa ziara ya kikazi ambapo atatembelea Hifadhi za Taifa za Udzungwa, Mikumi na Ruaha kukagua utekelezaji wa Mradi wa REGROW.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...