Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Mafunzo kwa Watoa Huduma za Utalii nchini kuhusu Mwongozo wa kukabiliana na janga la UVIKO-19 katika Sekta ya Utalii, Leo jijini Dar es Salaam.


NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amezindua rasmi Mafunzo kwa Watoa Huduma za Utalii nchini kuhusu Mwongozo wa kukabiliana na janga la UVIKO-19 katika Sekta ya Utalii kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Kampasi ya Bustani jijini Dar es Salaam leo.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Masanja amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo watoa huduma za utalii kuhusu  namna ya kukabiliana na UVIKO 19.

“Mafunzo haya yatawajengea uwezo watoa huduma za utalii nchini juu ya namna bora ya kukabiliana na janga la UVIKO-19 kwa kuzingatia matakwa ya kiafya na usalama pamoja na kuboresha huduma wanazotoa na hatimaye kimarisha ushindani wa nchi katika masoko mbalimbali ikiwemo kuvutia watalii wa kimataifa kuja nchini hasa katika kipindi hiki cha mtazamo mpya wa utoaji huduma za utalii na usafiri kukabiliana na UVIKO-19 yaani " the new normal of tourism and travel ” amesisitiza Mhe.Masanja.

Amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzindua Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, ambao utekelezaji wake umewezesha kufanyika kwa mafunzo hayo.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwafikia takriban watoa huduma 3,900 katika sekta ya utalii katika mikoa 26 nchini Tanzania.

Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Philiph Chitaunga amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika kuendelea kujengea imani watalii na ulimwengu kwa ujumla kuwa Tanzania imedhamiria kupambana na janga la UVIKO 19.Pia, amesema mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha kuwa Watanzania wanaofanya kazi katika Sekta ya Utalii wanakuwa salama.

Mafunzo hayo yamehusisha watoa huduma mbalimbali katika tasnia ya ukarimu na huduma za malazi na chakula kama vile katika hoteli, loji na kambi za kitalii; aina mbalimbali za waongoza watalii; watoa huduma katika shughuli za utalii wa kupanda mlima, uwindaji wa kitalii na utalii wa utamaduni; wakala wa safari za kitalii; wakala wa usafiri wa anga; na wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wanahusika na kutoa huduma.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizindua  rasmi Mafunzo kwa Watoa Huduma za Utalii nchini kuhusu Mwongozo wa kukabiliana na janga la UVIKO-19 katika Sekta ya Utalii.
Afisa Biashara wa Mkoa wa Dar es Salaam Thabit Massa akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo na kueleza kuwa Mkoa huo umekuwa na utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara na kuwapa elimu ya afya juu ya UVIKO-19 na namna ya kujikinga na kuwakinga wengine sambamba na kutoa chanjo.
baadhi ya washiriki wakifuatilia mada katika mafunzo hayo.
Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...