Na Mary Gwera, Mahakama

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi amezindua rasmi Bendera na Nembo ya Mahakama ya Tanzania katika sherehe za uzinduzi wa Wiki ya Sheria zilizoanza leo tarehe 23 Januari, 2022 jijini Dodoma.

Mahakama ya Tanzania kama ilivyo mihilimi mingine imepata Bendera na Nembo yake, hatua ambayo itasaidia kuitangaza na wadau kuijua zaidi Mahakama.

Akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa upatikanaji wa Bendera na Nembo ni sehemu ya mafanikio ya uboreshaji wa huduma mbalimbali unaoendelea mahakamani.

“Mahakama ya Tanzania imefanya uboreshaji wa huduma mbalimbali ukilenga wananchi na wadau. Mojawapo ya uboreshaji wa huduma za Mahakama ni pamoja na kupatikana kwa Bendera na Nembo yake ili kuendelea kuutangaza vyema Mhimili huu,” alisema Mtendaji Mkuu.

Aidha, Prof. Ole Gabriel alieleza kuwa Mahakama imepitia hatua nyingi za kiserikali kuandaa Bendera na Nembo yake ikiwa ni pamoja na kushirikisha wadau mbalimbali katika usanifu, kutoa maoni na hatimaye kupitishwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na kutolewa kwenye Tangazo la serikali (GN) Na. 787 la tarehe 26 Novemba, 2021.

Aliongeza kuwa mchakato uliowezesha Mahakama kupata Bendera yake umeanza mwaka 2003, yapata miaka 19 hadi sasa ambapo Mwaka 2004 Mahakama ilianza kutengeza sanamu ya Nembo ya Mahakama na kuikamilisha Septemba 2006 na baabaye mchakato wa Bendera ukaendelea kwa kusimamiwa na Majaji Wakuu waliokuwepo kwa nyakati tofauti na kukamilishwa na Mhe. Prof. Ibrahimu Juma, ambaye ni Jaji Mkuu wa sasa.

Alibainisha kuwa Sanamu ya nembo ya Mahakama ipo kwenye jengo la Mahakama ya Rufaa, Dar es Salaam. Nembo ya Mahakama ni yenye alama ya “Lady Justice” aliyeshikilia Kitabu na Mzani. Kitabu kina maana ya matumizi ya sheria katika maamuzi ya haki; na Mzani una maana ya upimaji na ulinganifu wa ushahidi kwa nia ya kutoa haki sawa kwa watu wote.

Kwa upande mwingine, Bendera ya Mahakama ina alama ya Duara ya Bendera ya Taifa na katikati ina Nembo ya Mahakama. Nje ya duara kuna maneno “The Judiciary of Tanzania” na chini yake kuna maneno “Mahakama ya Tanzania.”

Rangi ya Bendera kwa ujumla wake ni “nyekundu” ikiwa ni alama ya mamlaka yenye maamuzi ya mwisho ya utoaji Haki.

Upatikanaji wa Bendera na Nembo ya Mahakama vitatumika kuitangaza na kiutambulisha mahakama. Nembo itatumika kwenye nyaraka mbalimbali za kiofisi kama barua (Letter heads), ‘Dairy’, Kalenda, ‘notebooks’ ‘minute sheets’ na fulana ‘T-shirts’.

Kabla ya zoezi la uzinduzi, Rais Dkt. Mwinyi alizindua Wiki ya Sheria kwa kuongoza matembezi maalum yaliyoanzia Mahakama Kuu-Kanda ya Dodoma na kuhitishwa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini humo.

Katika matembezi hayo Rais Mwinyi aliambatana na Mwenyeji wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, baadhi ya Majaji wa Mahakama, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Mhe. Jacobs Mwambegele, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi na wadau wengine wanaoshiriki katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoanza kuanzia leo tarehe 23 Januari, 2022 hadi tarehe 29 Januari, 2022.

Mbali na Mahakama, Wadau wengine wanaoshiriki katika Maonesho hayo yanayobebwa na kaulimbiu ya Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho Kuelekea Mahakama Mahakama Mtandao’ ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) na wengine.

Hafla za kilele cha Siku ya Sheria nchini itafanyika kitaifa katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma tarehe 01 Februari, 2022 ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi akipandisha bendera ya Mahakama ya Tanzania kuashiria uzinduzi rasmi. Hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika leo tarehe 23 Januari, 2022 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma. Wanaoshuhudia uzinduzi huo ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto), Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (wa tatu kulia) na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansansu.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi (kulia) akifunua kitambaa kuashiria uzinduzi rasmi wa Nembo ya Mahakama ya Tanzania. Hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika leo tarehe 23 Januari, 2022 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma. Anayeshuhudia zoezi hilo kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria ulioenda sambamba na uzinduzi wa Bendera na Nembo ya Mahakama katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...